Mzunguko wa Kwanza Wala Vichwa vya Makocha 9 Bongo

LIGI Kuu Tanzania Bara kwa sasa inazidi kuchanja mbuga ikiwa ipo kwenye mzunguko wa kwanza, ushindani umekuwa mkubwa kwa timu zote huku jumla ya makocha tisa mpaka sasa wakiachana na timu walizoanza nazo kazi kutokana na sababu mbalimbali.

 

Timu ya kwanza kuachana na kocha msimu huu Bongo ilikuwa ni Alliance FC ya Mwanza baada ya kocha wake Athuman Bilal kuanza kwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbao akiwa nyumbani, alifungashiwa virago jumla kwa kile kilichoelezwa kuishindwa falsafa ya Alliance na kwa sasa ipo chini ya Habib Kondo.

 

Amri Said wa Biashara United alifuata kuachana na timu hiyo kabla ya kuthibitishwa hivi karibuni kwamba ameachwa, kwa sasa timu ipo chini ya Francis Baraza.

Mwinyi Zahera wa Yanga baada ya kuchapwa na Pyramids nje ndani kwa jumla ya mabao 5-1, safari yake ikaishia hapo na timu akakabidhiwa Boniface Mkwasa.

 

Mwingine ni Jackson Mayanja wa KMC kwa sasa timu ipo kwa Mohamed Ally, pia Juma Mwambusi wa Mbeya City alijiuzulu kutokana na timu kuwa na mwenendo mbovu kwa sasa Mohamed Kijuso ameishikilia timu.

 

Malale Hamsini wa Ndanda kutokana na mweneo mbovu alisimamishwa na inaelezwa kuwa Amri Said atapewa mikoba yake rasmi.

Patrick Aussems kocha wa Simba aliyeipeleka timu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, amesimamishwa jumla na inaelezwa kuwa Seleman Matola atabeba mikoba yake.

 

Felix Minziro, kocha wa Singida United, aliachwa na mikoba yake ipo kwa Ramadhan Nswanzurimo.

Etienne Ndayiragije wa Azam FC yeye amejiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania nafasi yake ndani ya Azam FC imechukuliwa na Aristica Cioaba.

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment