The House of Favourite Newspapers

Shigongo: Ahsante Rais Magufuli kwa Kutimiza Ndoto za Mwl Nyerere

DIARY ya Shigongo – 46: 

LEO ni Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetangulia mbele za haki Oktoba 14, 1999.

Ni miaka ishirini sasa imepita tangu Nyerere alipotutoka, lakini bado ni kama anaishi ndani yetu! Mambo makubwa aliyoyapigania kwenye nchi hii, jitihada kubwa alizozifanya kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi bora na ya kuigwa duniani, kamwe hayawezi kusahaulika ndani mwetu.

 

Binafsi namkumbuka Mwalimu Nyerere kwa mambo mengi sana! Ndiye aliyekuwa kinara wa mapambano ya kupigania uhuru wetu kutoka kwa wakoloni na hatimaye tukawa taifa huru, pamoja na kuchangia mataifa mengine mengi Kusini mwa Afrika kupigania uhuru wao.

 

Yapo mambo mengi aliyoyafanya enzi za uhai wake kubwa zaidi ikiwa ni jinsi alivyofanikiwa kutuunganisha kama taifa na kuwa kitu kimoja.

 

Siyo jambo rahisi kuiunganisha nchi yenye watu zaidi ya milioni hamsini na makabila zaidi ya mia moja na ishirini kuwa kitu kimoja, lakini Nyerere aliweza. Huwezi kusikia hata siku moja kwamba Watanzania wanabaguana, iwe kwa sababu ya dini, makabila au rangi tofauti na nchi nyingine nyingi.

 

Misingi imara iliyojengwa na baba wa taifa hili ndiyo inayotufanya leo hii tutembee vifua mbele, nchi yetu ikisifika dunia nzima kutokana na kuwa kisiwa cha amani.

 

Jambo lingine kubwa ambalo linamtofautisha Nyerere na viongozi wengine wengi duniani, ni kwamba hakuwa na tamaa kabisa. Wakati anaingia madarakani, Tanzania ilikuwa na utajiri mkubwa wa madini ya kila aina yakiwemo dhahabu, almasi na kadhalika.

 

Kwa sababu alikuwa anajua kwamba Watanzania wengi hawana uelewa wa namna ya kuchimba madini hayo, alipitisha msimamo nchi nzima kwamba dhahabu na madini mengine yote yasichimbwe kwanza mpaka Watanzania wazawa watakapokuwa na uelewa wa namna ya kuchimba madini yao.

 

Angekuwa ni mtu mwenye tamaa ya mali, angeweza kukubaliana na mabepari waliokuwa wakimfuata kila siku na kujaribu kumshawishi kwamba awauzie madini yetu. Alikuwa anajua kwamba zawadi ya madini iliyopo Tanzania, imetolewa na Mungu kwa ajili ya kuja kuwasaidia Watanzania na alitaka kila mmoja anufaike na zawadi hiyo.

 

Moyo aliokuwa nao, ulikuwa wa kipekee sana, mapenzi aliyokuwa nayo kwa Watanzania yalikuwa makubwa sana, yaani ni kama baba ambavyo anahangaika kujenga nyumba kubwa na nzuri ili wanaye waje kuishi hata kama yeye hatakuwepo tena duniani.

 

Mwalimu Nyerere alikuwa na maono ya mbali, alijua wazi kwamba kuingia kwenye shughuli za uchimbaji wa madini bila kuwa na uelewa wa kutosha, ni hatari kubwa kwa taifa kwa sababu mwisho wa siku, watakaonufaika na rasilimali za madini, watakuwa ni wale wajanja wachache mno.

 

Sijui nini kilitokea baadaye, watu wakaanza kuchimba madini! Kilekile alichokuwa amekikataa Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wake, kilianza kufanywa na watu waliomfuatia madarakani.

 

Baadhi ya viongozi tuliowachagua na kuwapa dhamana ya kutulindia rasilimali zetu, wakaungana na mabeberu kutunyonya, wakaingia mikataba ya kinyonyaji na kuanza kufaidi rasilimali zetu. Watu wakawa wanasomba madini yetu na kuyapeleka kwao, wakituachia mashimo tupu na umaskini wetu wa kutupwa!

 

Kwa kipindi kirefu nchi yetu ilikuwa ni kama shamba la bibi, tumeibiwa sana rasilimali zetu, tumeibiwa sana madini yetu! Na kibaya zaidi ni kwamba waliokuwa wakishirikiana na wanyonyaji hao, ni Watanzania wenzetu.

 

Mikataba isiyofaa iliingiwa na viongozi wetu, eti madini yanasafirishwa na Serikali inalipwa mrahaba wa asilimia tatu tu! Huu ulikuwa ni unyonyaji wa hali ya juu mno.

 

Katika kipindi ambacho kila mmoja alikuwa ni kama amekata tamaa, Mungu akaonesha miujiza yake kwa kumsimamisha Rais Dk John Pombe Magufuli kuwa kiongozi wa nchi hii.

 

Alipoingia madarakani tu, mara moja alipiga marufuku usafirishwaji wa makinikia kwenda nje ya nchi. Kwa miaka nenda rudi, madini yalikuwa yakisafirishwa kwa mbinu hii, huku tukiambiwa eti ni mchanga tu!

 

Nikiri kwamba kipindi ambacho Rais Magufuli anapiga marufuku usafirishaji wa makinikia, niliogopa sana ndani ya moyo wangu. Tuliambiwa kwamba wazungu wa makinikia, wanaweza kutupeleka mahakamani kutushtaki na mwisho tukatakiwa kulipa mabilioni ya fedha.

 

Sikuwa na hakika kama uamuzi wa Rais Magufuli utafanikiwa na pengine siyo mimi tu ambaye nilikuwa na hofu, Watanzania wengi tulikumbwa na hofu kubwa dhidi ya mabeberu, lakini kwa ujasiri wake, Rais Magufuli aliamua kusimamia msimamo wake na hatimaye matunda yakaonekana.

 

Hivi sasa Serikali inagawana mapato yatokanayo na madini yenu kwa asilimia hamsini kwa hamsini na Kampuni ya Barrick Gold Mining. Pengine hizi ni ndoto alizokuwa nayo Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi sana! Kuona Watanzania wananufaika na madini yao.

 

Ukimfuatilia kwa karibu Rais Magufuli, unaweza kugundua kwamba anayaishi sana mawazo na mitazamo ya Mwalimu Nyerere. Mambo mengi mazuri ambayo yalianzishwa na Nyerere, lakini kwa sababu moja au nyingine baadaye yakaja kukwama, yeye anayafufua upya!

 

Ni mtu ambaye pengine hakutarajiwa kabisa wakati wa vuguvugu la uchaguzi mkuu wa 2015, lakini anachokifanya tangu alipoingia madarakani, anatuthibitishia kwamba Mungu hakuwa ametutupa sisi wanaye. Alikuwa anajua kwamba Tanzania inamhitaji mtu kama Rais Magufuli ili kuikwamua pale ilipokuwa imekwama kwa miaka nenda rudi.

 

Binafsi nilikuwa namfahamu Magufuli kabla hajawa rais, lakini sasa naweza kusema kwamba nimemfahamu zaidi baada ya kuwa rais. Misimamo yake siyo ya kutetereka hata kidogo linapokuja suala la kuwatetea wananchi, hasa wanyonge. Anao uwezo wa kuthubutu katika mambo ambayo pengine wengine wote tungeona hayawezekani! Huyu ndiye rais ambaye Tanzania ilikuwa ikimhitaji.

 

Ahsante Mungu kwa kutupa rais wa aina hii na ahsante Rais Magufuli kwa kutimiza ndoto za Mwalimu Nyerere. Naamini huko aliko akiitazama Tanzania ya sasa, ataishia kutabasamu kwa furaha.

Mungu ibariki Tanzania, ahsanteni kwa kunisoma.

 

Comments are closed.