The House of Favourite Newspapers

Polisi Asakwa Kumbaka na Kumpa Ujauzitio Mwanafunzi

0

MSAKO mkali wa polisi aliyetoroka kwa tuhuma za kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha kwanza wilayani Kyela mkoa wa Mbeya bado unaendelea; duru za kipolisi zimeeleza.

 

Polisi huyo mwenye namba PC H 9946, Daniel Mlanda wa Kituo cha Polisi Kyela anadaiwa kutoroka lindoni kwake tangu Mei 28, mwaka huu kwa madai ya kuepuka soo la kumpachika mimba mwanafunzi huyo ambaye amekuwa akidai mtuhumiwa huyo asakwe popote alipo ili sheria ichukuwe mkondo wake.

 

“Haikuwa hiyari yangu; nilikuwa napelekwa na mama mdogo kwa huyo askari sijui kwa maslahi gani, nilikuwa nikifika eneo lake la lindo lililopo kwenye benki (jina linafichwa). Alikuwa ananichukua na kuniingiza kwenye chumba kidogo na kunifanyia ukatili huo,” alisema mwanafunzi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.

 

Mwanafunzi huyo alisema hayo wiki iliyopita mbele ya kamati inayoratibu kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kimkoa yanafanyika leo (Jumanne) wilaya ya Kyela.

 

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ulrich Matei, amethibitisha kutoroka kwa askari huyo na kusema akikamatwa atachukuliwa hatua za kijeshi ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani. Matei alisema, mpaka sasa askari huyo anahesabiwa kuwa ni mtoro kazini.

 

Kamanda Matei alisema, akikamatwa atachukuliwa hatua kama wahalifu wengine kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Awali, baada ya Daniel kudaiwa kufanya ubakaji huo, inaelezwa kuwa yalikuwepo mazingira ya kumlinda ili asichukuliwe hatua bila kutajwa aliyekuwa akimlinda.

 

Hata hivyo, baada ya taarifa za tukio hilo kufikishwa kituo cha msaada wa kisheria wilayani Kyela na kumfikia pia Mkuu wa Wilaya hiyo Claudia Kita, amri ya kukamatwa kwa askari huyo ilitolewa jambo lililomfanya mtuhumiwa kutoroka.

 

Hata hivyo, taasisi hiyo ya kisheria imesikitishwa na kitendo cha askari huyo licha ya kutafutwa, alipenyezewa taarifa za kusakwa kwake na watu wasiojulikana, jambo lililompa nafasi ya kuratibu utoro.

 

Inaelezwa, Daniel anadaiwa kuondoka mkoani Mbeya kwa kufungasha mizigo yake yote huku akisaidiwa na baadhi ya maofisa wenzake wa polisi (Hawakutajwa) na kuondoka nayo sambamba na mkewe.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Uwazi umebaini kuwa, askari huyo yuko mafichoni mkoani Mwanza nyumbani kwa wazazi wake.

 

Mbali ya kumpa mimba mwanafunzi kwa kumbaka, askari huyo amedaiwa pia kumzalisha afisa mtendaji mmoja kisha kumtelekeza na mtoto.

 

Kama hilo halitoshi, mwanafunzi mmoja kutoka Chuo cha Ufundi Kyela (jina linafichwa) naye ameibua madai ya kuzalishwa na askari huyo na kuachwa solemba licha ya awali kupewa ahadi ya kuolewa naye.

Stori: EZEKIEL KAMANGA, MBEYA

 

MIZENGWE WATOBOA SIRI KUDUMU MUDA MREFU

Leave A Reply