The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani – 22

0

ILIPOISHIA:
“Samahani, kwani hapa Kenya mrembo una muda gani?”
“Kama wiki na nusu hivi,” Papaa alijibu kwa kukisia.
“Ni kama ulivyosema?”
“Ndiyo.”
“Basi nina imani kazi itakuwa nzuri.”
SASA ENDELEA…

Baada ya muda nilifuatwa na yule dada aliyekuwa amevaa kitawa na kupelekwa chumbani ambako nilielezwa nioge nipumzike nimsubiri Papaa. Nilikwenda kuoga na kujifunga taulo kisha yule dada aliniletea glasi kubwa lililokuwa limejaa bia na kunikaribisha.
“Karibu mpenzi.”
“Asante.”
“Nilisahau kukusifia, umependeza sana.”
“Asante.”
“Basi mi  nipo nje.”
“Sawa aliniaga na kuondoka, nikiwa chumbani peke yangu nikinywa bia, nilijikuta nikiwa na maswali mengi juu ya kikao kile ambacho kilinijadili bila kujua walilenga kitu gani juu yangu japokuwa sikuwa na wasiwasi na chochote kitakachoamuliwa bila mwenyewe kushirikishwa.
Kwa vile nilivuta mipaka kutafuta pesa ili siku moja nirudi nyumbani kwetu kama mfalme, niliamua kusubiri kujua kikao kile kinahusiana vipi na mimi.
Niliendelea kunywa mpaka Papaa alipokuja na kunitaka tukaoge pamoja kisha tulifanya yetu na kupumzika. Tukiwa tumepumzika kila mtu akiwa amelalia mgongo macho yakiwa juu, Papaa alinisemesha.
“Konso.”
“Abee.”
“Jiite mtu wa bahati.”
“Kwa nini?”
“Yaani kupita kwenye kikao kizito kama kile bila kukosolewa.”
“Wangeanzia wapi kunikosoa, labda kazi yangu ya kuuza mwili, si katika sura na umbile, kwa siku moja niliyosimama barabarani nilijifananisha na mbingu na wenzangu ardhi.”
“Kwa nini?”
“Jibu unalo tafuta swali lingine.”
“Sasa sikiliza,” alisema huku akijisogeza kwenye ukuta na kukaa kitako na kunifanya na mimi niamke na kukaa kitako ili tuweze kusikilizana.
“Konso, unafaa kuwa mama wa nyumbani kwa nini uliingia kwenye biashara hii?”
“Ni historia ndefu.”
“Kwani ilikuwaje?”
Nilimwelezea makosa niliyofanya nikiwa chuo kikuu yaliyosababisha kuwa mbali na wazazi, nusu nilimweleza ya ukweli lakini mengine nilijaza chumvi.
“Ha! Kumbe Konso wewe ni msomi wa chuo kikuu?”
“Ndiyo, lakini tamaa iliniponza na ulimbukeni ndiyo ulionifikisha hapa, leo hii nimekuwa sina mwelekeo. Pamoja na kujitambua mrembo tena msomi, nimekuwa nikiandamwa na mikosi kila kukicha. Inaonekana ni laana ya wazazi wangu, naamini sitafanikiwa,” nilisema kwa uchungu.


Si mikosi bali moyo wako ndiyo unaamini hivyo, siku zote laana ya mtu hutokana na yeye mwenyewe na si mzazi wake. Hakuna mzazi anayemuombea mabaya mwanaye, bali kila kukicha hukuombea akili yako ijitambue na kuweza kurudi nyumbani kwa kujutia makosa yako.
“Hata Bwana alisema kondoo mmoja aliyepotea ni muhimu kuliko walio zizini kwa vile walio zizini hawahitaji kutafutwa wapo salama hivyo wasiwasi wote ni kwa kondoo aliyepotea huenda akaliwa na mbwa mwitu.”
“Kwa hiyo unataka kuniambia yanayonitokea si laana ya wazazi wangu?”
“Mzazi hawezi kumlaani mwanaye aliyepotea bali humuombea kila siku arudi kundini.”
“Samahani naomba kukuuliza kitu kabla hujaendelea na unachotaka kuniambia.”
“Niulize tu.”
“Ninyi ni kina nani, mnafanya kazi gani?  Maana mnanichanganya sana.”
“Usiulize sisi uliza juu yangu mimi.”
“Mimi ni mtume na nabii.”
“Mtume na nabii?” niliuliza kwa sauti kidogo kuonesha nimeshtuka.
“Ndiyo mbona unashangaa?”
“Mtume na nabii, kiongozi wa dini?”
“Ndiyo.”
“Sasa mbona maneno yako yana tofauti kubwa na vitendo?”
“Nilijua lazima utaniuliza swali hilo, lakini kwa vile tupo pamoja utajua vitu vingi, pia nakuona Konso wa mwaka mmoja unaokuja mbele kama mwanamke tajiri mwenye kanisa kubwa lenye kufanya muujiza mkubwa utakaotikisa dunia.”
“Mmh! Makubwa mimi Konso niwe tajiri mkubwa tena namiliki moja ya makanisa makubwa nchini Kenya? Nitaanzia wapi wakati najiona sina chembe ya ucha Mungu.”
“Konsooo, kwa vile upo na mimi nitakutumia kutengeneza pesa ambazo hukuwahi kuziota ndotoni.”

Makubwa, nilijikuta njia panda juu ya kauli za Papaa kuwa ndani ya mwaka mmoja nitakuwa tajiri mkubwa mwenye kanisa langu huku nikitenda miujiza itakayoitikisa dunia. Bado kwangu niliona mauzauza kutokana na kauli zake juu ya ucha Mungu wake na matendo yake kwenda tofauti.
Usikose mwendelezo wake katika gazeti la risasi jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply