Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani-11
ILIPOISHIA:
Nilipofika nyumbani nilikuta pigo jingine baadhi ya vitu vyangu na pesa vilikuwa vimeibwa. Nakumbuka siku niliyotekwa mlango wa chumbani sikuufunga. Ilionesha mlinzi baada ya kujua nipo kwenye hali gani aliamua kuniibia na kutoweka.SASA ENDELEA…
Nilizidi kuchanganyikiwa baada ya kugundua pesa zilizokuwa kwenye kabati zilichukuliwa baada ya kuvunja kabati. Lilikuwa pigo lingine kwangu! Yasikie tu kwa mtu siyo yakukute.
Nilichanganyikiwa mtoto wa kike nusra ninywe sumu, lakini wazo lile nililipinga kwa kuamini bado kuna maisha mengine. Nilijikuta nikijawa na mawazo mengi kwa kuamini hali ilikuwa mbaya baada ya kuandamwa na mikosi juu ya mikosi pia biashara yangu ya kujiuza kwa upande wangu ilikuwa imeisha haribika.
Baada ya kuumwa na nyoka sikutaka kurudia makosa kutembea na wanaume za watu. Lakini tatizo likabakia kwa vile wateja nitakaokutananao ilikuwa vigumu kujua kama wameoa au laa hivyo nilijua kutembea tena na mume wa mtu ni kuhatarisha maisha yangu.
Nilimuogopa mume wa mtu kama kifo baada ya kukutana na balaa ambalo sitalisahau mpaka naingia ardhini. Kwa vile biashara ile ilikuwa imeishaingia shubiri na wakati huo sikuwa na kitu kingine cha kuniingizia pesa hivyo lazima mji ningeuona mgumu sikuwa na hamu tena ya kuendelea kuwepo mjini.
Wazo lililonijia ni kurudi kwa wazazi wangu niwaombe msamaha ili nizaliwe upya kwa kuamini mtoto akinyea mkono haukatwi na pamoja na kuwakosea bado nilibakia mtoto wao japokuwa niliondoka nyumbani zaidi ya miaka saba bila kuaga.
Niliamua kuuza vitu vyangu vyote na kuamua kurudi nyumbani, baada ya kukata tiketi siku ya pili alfajiri nilikuwa Ubungo na kuingia basi la kuelekea nyumbani kujisalimisha kwa wazazi wangu. Wakati huo kumbe shetani alikuwa hataki nivunje naye ndoa.
Ndani ya basi nilishangaa kumuona shoga yangu niliyekuwa nafanya naye kazi ya kuuza mwili tuliyepotezana miaka kama miwili. Alionekana amependeza kuonesha mambo yake safi, aliponiona alishtuka.
“Ha! Konso ni wewe?”
“Ni mimi shoga,” nilisema huku nikikumbatiana naye.
“Kumbe tupo safari moja?”
“Ndiyo.”
“He! Za siku?”
“Nzuri kiasi,” nilijibu kwa upole.
“Njoo tukae hapa.”
“Si pana mtu?”
“Akija atakaa siti yako, nina mengi ya kuzungumza na wewe muda mrefu hatujaonana shoga.”
“Mmh! Ni kweli.”
Japokuwa namba ilikuwa tofauti na siti yangu tulikubaliana kumhamisha mwenye namba ya jirani na shoga yangu Doi kama akitokea. Baada ya kukaa alitaka kujua sababu za kuwa katika hali ile.
“Vipi mbona hivyo? Ulikuwa unaumwa?” alionesha kunishangaa kwa vile afya yangu aliifahamu vizuri.
Kwa vile alikuwa shoga yangu nilimweleza kila kitu kilichonitokea, baada ya kunisikiliza, kwanza alinipa pole na kuniuliza:
“Kwa hiyo ndiyo unarudi nyumbani?”
“Ndiyo shoga nakwenda kuomba msamaha kwa wazazi najua nimewakosea sana sijui watanipokeaje,” nilizungumza kwa sauti ya huruma.
“Je, wakikukatalia?”
“Mmh! Hata sijui.”
“Siyo hujui wakikukatalia utafanyaje?” shoga yangu aliniuliza swali lililotaka jibu makini.
“Nitaondoka sasa nitafanyaje.”
“Utakwenda wapi?”
“Nitajua hukohuko baada ya kukataliwa.”
“Sasa sikiliza wewe huna mkosi bali ulijichanganya mwenyewe, kwa uwezo uliokuwa nao hukutakiwa kufikia hatua hii. Ulijua kabisa una wanaume wa nje tena wanaokuweka mjini ilikuaje ukakifuga kibwana uchwara kisicho na mbele wala nyuma matokeo yake kimekuharibia kila kitu.
“Kama ulivyosema yule jamaa yako Mwarabu alivyokuwa anakuhudumia na kutaka akuoe sasa ulikataa nini?”
“Dini.”
“Shoga unachekesha mwenye dini huuza mwili wake, shoga duka la pesa ulilipiga teke.”
“Sina jinsi imeishatokea.”
“Ulitakiwa kukifukuza kile kibwana au kukipa uhuru wa kuishi kitakavyo mbali na wewe na kukitumia siku ukishikika.”
“Mm! Shoga yote hayo sikuyajua.”
“Kingine ulikosea kuwa na wateja wa kudumu, biashara yetu inataka mkimalizana na mtu hamjuani, akija tena kesho huyo mteja mpya siyo kukufanya anakujua sana.”
“Sikujua shoga, niliamini kuwa na waume wa watu ni afadhali kuliko kupigwa baridi na kung’atwa na mbu.”
“Dada wee, biashara ya usiku kupigwa na baridi na kung’atwa na mbu ndiyo raha yake kama mnywa kahawa ya moto na kuungua vidole kwani wauza kahawa walishindwa kuuza kahawa kwa vikombe vya mikono walijua watamaliza raha. Ingekuwa kazi nyepesi wengi tungekuwa nao uvumilivu wa kung’atwa na mbu na kupigwa baridi ndiyo mtaji wake. ”
“Basi ndiyo hivyo, nimechemka nimeamua kurudisha majeshi nyumbani.”
“Sikiliza Konso kilichotokea ni ajali kazini hukutakiwa kurudi nyumbani zaidi ya kubadili mji.”
“Kuna mji gani mkubwa wenye biashara kushinda Dar?”
“Ungeenda machimboni kwa umbile lako muda mfupi ungetengeneza pesa za ajabu.”
“Kwani wewe sasa hivi uko wapi?”
“Mimi niko kwa baba Moi.”
“Ndiyo wapi?”
“Jijini Nairobi tunakula vichwa, tena nimekumbuka itabidi twende wote achana na mawazo ya kurudi nyumbani bado una nafasi ya kutengeneza pesa na kurudi nyumbani ukiwa vizuri heshima itakuwepo.”
Je, kiliendelea nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.