The House of Favourite Newspapers

Shuhudia Raundi Zote 10, Mwakinyo vs Tinampay (Picha +Video)

0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiongea jambo baada ya Hassan Mwakinyo kutangazwa mshindi dhidi ya  Arnel Tinampay kutoka Ufilipino usiku wa kuamkia leo katika Uwanja wa Uhuru.

BONDIA Hassan Mwakinyo amemchapa Arnel Tinampay kutoka Ufilipino katika pambano  kali la Super Welter la raundi 10, lililopigwa usiku wa kuamkia leo katika Uwanja wa Uhuru ulioko Temeke jijini Dar es Salaam.

…Mwakyembe akiompongeza Hassan Mwakinyo.

Pambano hilo limeacha maswali kwa baadhi ya mashabiki kutoonekana kuridhika na ushindi wa pointi wa Mwakinyo, ambapo walitamani kuona akishinda kwa KO.

 

Tinampay alikuwa mgumu na kumkabili Mwakinyo hadi kumaliza raundi zote 10 na majaji kuamua mshindi kwa pointi.

Hassan Mwakinyo (kulia) akizichapa na Arnel Tinampay kutoka Ufilipino

Jaji namba moja alitoa ushindi wa pointi 98-92, jaji namba mbili alitoa pointi 97-93 kwa Mwakinyo na jaji namba tatu alitoa sare ya pointi 96-96.

 

Katika pambano hilo lililoanza saa 5.25 usiku jana, Mwakinyo alilazimika kusubiri hadi raundi ya tatu kuwanyanyua mashabiki baada ya kumsukumia makonde mazito Tinampay. Katika raundi hiyo, Mwakinyo akishangiliwa na mamia ya mashabiki waliofurika uwanjani, alionyesha uhai mkubwa na kiu ya mashabiki ilikuwa ni kummaliza mapema mpinzani wake.

“Piga huyo, uaaa… mmalize kabisa huyo arudi kwao….” zilikuwa ni kelele za mashabiki wa ngumi waliofurika uwanjani hapo, kumshangilia bondia Mwakinyo.

 

Mfilipino ndiye alikuwa wa kwanza kurusha ngumi baada ya mwamuzi Emmanuel Mlundwa kulianzisha tu, ambapo ilimkuta Mwakinyo mbavuni kabla ya kuanza kujibu mapigo. Tinampay aliganda kwa sekunde mbili akimkodolea macho Mwakinyo katikati ya mchezo.

Raundi ya pili, Tinampay aliendeleza mashambulizi huku akicheza kwa staili ya kutorudi nyuma na kumbananisha Mwakinyo kwenye kamba, lakini Mtanzania huyo alijibu mapigo dakika ya mwisho ya raundi hiyo kabla ya kurudi kwa kasi raundi ya tatu.

 

Raundi ya nne, Mfilipino alionywa na mwamuzi baada ya kupiga ngumi chini ya mkanda, baada ya kuchezea kipigo katika raundi hiyo. Raundi ya tano, Mwakinyo alianza kwa kupiga ngumi  nne mfululizo za kudokoa na ambazo zilimkuta kwenye paji la uso,  naye bila kuchelewa akajibu mapigo.

Dakika ya pili ya raundi hiyo, Tinampay alitumia tena mbinu ya kumbananisha Mwakinyo kwenye kona na kumshambulia, lakini alijihami na kujibu mashambulizi kwa kupiga ngumi zilizompata sawia Tinampay.

Hassan Mwakinyo akiongea jambo baaada ya kumshinda Tinampay kutoka Ufilipino.

Tinampay, ambaye alionekana kutochoka, alimpiga ngumi za tumbo mfululizo Mwakinyo raundi ya sita kwa lengo la kumkata pumzi, lakini Mwakinyo alionekana kumpuuza huku akitikisa kichwa kuonyesha ishara kwamba, hazijamwingia.

 

Kwenye raundi ya saba, Mwakinyo alikwenda chini lakini si kwa konde bali aliteleza na kunyanyuka kisha kuendelea huku akicheza kwa kujihami na kumpa Tinampay fursa ya kushambulia.

PICHA NA RICHARD BUKOS | GPL

TAZAMA RAUNDI ZOTE 10

Raundi ya nane, Tinampay alianza kwa kasi na kumbananisha tena Mwakinyo kwenye kona, ingawa Mtanzania huyo alitumia mbinu ya kumkimbia huku akijibu mashambulizi kwa kumshtukiza.

 

Raundi ya tisa, Tinampay aliendelea kumshambulia Mwakinyo ambaye alionekana kama kulewa,  huku maelfu ya mashabiki wakiongozwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe wakiwa kimya huku wachache wakipiga kelele kumtaka Mwakinyo amkimbie mpinzani wake ili amalize raundi hiyo.

 

Raundi ya 10, Mwakinyo aliwanyanyua mashabiki uwanjani hapo baada ya kumshambulia mfululizo Tinampay, ambaye kuna wakati alionyesha ishara ya kuzikubali kwa kusimama wima katikati ya mchezo na kutikisa kichwa kwa sekunde kadhaa na kuendelea kujibu mashambulizi kwa kushtukiza.

 

Baada ya mchezo huo, Mwakinyo alisema amepata changamoto kubwa kusaka ushindi katika pambano hilo, lakini umati uliofurika kulishuhudia ndiyo ulimfanya kupambana zaidi ili kushinda.

Leave A Reply