The House of Favourite Newspapers

Oyaa wadada wa redio, dili hilo!

0

UZURI wa sie Wabongo tunajali sana ndugu zetu, na hasa sie wa kizazi cha zamani ambao bado tuna mawasiliano na ndugu zetu kijijini. Tunajua kabisa usipomtendea vizuri ndugu yako toka kijijini, akirudi huko anaweza akatengeneza mambo fulani, ukaanza kuandamwa na mikosi isiyoeleweka.

Ukiona kila ukipanda daladala lazima ugombane na konda ujue kijijini wameshafanya mambo, ukiona kila siku lazima uibiwe, ujue kijijini tayari wamekutenda, ukiona wananchi wanakutuhumu kuwa wewe ni jipu ujue kijijini wameshafanya mambo.
Hata kama wewe dreva wa bodaboda ukaona kila siku unakoswakoswa na ajali ujue kijijini ndugu zako wameshakufanyishia. Hivyo ni muhimu kujali shida za nduguzo kwa usalama wako. Sasa wiki iliyopita mtoto wa shangazi wa jirani na rafiki yake mama mdogo kule kijijini, ghafla waliweza kufika kwangu.
Nilifurahi kwa kuwa nilipata stori nyingi za kijijini, kuna mwenyekiti mpya, mwalimu mkuu kamuoa bibi afya, mzee mwenye duka kaoa mke wa 12, ila stori zilikata ghafla, nilikosea nikawasha runinga, ndugu yangu huyu akaacha kuongea akili yake yote ikawa kwenye runinga.
Majibu yakawa ya mkatomkato tu, nikalazimika kuizima niendelee kupata habari motomoto toka kijijini, unajua sijafika huko mwaka wa ishirini sasa.
Hatimae ikafika wakati wa kumuuliza ndugu huyu sababu ya kuja mjini, hii ni muhimu maana hapo ndipo utakapojua namna ya kujipanga, ujue anakaa siku ngapi kwako. Ndugu yangu huyu akaniambia kuwa amekuja mjini kutafuta mchumba. Nilishtuka maana ninavyojua mimi watu wanaenda kijijini kutafuta wachumba huyu mbona anafanya kinyume?
Nikaanza kusikiliza kwa makini nimuelewe. Ndugu yangu akaniambia kuwa yeye ni msikilizaji mzuri wa vipindi vya redio. Na kwa kweli lafudhi ya Kiswahili na sauti nyororo za watangazaji wa kike kwenye vipindi vile vya mipasho imemteka kabisa hivyo aliona aje mjini ili akimpata mmoja wa watanganzaji hawa amuoe ampeleke kijijini.

Kwanza itakuwa sifa kwake kuwa na mke mwenye sauti nyororo na Kiswahili kilichonyooka, pili amekuwa akiwasikiliza wanavyotoa ushauri kuhusu maisha ya ndoa, ameona kuoa mke wa namna hiyo ndoa yake itakuwa raha mstarehe. Tayari amekwisha tayarisha ng’ombe sita kwa ajili ya mahari, kimsingi yuko vizuri. Jamani watangazaji wa kike dili hilo, tumeni maombi kwangu.

Leave A Reply