The House of Favourite Newspapers

Nelly Muosha Magari wa Posta-25

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale fundi Yassin alipomwambia Nelly asiwaze sana kuhusu kumsimamisha kutokwenda site na kumweleza akipata kazi katika site nyingine wataenda wote. Je, kilifuatia nini? Songa nayo…

Alipoambiwa hivyo, si akakumbuka kwamba Doreen alimpatia simu ambayo mpaka muda huo hakumuonesha fundi Yassin akajikuta akiachia tabasamu lililoonwa na fundi.
“Vipi naona umefurahi!” fundi Yassin alimwambia.

Kutokana na kauli hiyo, kumzuga fundi wake, Nelly alimwambia alimfurahisha sana alipomwambia atakapoanza kwenda kwenye site nyingine wataenda wote.

“Ndiyo hivyo, siwezi kukutupa mdogo wangu,” fundi Yassin alimwambia Nelly bila kujua mwenzake alifurahi kukumbuka alikuwa kapewa simu ambayo ingemsaidia kuwasiliana na mpenzi wake Doreen.
Wawili hao walipotosheka kwa kinywaji waliondoka na kuelekea nyumbani, walipokaribia Nelly alimwambia fundi wake kwamba anakwenda kumsalimia rafiki yake Ipyana ambaye hakuonana naye kama siku nne hivi.

“Dogo ukiwa na hela hutulii, au unakwenda kuongeza mbili za kulalia nini?” fundi alimwuliza.
“Hapana, naenda tu kumwona mshikaji wangu huenda atanipa mchongo wa kazi maana kuanza kushinda nyumbani bila kazi kwa mtoto wa kiume haipendezi,” Nelly alimwambia.
Kutokana na maneno ya Nelly, fundi alimfagilia na kumweleza alikuwa na mawazo mazuri, akamwambia waonane kesho jioni ili ajue alifikia wapi.

“Poa bro wangu, kanisalimie shemeji yangu,” Nelly alimwambia.
Walipoachana, kijana huyo alikwenda kwenye genge la Chinga akamwambia amkatie tango, Chinga akamtania kwamba mambo yake yalikuwa mazuri maana kila jioni alikuwa akipasha kilaji.
“Hamna bwana, rafiki yangu kanipa tubia tuwili sasa kwenda homu na harufu ni so kwa washua,” Nelly alimwambia wakati huo alikuwa akila ndizi mbivu.

Alipomaliza kula ndizi na tango akaenda nyumbani kwa akina Ipyana na kumkuta akiwa ameketi kwenye moja ya matairi ya gari waliyoyafukia ardhini nyumbani kwao kuzuia magari yasipite.
Marafiki hao walipoona walifurahi sana, katika maongezi yao Nelly alimsimulia kila kitu Ipyana kuhusu kule site na alivyosimamishwa kwenda.

“Da! Wewe kweli balaa, siku mbili tu za kwenda site umempata mtoto wa kishua na kakupa hadi simu, kijana unatisha,” Ipyana alimfagilia Nelly.

“Si unajuaga mambo yangu, mimi huwa sirembi hata siku moja, sasa unafikiri mtoto kajipendekeza mwenyewe mara sijui maziwa, mayai sijui mazagazaga gani, sasa ukimuacha mtoto kama huyo si utapata dhambi za bure kaka!” Nelly alimwambia Ipyana wakaishia kucheka.

Baada ya mazungumzo, Ipyana alimwuliza Nelly kama anaweza kujitoa ufahamu ili siku iliyofuata waongozane kwenda Posta kufanya kazi ya kuosha magari ya wafanyakazi wa serikali, wafanyabiashara na mabosi mbalimbali.

“Kaka kwa hali ilivyo sasa sichagui kazi kinachotakiwa ni kupata fedha tu, wewe unafikiri kama nisingeenda na fundi Yassin kule site ningempaje mtoto wa kishua Doreen aliyenipa hii simu kali?” Nelly alimwambia Ipyana, wakacheka.

“Kama ndiyo hivyo basi poa sana, wewe si unaona jinsi geto langu lilivyo na kila kitu cha maana na ninavyopiga pamba za kishua, kazi ya kuosha magari hiyo kaka!” Ipyana alimwambia Nelly.
“Hivi kazi ya kuosha magari inalipa eh?” Nelly alimwuliza.

“Kaka acha, kwa siku mimi kurudi homu na shilingi ishirini na tano hadi thelathini ni jambo la kawaida, halafu kule dili zipo kibao mfano bosi anaweza kukutuma sehemu ukirudi anakupa teni au zaidi,” Ipyana alimwambia Nelly aliyeishia kushangaa.

“Ipyana bwana si ungeniambia muda mrefu nami saa hizi si ningekuwa na geto kali kama lako na watoto wakali wangenikoma?” Nelly alimwambia.Ipyana alicheka sana na kumweleza kwa jinsi alivyokuwa akimuona sharobaro alijua asingeweza kufanya kazi ya kuosha magari ndiyo maana hakumwambia.

“Kaka kama ndiyo hivyo kesho mimi na wewe mguu na njia hadi Posta, kweli jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza, kumbe kila siku unapiga hela ya maana namna hiyo?” Nelly alimwuliza Ipyana.
“Ndiyo hivyo, kikubwa ni kuchakarika tu, wewe kesho twende nikakufundishe kazi,” Ipyana alimwambia.

Baada ya kukubaliana siku iliyofuata kwenda Posta, waliagana ndipo Nelly akaenda kwao na kuwakuta wazazi wake wakiwa wanamalizia kula, walisalimiana kisha akaenda kuoga.
Kwa kuwa alikuwa ameshiba, mama yake alipomwuliza suala la msosi alimwambia kuna sehemu walipitia na fundi Yassin wakala ndipo mama mtu akamwuliza kuhusu kazi.

Aliwaambia ilikuwa nzuri kisha akaenda chumbani kwake akachukua shilingi elfu kumi na tano na kumkabidhi mama yake akamwambia kesho yake anunue mboga.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni tumia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply