The House of Favourite Newspapers

Senene Wasababisha Bei ya Nyama Kudorora

0

BIASHARA ya nyama imedorora sasa nchini Uganda kutokana na msimu wa senene kuanza. Raia wa Uganda sasa hununua viazi na kushushia na senene. Kuenea kwa senene zinazojulikana kama Nsenene katika manispaa ya Rukungiri nchini Uganda kumesababisha mauzo ya nyama nchini humo kuzidi kushuka.

 

Kilo moja ya nyama kwa sasa nchini humo ni Sh 6200 wakati awali ilikuwa 8100. Mmoja wa wachuuzi katika bucha lililopo katikati ya soko kuu la Rukungiri, Abdullah Tumwebaze, anasema watu wachache wananunua nyama tofauti na zamani kabla ya msimu wa senene kuanza.

 

Anasema mahitaji ya nyama kwa sasa yanazidi kupungua na kuongeza kuwa alikuwa akiuza kati ya kilo 100-150 za nyama kwa siku lakini kwa sasa anauza kilo 50-80 kwa siku. Abdullah ambaye ni msimamizi wa uchinjaji kwa imani ya kiislamu katika Manispaa ya Rukungiri, anaongeza idadi ya ng’ombe wanaochinjwa katika manispaa hiyo inazidi kupungua.

 

“Biashara ni mbaya kwa kweli, hasa ukizingatia msimu huu wa sikukuu pia ni msimu wa senene, watu wananunua viazi, wanakwenda kuchanganya msosi wao na senene. Kwa sasa ninauza kilo 50 za nyama na siku ambayo nikiuza sana nafikisha kilo 80. Nilikuwa nikichinja ng’ombe 2 kwa siku na nyama yote inaisha lakini kwa sasa nachinja mmoja na anabaki,” alisema Abdullah.

 

Joseph Friday ni muuzaji wa mishkaki katika uwanja wa Ntungamo uliopo mji wa Rukungiri, anaunga mkono hoja hiyo na kueleza kuwa amepunguza idadi ya nyama aliyokuwa anaandaa kwa biashara yake kutoka kilo 7 hadi 3 kwa siku kutokana na msimu wa senene.

 

“Hali sasa imekuwa mbaya kwa sababu ya senene, ninatamani kama zingeanza kutoweka mapema ili niongeze kipato changu kwa sababu nilikuwa nikiuza mishkaki kilo 7 ya nyama kwa usiku mmoja, lakini kwa sasa ninauza kilo 3 tu, wateja wamepungua sana. Badala yake wananunua senene na kuacha nyama,” Joseph aliongezea.

 

Jackson Mukuru, mkazi wa kaunti ndogo ya Buyanja kaunti ya Rukungiri naye aliongeza kuwa alipokamata senene kwa usiku mmoja, siku iliyofuata wakati akielekea sokoni kununua kitoweo, alibadilisha mawazo na kununua senene.

 

“Kwa sababu pamoja na kwamba ni watamu, lakini senene huja mara moja kwa mwaka na nyama iko hapa kila siku. Kwa hivyo siwezi kununua nyama na kuacha senene hata kama nimepelekewa kijiko mdomoni, nitachagua senene”

GABRIEL MUSHI NA MTANDAO

Leave A Reply