The House of Favourite Newspapers

Mwamuzi Aliyepigwa Tanga Atoka Hospitali

YULE mwamuzi aliyechezea kichapo kutoka kwa mashabiki wa Coastal Union, Jumapili iliyopita, Thomas Mkombozi ameripotiwa kuendelea vizuri kiafya baada ya kupatiwa matibabu hospitali na amesharuhusiwa kutoka.

Mkombozi alipata mkong’oto huo kwa kupigwa na magongo na makonde kutoka kwa mashabiki hao mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza baina ya Coastal ya Tanga dhidi ya KMC ya Dar es Salaam, uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Coastal ilifungwa mabao 3-2.

Msimamizi wa Kituo cha Tanga, Khalid Abdallah ameliambia Championi Jumatano kuwa tetesi zinazosambaa kuwa mwamuzi huyo alipoteza fahamu na hakujitambua mpaka alipofika hospitali si za kweli na kwamba alifanyiwa matibabu siku hiyohiyo kwa kushonwa jeraha lake la kichwani na kuruhusiwa.

“Mimi nilikuwa naye (Mkombozi) tangu tunampelekea hospitali, mpaka anatibiwa na kushonwa kichwani kutokana na jeraha alilopasuka kichwani, akaruhusiwa kwa maana hakukuwa na haja ya kulazwa kutokana na hali yake, baada ya hapo tukaenda polisi na kisha hotelini kwake.

“Si kweli kwamba alizimia, alikuwa anaelewa kila kitu kinachoendelea, kwa sababu tulikuwa na waamuzi wengine na tulikuwa tunaongea naye kama kawaida, isipokuwa tunaweza kusema anaumwa kutokana na majeraha lakini kwa kifupi yupo vizuri na anaendelea vizuri kwa sasa,” alisema Khalid.

Kutokana na tukio hilo, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia kwa Ofisa Habari, Alfred Lucas, limeweka wazi kuchukuliwa hatua na kutolewa maamuzi na Kamati ya Saa 72.

Na Hans Mloli, Dar es Salaam

Comments are closed.