The House of Favourite Newspapers

Ni sahihi kuoana kwa sababu ya UJAUZITO?

WAKATI wa kuongeza kitu ubongoni kuhusu uhusiano na mapenzi umewadia. Ni imani yangu kuwa kila wakati umekuwa ukijifunza mambo mbalimbali kupitia kona hii. Karibuni sana.  Nakwenda kwenye mada; nazungumzia suala la mimba. Hivi, hujawahi kusikia msichana akilazimishwa kuolewa kwa sababu amepata mimba? Je, hujawahi kusikia msichana aking’ang’aniza ndoa baada ya kuwa amepata mimba?

Bila shaka ni mambo ambayo umekutana nayo katika jamii inayokuzunguka. Kama halijawahi kukuta moja kwa moja basi hata kwa ndugu, jamaa au rafiki zako. Hilo ndilo nililolipa nafasi ya kulijadili leo katika ukurasa huu.

Kwa bahati mbaya sana wengi wetu tumekuwa na tabia ya kujadili mambo ambayo tayari yameshakuwa matatizo. Hapa namaanisha kwamba, baada ya tatizo kutokea ndipo tunapotafuta ufumbuzi. Mfano, wasichana wengi siku hizi huwa hawajali sana suala la matumizi ya kondom kwa sababu tu tayari ameshafahamiana na patna wake kwa muda wa miezi miwili mitatu – tayari wameshaaminiana!

Jambo hili siyo sawa kabisa na ndiyo maana leo tunajadili jambo hili. Unajua wanawake wakati wakikubali kukutana na wenzi wao bila kinga wala tahadhari yoyote huwa hawafikirii kabisa suala la kupata ujauzito lakini ikishatokea ndiyo wanatafuta utatuzi.

Ndugu zangu, kuna utatuzi gani hapo zaidi ya kuzaa? Hapo sasa ndipo linapoibuka suala la baadhi kukimbilia kutoa! Athari zake hapo ni nyingi na leo sitazingumzia kwanza.

ANGALIA MFANO HUU:

Tusiende mbali sana, ngoja nikupe ushuhuda huu; wasichana nane kati ya 10 wanaonipigia simu kuomba ushauri, katika maelezo yao huwa wanaeleza wazi kuwa hawatumii kinga yoyote wala tahadhari ya kujihami na mimba.

Sababu nyingi zinazotolewa na wasichana hao ni kwamba wanaaminiana. Wengine huthibitisha kuwa wameshafanya hadi kipimo cha ukimwi hivyo hakuna shaka ya kutumia kinga. Ukiuliza kuhusu mimba, hubaki kujiumauma!

TAZAMA SASA…

Hapa namzungumzia mwanamke ambaye tayari ameshapata ujauzito kabla ya ndoa. Ni mimba ya boyfriend tu. Hapa ndipo mahangaiko yanapoanzia.

Msichana anahaha, tena mbaya zaidi wazazi au walezi wake wanakuwa wameshatambua kuwa binti yao ni mjamzito.  Swali la kwanza binti kuulizwa na wazazi wake litakuwa: “Hiyo mimba ni ya nani?” Akimtaja tu baasi! Atapelekwa mkuku huko au atafukuzwa na kutakiwa aende kwa mwanaume wake au busara itatumika kuzikutanisha familia mbili lakini lengo likiwa moja, vijana hao waunganishwe.

NI SAHIHI?

Kwa hakika siyo sahihi hata kidogo. Kwa maamuzi ya haraka mzazi anaweza kuona njia nyepesi ya kumuondolea aibu nyumbani kwake ni kumuoza au kumpeleka binti yake kwa mwanaume aliyempa mimba lakini athari zake ni nyingi – tutaziona baadaye.

Suala la kuoana ni maridhiano ya ndani. Inawezekana vijana hao kwa kudanganyana kwao au kwa kutokuwa makini kumewafanya wajikute tayari wapo kwenye matatizo. Inawezekana kipaumbele cha uhusiano wao haikuwa ndoa.

Vijana wanapaswa kupewa muda wa kutafakari kwanza tatizo ambalo limejitokeza ambalo kwa hakika limetokea kwa uzembe wao wenyewe. Nasema uzembe kwa sababu kwanza hairuhusiwi watu walio nje ya ndoa kukutana kimwili.

Pili, pamoja na kukiuka utaratibu huo hawakuwa makini kujikinga na upatikanaji wa mimba hiyo. Hilo ni tatizo lao ambalo wanapaswa kujadiliana pamoja. Si ajabu uhusiano unaweza kuwa mzuri kwa binti kupata matunzo mazuri na baadaye kujifungua kisha taratibu nyingine (kwa hiyari yao) za ndoa zikafuata wote wakiwa na furaha na tendo hilo.

Si jambo zuri mwanamke kujipeleka kwa mwanaume kwa sababu tu amepata mimba. Vilevile si sahihi kumfukuza binti au kumlazimisha mwanaume aliyempa mimba aishi naye tena wakati mwingine bila ya ndoa kwa sababu tu amepata mimba.

Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE! Joseph Shaluwa ni mshauri wa uhusiano na maisha anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vilivyopo mitaani. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA.

Comments are closed.