The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 45

3

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa anashirikiana na Diego kutaka kumuibia Msuya kisha kutoroka pamoja. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…Ulikuwa mpango kabambe walioupanga ambao ulitakiwa kufanyika ndani ya saa chache na kutoroka kutoka ndani ya nyumba hiyo. Kila kitu kilikuwa kimekamilika, Arianna akachukua kiasi kikubwa cha fedha na madini ya Tanzanite yaliyokuwepo chumbani kisha kuyaweka ndani ya begi.

Wakati akiendelea kufanya hivyo, moyo wake uligawanyika, kulikuwa na upande ambao ulimwambia kwamba kile alichokuwa akikifanya kilikuwa sahihi kabisa kwani hata zile fedha alizoziiba zingemsaidia katika kununua madawa ya kulevya na kujidunga kama kawaida.

Upande mmoja wa moyo wake ulikuwa kinyume chake, huo ulimwambia kwamba kile alichokuwa akikifanya hakikuwa sahihi hata mara moja. Mzee huyo bilionea aliamua kumchukua, kumuondoa katika wimbi la ufukara aliokuwa nao na hatimaye kumpa maisha mazuri, alimpa kila kitu alichotaka na katika maisha yake hakutaka kuona hata siku moja binti huyo anapatwa na tatizo lolote lile.

Pamoja na kufanyiwa hayo yote, eti leo hii alikuwa akimuibia fedha, pamoja na kumfanyia wema wote huo eti leo hii alikuwa akimuibia madini yake ya thamani, aliyoyategemea katika kumuendeshea maisha yake, hakika lilikuwa jambo baya na lililojaa ukatili, kwa yale aliyoyafanya mzee Msuya, hakutakiwa kufanyiwa mambo hayo.

Moyo wake ulijaa tamaa, hakutaka kuisikiliza sauti ya pili ilimwambia nini, alichokifikiria wakati huo ni kuchukua fedha hizo na kuondoka nazo tu. Alipokamilisha kila kitu, ilipofika saa kumi jioni ndiyo ulikuwa muda wa kuondoka nyumbani hapo na Diego.
“Subiri kwanza…” alisema Diego.
“Tusubiri nini?”

“Ni lazima tucheze mchezo kabambe kama C.I.A,” alisema Diego.
“Kivipi?”
“Wachukue watoto usiku kisha wapeleke sehemu kula ice cream…”
“Kwa nini?”

“Huku nyuma nitavunja mlango, nitachukua damu ya ng’ombe na kuinyunyizia baadhi ya maeneo humu ndani,” alisema Diego, japokuwa alikuwa mtumiaji mzuri wa madawa ya kulevya lakini alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria.
“Mmh!”

“Ndiyo hivyo! Tunaposema tumevamiwa, milango ionekane imevunjika, itakapojulikana umetekwa, basi watu waone hata damu, kwamba ulipigwa kidogo, iko poa sana kama tutafanya hivyo,” alisema Diego na kuachia tabasamu pana.

Wazo lake lilionekana kuwa zuri, liliungwa mkono na Arianna na hivyo kuanza kufanya mikakati ya kuwaambia watu wengine ndani ya nyumba hiyo kwamba siku hiyo, chakula cha usiku wangekwenda kula katika hoteli ya kifahari ya Amazon iliyokuwa hapohapo Arusha.

Ilipofika saa moja na nusu usiku, wakatoka na kuelekea huko huku wakiongozana na watoto wa mzee Msuya, mfanyakazi wa ndani na Diego mwenyewe. Walikwenda mpaka katika hoteli hiyo lakini Diego hakutaka kukaa sana, akaaga kwamba kuna sehemu alitakiwa kwenda hivyo wamsubiri na angerudi mahali hapo muda mchache ujao, akakubaliwa.

Alichokifanya ni kurudi nyumbani. Alipofika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuvunja milango kadhaa, ukiwepo wa kuingilia sebuleni, chumbani kwa mzee Msuya na katika chumba cha Diego, baada ya kufanikisha, akairudisha milango ile kwa kuiegesha kisha haraka haraka kurudi hotelini.
“Nimekamilisha kila kitu, turudini sasa…” aliandika Diego kwenye ujumbe mfupi.

Hawakutaka kuendelea kukaa tena hotelini, kile walichokuwa wamekihitaji tayari kilifanyika hivyo kuanza kurudi. Kwa kuwa kila kitu kilikuwa kwenye mipango, hata mlango wa kuingia ndani haukuwa ule wa sebuleni bali ulikuwa ni wa jikoni.

Ndani, hakutaka watoto hao au mfanyakazi wa ndani atoke chumbani, aliwaambia watulie chumbani na walale kitu walichokitii kwa haraka sana.
“Kwa hiyo inakuwaje?”
“Tuanze kazi…begi la mkwanja unalo?”
“Ninalo….”
“Na madini je?”
“Kila kitu kipo.”

Hicho ndicho kilichokuwa kikihitajika, hakukuwa na sababu ya kuchelewa, walichokifanya ni kunyunyizia kiasi kidogo cha damu sehemu mbalimbali kisha kuchukua begi hilo na kuondoka nyumbani hapo huku tayari ikiwa ni saa sita za usiku.
****
“Kijana mbona unahema hivyo?” lilikuwa swali moja kutoka kwa polisi, alikuwa akimuuliza kijana aliyefika nyumbani hapo huku akihema kama mbwa aliyechoka.
“Kuna tukio limetokea, tena sasa hivi?” alisema kijana huyo huku akiegemea kwenye kaunta ya kituo hicho cha polisi. Polisi wote waliosikia hivyo, wakamsogelea.
“Tukio gani?”
“Majambazi wamevamia kwa mzee Msuya!”
“Unasemaje?”

“Majambazi wamevamia kwa mzee Msuya…”
“Mzee Msuya yupi? Huyu bilionea?”
“Ndiyo,” alijibu kijana huyo.
Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, harakaharaka wakatoka polisi wanne, wakaingia ndani ya gari lao na safari ya kuelekea nyumbani kwa mzee huyo kuanza huku mikononi mwao wakiwa na bunduki za moto.

Njiani, walikuwa wakiulizana tu, ilikuwaje majambazi wavamie ndani ya jumba hilo kubwa na wakati waliamini kwamba kulikuwa na ulinzi wa kutosha? Wakati tukio hilo likitokea, mlinzi alikuwa wapi? Kila walichojiuliza, wakakosa jibu.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Mtaa wa Nyamanoro aliokuwa akiishi mzee huyo, wakaanza kuelekea katika sehemu ilipokuwa na nyumba hiyo, hata kabla hawajaifikia, wakaruka kutoka garini mwao, wakabimbilika kama makomandoo na kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo.
Kitu cha kwanza kabisa walichokiona, mlango wa kuingilia sebuleni ulikuwa umevunjwa, wakakoki bunduki zao, wakaanza kutembea kwa mwendo wa machale, kitu walichoamini ni kwamba bado majambazi hao walikuwa ndani ya nyumba hiyo.

“Watakuwa ni Wasomali…mkiwaona, wapigeni risasi…” ilikuwa ni amri kutoka kwa mkuu wa kituo ambaye yeye alibaki garini.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

3 Comments
  1. Deborah says

    Mbona upande mmoja tu. . … .

  2. Deborah says

    Mbona upande mmoja tu. . . . . . Vipi kuhusu briana

  3. david moses says

    Ngependa kuona na upande wa brianna..

    Kwel tamaa mbaya na wema ote alofanyua malipo yake ndo hayo?

Leave A Reply