The House of Favourite Newspapers

Msuva amvuruga Pluijm

Msuva..Simon Msuva.

Sweebert lukonge, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Dar Pluijm hivi sasa anaumiza kichwa ili kuhakikisha kikosi chake kinafanya vizuri zaidi katika mechi zake zijazo za Ligi Kuu Bara ambayo itaanza tena kutimua vumbi Desemba 12 mwaka huu, lakini winga Simon Msuva ndiye anayemuumiza kichwa zaidi Mzungu huyo kwa sasa.

Msuva ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu baada ya kufunga mabao 17, hajafanikiwa kuonyesha kiwango chake msimu huu, hatua ambayo ilisababisha asotee benchi lakini ameibukia kwenye michuano ya Chalenji nchini Ethiopia na amekuwa akifanya vyema huko.

Kutokana na hali hiyo, hivi sasa Pluijm anaumiza kichwa akifikiria ni jinsi gani atalazimika kukibadili kikosi chake pindi michuano ya ligi kuu itakapoanza kutimua vumbi tena ili Msuva ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Malimi Busungu awe anaanza kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema kuwa anavutiwa vilivyo na kiwango cha Msuva anachokionyesha katika mashindano hayo ya Chalenji ukilinganisha na wachezaji wengine wa timu hiyo.

“Nafurahia kumwona Msuva anafanya vizuri katika michuano hiyo, ni jambo zuri kwani linanifanya na mimi kuumiza kichwa kwa ajili ya ligi kuu kwa sababu siku zote nahitaji wachezaji wanaofanya vizuri.

“Kuhusu nafasi ya Msuva katika kikosi changu cha kwanza, hilo ni jambo jingine ila ninachoweza kusema ni kwamba ninafurahishwa na kiwango anachokionyesha, namwomba aendelee kufanya vizuri zaidi kwa sababu mchango wake pia bado unahitajika kwa kiwango kikubwa katika kikosi changu,” alisema Pluijm.

Mpaka sasa Msuva amesha-zifumania nyavu mara mbili katika mashindano hayo ya Chalenji, sawa na John Bocco pamoja na Elias Maguri, lakini pia amete-ngeneza nafasi mbili za mabao.

Kilimanjaro Stars itavaana na Ethiopia katika robo fainali ya michuano hiyo leo Jumatatu.

Comments are closed.