The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani 34

0

ILIPOISHIA:
“We nani?” aliuliza kwa sauti kubwa.
Nikijifanya mapepo yamenipanda nilimvamia Mtume Mutombo kwa kushika vazi lake kwa nguvu mpaka nikalichana. Kwa vile nilikuwa kazini nilifanya nilichoelekezwa kwa ustadi mkubwa ili ionekane pepo langu lina nguvu kuliko  yote  yaliyotangulia.
SASA ENDELEA…

Nilikamatwa na walinzi wenye nguvu na  kukandamizwa chini huku mchungaji akienda kubadili nguo. Baada ya muda Mtume Mutombo alibadili nguo na kuvaa suti safi iliyompendeza sana.
Alipofika alinimwagia maji, kumbuka kila kitu kilikuwa kimepangwa nami niliimeza scripti kisawasawa nilikuwa kama masanii wa Holly Wood niliyekuwa nikitafuta tuzo ya msanii bora wa mwaka ya Oscar. Baada ya kumwagiwa maji alisogea pembeni na kutoa amri.
“Muachieni.”
Waliponiachia nilinyanyuka nilipokuwa nimelala chini kwa kujizoazoa na kuanza kumfuata tena Mtume Mutombo huku nimemtolea macho na kupiga kelele kama naungua. Nilikuwa kama mzimu uliofufuka na kufanya kila mmoja kuhamishia mawazo yake kwangu, lilikuwa tukio la kusisimua pale kanisani.

Mtume Mtombo alisema kwa sauti:
“Tokaaaa pepo mchafu.”
“Sitokii,” nami nilijibu kwa sauti, huku nikimfuata kama kuna kitu kinanizuia.
“Tokaaa,” alirudisha mkono kama ananitupia kitu na kunifanya niyumbe kidogo kisha niliendelea kumfuata.
“Sitokiii,” niliunguruma kwa sauti kubwa mpaka nikahisi koromeo linawaka moto.
“Kwa jina la Yesu Kristu, pepo mchafu toookaaaa,” alisema baada ya kuutoa mkono nyuma kama anaongeza nguvu kisha kunitupia nami nilijirusha nyuma kwa nguvu kama nimepigwa na kombora nikijua kuna watu watakuwepo kunidaka.
Kwa jinsi nilivyojirusha kama wasingenidaka ningepasua kichwa. Baada ya kunidaka walinilaza chini nami nilitulia pale chini kama nimepoteza fahamu. Mtume na Nabii Mutombo alisema waniache. Aliachana na mimi kama hakuna kilichotokea kisha aliendelea na mahubiri.

Baada ya dakika ishirini nikiwa bado nimelala chini, alinigeukia na kunimwagia maji aliyosema ya baraka lakini yalikuwa ya kawaida, kisha alisema:
“Mnyanyueni.”
Wasaidizi wake walininyanyua, baada ya kufanya hivyo nilijifanya kujishangaa kujikuta mbele ya umati wa watu kanisani.
Kisha nilirudisha macho yangu kwenye mwili wangu na kuonesha kuyashangaa mavazi yaliyokuwa nimevaa na kuuuliza nipo wapi na kuanza kulia.
“Ooh! Nyamaza dada yangu, uko katika mikono salama,” aliniambia Mtume Mutombo kisha aliuliza:
“Kuna mtu anayemfahamu huyu?”
“Sisi,” walijitokeza kila Doi ambao walikuwa katika mavazi ya kuvutia.
Walipofika mbele Mtume Mutombo aliwauliza:
“Mnamfahamu vipi huyu?”
“Ni ndugu yetu.”
“Aleluya hili ni jambo la kushangaza kumbe tuna waumini humu ndani lakini wana ndugu zao wana watatizo. Dada aliyekuwa mgonjwa anaitwa nani?”
“Konsolata.”
“Hili tatizo alikuwanalo kwa muda gani?”
“Huu ni mwaka wa tatu sasa.”

“Wooo! Kwa nini hamkumleta muda wote huo?”
“Huwezi kuamini, tumetua hapa jana usiku tulipanga kusali katika kabisa hili ili tuanze kumsaka kwa vile alitoweka katika mazingira ya kutatanisha.”
“Kwani ninyi mnatokea wapi?”
“Lokichokio .”
“Ha! Mbali sana, amewezaje kufika Nairobi akiwa katika hali hii?”
“Hata sisi tunashangaa.”
“Mmeishawahi kumpeleka kwenye maombi?”
“Ndiyo lakini mara nyingi hutulia tu kisha hulipuka tena na kutoroka, tumeangaika sana. Ila kwa zaidi ya wiki mbili tulikuwa hatujui yupo wapi.”
Usikose mwendelezo wake katika gazeti la risasi jumamosi.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply