The House of Favourite Newspapers

Mwanamke agongwa na gari la ‘Freemason’

0

morogorohospital-990x743Stori: Dustan Shekidele, Wikienda

MOROGORO: Wananchi wa Mtaa wa Mtawala Kata ya Mji Mpya Manispaa ya Morogoro mkoani hapa, wamelizingira gari la matangazo ya kujiunga na jamii ya Freemason wakitaka kulichoma moto kufuatia dereva wake kumgonga Janeth Ngolika muuza mbogamboga mitaani.

Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita maeneo hayo ya Mtawala ambapo mashuhuda, Asha Juma na John Lazaro walikuwa na haya ya kusema:

“Huyu mwanamke alikuwa na kapu lake la mboga, wakati anakatiza barabara ghafla lilitokea gari la matangazo ya Freemason likiwa mwendokasi na kumgonga kisha nalo likatumbukia mtaroni,” alisema John.

Kwa upande wake Asha alisimulia: “Nimeshuhudia hili gari (Toyota Noah) la matangazo ya Freemason likimgonga na watu kutaka kulichoma moto kwa sababu yule mama aliumia sana na alikuwa akitokwa damu usoni.”

Mwandishi wetu alilishuhudia gari hilo likiwa na ‘chata’ za Freemason likiwa mtaroni hapo kwa muda mrefu huku dereva wake akitokomea kusikojulikana. Baada ya kuondoka eneo la tukio, mwanahabari wetu alitinga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kumkuta Janeth akiwa hoi kitandani.

Akizungumza na Wikienda kwa tabu, mwanamke huyo alieleza mkasa huo: “Nilikuwa kwenye biashara yangu ya kuuza mboga. Nilipofika maeneo ya Mtawala niligongwa na gari na kupoteza fahamu hadi nilipozinduka nikiwa hapa (hospitalini).”

Kwa takriban mwezi mzima sasa, gari hilo limekuwa likizunguka mitaani mjini hapa likiwahamasisha wananchi kujiunga na kundi hilo.

Leave A Reply