The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-9

Ilipoishia wiki iliyopita
Kijasho kikanitoka, nikafikiri jinsi gani ningeweza kufanya, nikaona hapa njia rahisi ni kurudi tena kwa rafiki yangu aliyenishauri kuhusu suala hili. Nikatoka kwa mganga na moja kwa moja nikaelekea Masuguru, ambako nilitaka nikapate ushauri mpya kwa sababu bado nilihitaji utajiri.
Sasa endelea…

“Niliondoka na kutafuta usafiri wa Masuguru ili nikaweze kupata ushauri mpya. Nilipofika kule kesho yake, Jerry alikuwa bado hajafika, hivyo nami nikaunga moja kwa moja kuanza kununua madini ili atakapokuja anikute nikiwa na mzigo tayari.

Baada ya siku tatu hivi akina Jerry waliwasili pale machimbo na kama ilivyokuwa kawaida, mimi ndiye nilikuwa mtu wao wa kwanza ili wajue kiasi cha mzigo nilichokuwanacho, nikawaeleza na tukazungumza biashara mambo yakaisha.

Jioni ya siku hiyo nikiwa sehemu ya kunywa bia, niliamua kumweleza Jerry ishu nzima jinsi ilivyokwenda bila kumficha hata kitu kimoja, jambo ambalo lilimshangaza sana, kwa sababu aliniambia katika waganga ambao anawaamini basi yule wa Ngende ni namba moja na akasema kama ni kweli vile ndivyo ilivyokuwa, basi hata yeye angenishauri niachane na utajiri wa madawa na badala yake nibadilishe biashara nyingine ili nisake mafanikio.

Nilimweleza wazi jinsi gani sikuwa tayari kuachana na mpango ule, nikamwambia huenda mambo yalikuwa mabaya tu kwa mganga, maana niliamini wapo waganga wengine wanaoweza kufanikisha. Jerry hakuweza kubisha sana, lakini akasema yeye hawezi kuniongoza tena katika suala lile kwa sababu mtu pekee aliyekuwa akimuamini ni yule mganga wa Ngende.

Tulipokubaliana tuliendelea kunywa bia kila mmoja akiwa na akili yake, kichwani mwangu sikukubali kushindwa, nilishasikia simulizi kadhaa za waganga wa kienyeji na nilidhamiria kufanya kadiri niwezavyo kuhakikisha ninampata mmoja wao ili anipatie utajiri niliouhitaji.

Kesho yake majira ya mchana, niliondoka machimboni Masuguru kuelekea Songea mjini, ambako nilifika kama saa kumi hivi. Nikaulizia magari ya Iringa, nikaambiwa kwa muda ule nisingeweza kupata, labda hadi kesho yake asubuhi au nipande magari ya Njombe ambayo yalikuwepo, huenda pale ningeweza kubahatisha ya Iringa.

Nikaona ushauri mzuri, nikajipakia kwenye Hiace moja iliyokuwa inajaza na mara tu tukaondoka na kufika njombe majira ya saa nne usiku. Sikutaka kulala, lengo langu lilikuwa ni kufika Wilaya ya Makete, maana kuna jamaa zangu wengi waliwahi kuniambia kuwa kule kuna wataalam wengi wanaoweza kugeuza mambo kama ninayohitaji kwa ufanisi mkubwa.

Muda ule nilibahatika kupata Land Rover ambalo lilikuwa linajaza abiria, nikajumuika nao na saa saba hivi usiku, ndipo tulipoingia Makete. Nilipata nyumba ya kulala palepale maeneo ya stendi na hadi kunakucha, kichwa changu kilikuwa na mambo mengi ambayo sikuwahi kuyafikiria kabla.

Asubuhi kulipokucha, nilioga kisha nikaanzisha stori na mhudumu wa pale gesti, nikijifanya nabadilisha mazungumzo kutoka huku hadi kule, lengo langu lilikuwa ni kutaka kujua kama ningeweza kumpata mganga ambaye angenisaidia shida yangu.

atika mazungumzo yetu, hatimaye nikafanikiwa kumwingiza kule nilikokuwa nataka.
Akaniambia kama kuna sehemu yenye waganga wengi wanaoweza kuwapa watu utajiri wa haraka, basi ni Makete, kwa sababu kwa macho yake alishuhudia vijana wengi wakibadili maisha yao kwa namna ya kustaajabisha sana na alipouliza kilichotokea, walisema ni ushirikina.

Kwa jinsi nilivyomdadisi, alifanikiwa hadi kunieleza kuhusu mganga mmoja anayesifika sana kwa kazi hiyo, aliyemtaja kuwa anakaa kijiji kimoja kinachopakana na Mkoa wa Mbeya. Kimoyomoyo nikajisemea huko ndiko nilitaka kwenda na kupanga siku iliyofuata alfajiri kuanza safari!

Je, ilikuwaje kesho yake? Usikose kufuatilia mkasa huu wa aina yake katika toleo lijalo.

Comments are closed.