The House of Favourite Newspapers

Mshua, Tupe Mizigo Yetu!

0

mpekeWiki iliyopita nilikuwa Mtwara natafuta fursa ili nami niwe pedeshee, nilipe kodi na nimiliki kavideo-kwin ka nguvu niweke heshima mtaani. Unajua mwaka jana ilikuwa ukitaka kuweka heshima uwe na Bongomuvi, mambo yameshageuka sasa ni ishu ya videokwin.

Ndo hivyo tena wiki iliyopita nilienda Mtwara kuzitafuta za kununulia kavideokwin. Nilipomaliza mishemishe zangu nikaingia kwenye basi moja kurudi Dar. Kabla ya safari kuanza trafiki mmoja akaingia kwenye basi na kutoa maneno ya busara kwetu wasafiri, kuwa tukiona dreva anaenda mwendo mbaya tumtaarifu konda amshitue apunguze mwendo, ikishindikana abiria wapige simu namba zilizokuwa zimewekwa mbele yetu.

Ndipo akaingia dreva wetu, jamaa mjanjamjanja hivi, ile kuingia tu kwanza akavua shati, mie nikashituka kidogo, akawasha gari tukaondoka. Ile tupo bado Mtwara mjini, hiyo spidi yake utadhani kabanwa na tumbo anakimbilia choo mtaa wa sita.

Kiukweli tumbo likaanza kunisumbua kwa woga, nikawa najiuliza tutafika kweli leo? Ina maana nitakufa kabla ya kumiliki kavideokwin? Watu wote tulikuwa kimyaa kama tunasubiri hukumu, mama mmoja jasiri akamwita konda na kumwambia amwambie dreva huo mwendo haufai.

Kimoyomoyo nikamuunga mkono yule mama. Dreva akapunguza spidi, lakini sasa akawa anaenda mwendo wa kobe, hata wenye baiskeli wakaanza kutupita. Dahh sasa kitendawili tumwambie akimbize au tukubali mateso ya kuingia Dar baada ya siku mbili?

Kulikuwa na kundi la wavuta bangi viti vya nyuma wakalianzisha, si wakaanza kumtukana yule mama aliyetaka spidi ipungue, ndio maana nawaita wavuta bangi, badala ya kuonyesha hasira zao kwa dreva wakaanza kumlaani yule mama kwa nini alilalamika. Kimoyomoyo nikawa namuunga mkono yule mama lakini naogopa kusema, si ndio zetu Wabongo, tunaumia lakini tunaogopa kusema.

Basi liliendelea mwendo wa jongoo mpaka tukafika mwisho wa safari. Dreva katukomoa kwa kulalamikiwa kuwa anakimbia mno, najiuliza tu hivi huyu namshitaki kwa nani na kosa lake linakuwa lipi? Kuendesha basi kwa mwendopole?

Nikaingia mtaani kwetu saa saba usiku na mizigo, vibaka wakanipokea utadhani tulikubaliana niwaletee wao, maana walikuja kundi kama watu saba hivi wakaniambia, ‘Mshua hebu tupe hiyo mizigo yetu uliyotuletea’ Sikubisha nilikuwa kimya kama nilivyokuwa kwenye basi.

Leave A Reply