The House of Favourite Newspapers

MSHTUKO MUME ADAI MADAKTARI KUUA MKEWE NA MTOTO

MSHTUKO! Chrispine Mtuta, mkazi wa Mbezi- Kwembe jijini Dar, ameibuka na tuhuma nzito za kushtua kwamba, madaktari wamechangia kifo cha mkewe, Paulina Patrick.  Paulina alikata roho Julai 24, mwaka huu katika Hospitali ya…. (jina linahifadiwa kwa sasa), yeye na mtoto wake mchanga akiwa kwenye harakati za kujifungua.

Mume wa mwanamke huyo anautaja uzembe wa madaktari kwamba ndiyo uliosababisha mkewe na mtoto wake kupoteza uhai, jambo ambalo mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo alipozungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda alisema; “Tuhuma hizo si za kweli.”

PAULINA ALIFIKAJE HOSPITALINI HAPO?

Akizungumza na waandishi wetu, Mtuta alisema alimpeleka mkewe huyo kwenye hospitali hiyo baada ya kupatiwa rufaa kutoka Hospitali ya Medwil iliyopo Kibaha, Pwani alikokuwa akihudhuria kliniki.

“Siku ya Jumatano (Julai 17) mke wangu alikwenda kupima kwenye Hospitali ya Medwil, majibu yakawa ni kwamba presha yake iko juu na wakatushauri kumpeleka Hospitali ya… (anaitaja) kwa ajili ya tiba na uchunguzi zaidi. “Kwa kuwa siku zake za kujifungua zilikuwa zimefika pia ikabidi Jumamosi (Julai 20) tumpeleka huko baada ya kupatia rufaa,” alisema Mtuta.

LAWAMA KWA MADAKTARI

Mtuta aliwaambia waandishi wetu kuwa baada ya kumfikisha mkewe hospitalini hapo madaktari hawakumpatia tiba mkewe kwa haraka kama ilivyoshauriwa na wenzao wa Medwil alikotokea.

“Siku ya kwanza, ya pili hakuna kilichokuwa kimefanyika zaidi ya kuwekewa vidonge walivyodai vitasaidia kumvuta mtoto. “Siku ya tatu hali ya mke wangu ilizidi kuwa mbaya, tukauliza kwa nini hafanyiwi upasuaji hatukupata jibu, siku ya nne alfajiri ndiyo wakamuwekea dripu ya maji ya uchungu; sasa huu kama si uzembe ni kitu gani?” Alihoji Mtuta.

DADA WA MAREHEMU

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda kwa masikitiko makubwa, dada wa marehemu aitwaye Agatha Patrick alisema mdogo wake alikuwa mjamzito aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo la presha. “Baada ya madaktari wa Medwil kuonesha kushindwa kumudu tatizo la mdogo wangu aliniambia ameambiwa aende Hospitali ya… (anaitaja jina), lakini mimi nilikataa, nikasema bora aje Hospitali ya Mwananyamala, Dar.

“Akasema acha tu akatibwe huko, alipofika ndiyo uzembe wa kumpatia matibabu ulipojitokeza; amelazwa siku nyingi bila kuhudumiwa. “Siku walipoamua kwenda kumfanyia upasuaji kwa ajili ya kumtoa mtoto walikuwa wamechelewa, matokeo yake tukapoteza mtoto na mama,” alisema dada huyo wa marehemu akiendeleza tuhuma dhidi ya madaktari.

WAPEWA KICHANGA KINYEMELA

Katika hatua nyingine, dada huyo wa marehemu alieleza kuwa wahudumu wa hospitali hiyo waliwapatia kinyemela mwili wa kichanga kilichotolewa baada ya kupasuaji.

“Walituambia mtoto alikuwa amefia tumboni siku nyingi, wakasema haina haja ya kuupeleka mwili wake mochwari, wakatupatia kwenye kanga na kutuambia tutoke nao bila walinzi kujua tukauzike nyumbani,” alisema dada huyo wa marehemu na kuongeza kuwa walishangazwa na mwili huo kujaa majeraha yakiwa bado mabichi.

DAKTARI WA HOSPTALI AFUNGUKA

Baada ya waandishi wetu kupokea rundo la lawama kutoka upande wa ndugu wa marehemu Paulina kwamba walikwenda ofisi ya uhusiano wa hospitali hiyo ili kuweka mzani wa kihabari. Hata hivyo, huko hawakupata majibu badala yake mmoja wa maofisa habari aliwachukua waandishi wetu na kuwapeleka kwa dokta wa magonjwa ya akina mama wajawazito ili aweze kuziongelea tuhuma hizo za uzembe.

“Nakiri kumpokea Paulina Patrick siku ya Jumamosi na alikuja akiwa presha yake iko juu.“Kutokana na hali hiyo tukaamua kumpa huduma ya kushusha presha kwanza kabla ya kumfanyia chochote. “Tulipojiridhisha kuwa presha yake iko sawa, tukaamua kumfanyia operesheni kwa kuwa njia ya kujifungulia ilikuwa imegoma kufunguka.

“Hata hivyo, baada ya operesheni hiyo ilionekana kwamba mtoto ameshafia tumboni muda mrefu; tulijitahidi kumhudumia mama; maana baada ya kumfanyia operesheni aliendelea kutokwa na damu nyingi kuliko kawaida, jambo ambalo liliwalazimu madaktari kumrudisha tena kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili operesheni nyingine ambayo ilishindikana na mama akapoteza maisha.

“Sasa kama ndugu wanasema ni uzembe, hapana; hakuna uzembe wowote kwa upande wetu,” alisema daktari huyo wa magonjwa ya akina mama

Comments are closed.