The House of Favourite Newspapers

Tafrani Nzito Yaibuka Marufuku Wauza Bima

0

DAR: Ni janga, ndivyo unavyoweza kutafsiri baada Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira), kupiga marufuku kampuni za bima nchini kuendelea kuwatumia wauzaji wa bima kwa niaba ya kampuni hizo (DSF) ambao wanakadiriwa kuwa zaidi ya 500 nchi nzima. Gazeti la IJUMAA linaripoti.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Novemba 15, mwaka huu, Tira kutoa barua yenye namba 083/2019 na kuisambaza kwa kampuni za bima, mawakala na ‘mabroka’ na kuwaagiza kusitisha mara moja kufanya kazi na wauzaji hao wanaokadiriwa kukusanya shilingi bilioni 1.2 kwa mwezi.

 

Kwa mujibu wa barua hiyo, kuanzia Novemba 15 ni marufuku kuwatumia wauzaji hao kwa sababu wengi wao hawana elimu yenye vigezo vya kuwawezesha kuhudumia soko la bima nchini, wamekuwa wakikata bima za uongo na kuvuruga soko la bima nchini.

 

Ilisema vitendo hivyo vya wauzaji ni kinyume cha sheria ya bima namba 10 ya mwaka 2009, kifungu cha 161 (1), lakini pia makampuni hayo kuendelea kuwatumia baada ya agizo hilo la Tira ni kinyume cha sheria hiyo kifungu namba 157 (3).

 

“Kwa hiyo tunawaagiza kuacha mara moja kuendelea kuwatumia hadi hapo mamlaka itakapotangaza hatua nyingine zaidi,” ilisema barua hiyo iliyosainiwa na Kamishna wa Tira nchini, Dk Mussa Juma.

 

RAIS TAASISI YA BIMA AFUNGUKA

Akizungumza na IJUMAA, Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania, Bosco Bugali alikiri kupokea maagizo hayo kutoka kwa Tira kwa wanachama wake ambao ni wa bima za jumla kama vile majanga ya moto, ajali na maisha.

Akifafanua zaidi, Bugali alisema marufuku ya Tira ina athari hasi na chanya, lakini athari hasi ni kubwa zaidi kutokana na hali ya soko la ajira lililopo nchini.

 

Alisema kiujumla Tira imeamua kupiga marufuku wauzaji wa bima kutokana na udhaifu wa baadhi ya makampuni ya bima nchini kuajiri wauzaji ambao hawana vigezo kitaaluma.

 

“Kwa sababu ili kumuingiza mtu akuuzie bima, kigezo cha kwanza ni kuwa na Certificate of Proficiency in Insuarance (COP) ambacho ndicho kigezo cha chini, anaweza kuwa na uwezo wa kuuza, lakini hajawa na ujuzi huo kitaaluma,” alisema.

Alisema cheti hicho hutolewa na Chuo cha IFM kwa muda wa miezi mitatu na ada yake haizidi Sh. 450,000.

 

“Kuna mawakala walikuwa wanakuja kutulalamikia, kuwa lazima wauzaji wawe COP, kwa sababu kwa upande wao wamewalipia na kuwasomesha, lakini kuna baadhi ya kampuni hazizingatii hilo na kuruhusu ambao hawana vigezo,” alisema.

 

Alisema kumekuwa na nyaraka za bima ambazo zimefojiwa, jambo ambalo pia Tira wamelizingatia na kuamua kuchukua hatua hizo.

 

WAHITIMU, VIJANA WAPOTEZA AJIRA…

Wakati Serikali ikihaha namna ya kutatua bomu la ukosefu wa ajira kwa vijana, hatua hiyo ya Tira imeelezwa kusababisha zaidi ya vijana 500 kupoteza ajira.

 

Hatua hiyo inatokana na wingi wa vijana wanaohitimu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambapo kwa mwaka wanakadiriwa kuhitimu zaidi ya 600 katika fani ya bima, ilhali kampuni za bima nchini zikiwa 31 pekee.

 

Buhali alisema wauzaji hao wa bima wameathiri siyo tu kampuni hizo za bima, bali soko hilo la ajira kwa sababu walikuwa ni waajiriwa kabisa.

 

“Kwa sababu kwa mfano kampuni moja kama Jubilee imepoteza wauzaji 200, ambao walikuwa na uwezo wa kukusanya zaidi ya bilioni moja kwa mwezi, sasa hiyo ni kampuni kubwa, kuna hizi kampuni ndogondogo… kiujumla athari ni kubwa. Hivyo, Tira wanapaswa kuangalia marufuku hii.

 

“Nakumbuka miaka yetu tuliokuwa tunahitimu IFM tulikuwa hatuzidi 15, lakini sasa wapo zaidi ya 600, hebu niambie hawa wote wataenda wapi. Na tayari walikuwa na uwezo wa kujilipa mishahara kwa mwezi na kukua kibiashara hadi kuja kufungua kampuni zao?” Alihoji.

 

Hata hivyo, alisema wauzaji hao walikuwa wanazisaidia kampuni za bima nchini kwa sababu asilimia kubwa ya madalali walikuwa wanakusanya fedha za bima na kukaa nazo.

“Lakini sasa soko la bima limekuwa, tunakusanya zaidi ya bilioni 90 kwa mwaka na linazidi kukua kila siku,” alisema.

 

WAUZAJI (DSF) WAANGUA VILIO

Baadhi ya wauzaji wa bima hizo kwa niaba ya makampuni, waliozungumza na IJUMAA, walielekeza kilio chao kwa Serikali, kuagiza Tira itengue marufuku hiyo na badala yake itathmini namna bora ya kushughulikia changamoto zilizopo kwenye tasnia hiyo.

 

“Unajua samaki mmoja akioza kwa hali ya sasa, huwezi kusema wote wameoza, kwa sababu si kweli kwamba sisi wote nchi nzima hatuna vigezo kitaaluma. Vyeti tunavyo, ni wachache sana ambao hawana vyeti.

 

“Kwa hiyo, Tira kama ikiamua kufanya ukaguzi, kwa kupitia makampuni ya bima na mawakala, ni jambo ambalo linawezekana kabisa, kwa sababu wanaagiza kuleta wauzaji wao na kukagua kila kitu chao na wakienda kinyume na hapo hatua zinachukuliwa, siyo kutufungia kwa sababu athari ni kubwa mno,” alisema mmoja wa wauzaji hao ambaye alikuwa na ofisi yake keneo la Goba-Mwisho, Dar.

 

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na muuzaji mwingine kutoka Ilala-Boma, ambaye alisema licha ya kwamba hakuweza kupata ajira, aliamua kujiajiri na kuuza bima za kampuni moja.

 

“Nilianza taratibu kwa kupata kamisheni ya Sh. 200,000, lakini mpaka sasa ninapata milioni moja kwa mwezi, nina cheti, kila kitu ninacho, lakini nimefungiwa kwa sababu ya wachache, hebu niambie nitaenda wapi,” alisema.

 

Leave A Reply