The House of Favourite Newspapers

PanAfrican Energy kusaidia watoto wenye saratani Lindi

Mkurugenzi Mtendaji wa PAET, Andy J Hanna (kulia) na Mwenyekiti wa bodi ya TLM Gerald Mongella (kushoto)  wakisaini mkataba wa makubaliano kusaidia watoto wenye saratani mkoani Lindi.

Kampuni ya uzalishaji gesi ya PanAfrican Energy Tanzania Limited (PAET) imesaini mkataba wa makubaliano (MoU) na Shirika la kuhudumia watoto wenye saratani la Tumaini la Maisha (TLM) kwaajili ya kusaidia utoaji wa huduma za matibabu kwa watoto wenye saratani katika Hospitali ya rufaa ya Sokoine mkoani Lindi. Makubaliano hayo yalisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa PAET, Andy Hanna na Mwenyekiti wa bodi ya TLM, Gerald Mongella ambapo pande zote mbili zilieleza kuwa na imani na hatua hiyo ambayo ni mwanzo katika kufikisha huduma hiyo katika maeneo mengine ya nchi.

“Ushirikiano huu utasaida katika utambuzi wa magonjwa ya saratani kwa watoto hususani kwenye maeneo yasiyofikika kwa urahisi hapa nchini baada ya kazi hii kufanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tunafarijika kuunga mkono jitihada hizi ambazo ni msaada mkubwa kwa rika la watoto hapa Tanzania,” alisema Hanna.
Aliongeza “Ushirikiano huu utaanza na uanzishwaji wa kituo cha matibabu hapo mkoani Lindi ili kuleta huduma karibu na wahitaji.Tunaamini kuwa huu ni mwanzo tu wa ushirikiano utakaofanya kufikisha huduma hizi maeneo mengi ya nchi siku za karibuni.” Msaada huu utasaidia kuhakikisha watoto wanapata matibabu bora na ya uhakika karibu na makazi yao. 
Msaada huu wa PAET kwa TLM katika utoaji wa huduma za matibabu kwa watoto ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii ambapo kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa afya, kampuni  inategemea kuleta mchango chanya katika kuokoa maisha ya watoto wenye saratani nchini.
Tumaini La Maisha, ni shirika lisilo la kiserikali lenye lengo lakutoa huduma za matibabu bure kwa watoto wenye wenye saratani nchini ili kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo.
PanAfrican Energy Tanzania (PAET) ni kampuni ya uzalishaji gesi asilia inayowajibika kulinda mazingira pamoja na jamii ikijidhatiti kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa sekta ya gesi nchini kwa wateja pamoja na jamii zinazozunguka maeneo ya uendeshaji. Ikiwa na shabaha ya afya na elimu, kampuni hii imeendelea kufanya uwekezaji kwenye sekta hizo huku ikichochea uvumbuzi, miradi yenye kuleta manufaa kwa nchi.
  Miaka 20 ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi nchini.
Kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa zaidi ya miaka 20, PanAfrican Energy ni kampuni yakitanzania inayoongoza katika uzalishaji,uwekezaji pampoja na uendelezaji wa gesi asilia nchini.

Comments are closed.