The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness – 63

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.

Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi.

Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya bila mtu yeyote kujua kwamba bado yupo hai, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna na tayari amefika nyumbani kwa Msuya.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Furaha kubwa ikatanda kwenye nyumba hiyo, kila mtu akawa anamshukuru Mungu wake kwa kilichotokea. Msuya na Diego walipitiliza hadi ndani wakiwa na msichana huyo na kumpeleka sebuleni ambapo hakukaa sana, Msuya akamtaka waelekee chumbani.

Brianna alishindwa kubisha, mwanaume huyo akamshika mkono na kumuongoza kupanda kwenye ngazi za kuelekea chumbani na muda mfupi baadaye, tayari walikuwa chumbani.
“Arianna!”

“Abee!” aliitikia Brianna kwa kusitasita kwani ukweli ni kwamba hilo halikuwa jina lake, bali la pacha wake.
“Namshukuru Mungu wangu kwamba hatimaye umerudi kwenye mikono yangu,” alisema Msuya na kumkumbatia Brianna, ndani ya akili yake akiamini kabisa kwamba huyo alikuwa ni Arianna, akawa anambusu sehemu mbalimbali za mwili wake kama ambavyo alikuwa akimfanyia mkewe.

Tofauti na Arianna, Brianna alikuwa mgeni kabisa kwenye ulimwengu wa mapenzi. Licha ya urembo wa kipekee aliojaaliwa, uliosababisha apate usumbufu mkubwa kutoka kwa wanaume wa kila rika, kuanzia vijana, watu wazima mpaka wazee, siku zote alikuwa na msimamo uliosababisha kila mmoja amheshimu.

Mpaka anafikisha umri huo, Brianna hakuwahi kuwa na ukaribu na mwanaume yeyote, hakuna mwanaume aliyewahi kumshika mkono kimahaba wala kumsogelea kama alivyokuwa amefanya Msuya, achilia mbali kushiriki naye tendo.

Alishajiapiza kwamba atautunza usichana wake mpaka siku atakayokuja kuolewa na hiyo ndiyo itakayokuwa zawadi ya mumewe. Kitendo cha Msuya kumkumbatia kimahaba na kumbusu sehemu mbalimbali za mwili wake, kilimfanya awe kwenye wakati mgumu mno kihisia.

Kila alipokuwa anaguswa alikuwa akishtuka sana, wakati mwingine akipiga kelele huku akionesha kutokuwa tayari kwa kile kilichokuwa kinafanywa na Msuya, jambo lililomshangaza sana mwanaume huyo.

Hata hivyo, alijipa moyo kwamba huenda mkewe amekumbana na tukio baya alipokuwa nchini Kenya lililomuathiri sana kisaikolojia kama alivyoambiwa na Diego, ikabidi awe mpole.

“Vipi mwanangu, nataka kusikia kutoka kwako,” Msuya alirudia tena swali lake lakini msichana huyo alikosa cha kujibu, ikabidi abadilishe maada kwani hakutaka kuendelea kumuona akikosa amani.
“Leo nimeagiza wakupikie chakula unachokipenda, si utafurahi?” alisema Msuya, msichana huyo akawa haelewi ni chakula gani kinachoandaliwa kwani kila kitu kilikuwa kigeni kwake. Kama ilivyokuwa mwanzo, akakosa pia majibu na kuanza kubabaika, ilibidi Msuya asimame pale kitandani na kutembea kuelekea kwenye friji.

Akatoa mvinyo laini ambao alikuwa akipenda kunywa na mkewe kabla hawajapumzika, akachukua glasi mbili na kumimina, akarudi kitandani na kumpa Brianna.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Arianna ambaye alikuwa anaweza kugida hata chupa nzima bila kulewa, Brianna aliipeleka taratibu kinywani akiwa ni kama anayejishauri kama anywe au la, akaonja kidogo kisha akamtazama Msuya kwa macho ya kuibia, alipogundua kwamba anamtazama alijilazimisha kunywa kidogo kisha akaiweka glasi juu ya meza ya kioo iliyokuwa pembeni.

“Vipi upo sawa?” Msuya alihoji huku akiendelea kumshangaa mkewe. Hakuwa Arianna yule anayemjua, alibadilika kwa kila kitu, akazidi kuamini kwamba huenda amepatwa na jambo baya sana. Hata hivyo, kama alivyokuwa amejiapiza kutoka mwanzo, aliendelea kuwa na subira.

Akaendelea kumhimiza anywe mvinyo ule, kwa taabu Brianna alifanikiwa kumaliza glasi moja lakini tayari alishaanza kuonesha mabadiliko makubwa kama mtu aliyelewa. Jambo hilo lilizidi kumshangaza Msuya, ikabidi amsaidie kumuinua na kumuelekeza kwenda kuoga ili kupunguza uchovu.

Brianna alijikaza kisabuni, akasimama japo alikuwa akipepesuka kwa mbali na kutaka kwenda bafuni kuoga lakini kituko kingine kilitokea. Tofauti na Arianna ambaye akitaka kwenda kuoga huwa haoni aibu yoyote kuvua nguo mbele za Msuya na kuchukua taulo, Brianna aliingia bafuni akiwa na nguo zake.
“Mbona unaingia bafuni na nguo mpenzi?” alihoji Msuya huku akisimama na kumfuata Brianna ambaye tayari alishaingia bafuni ambako nako alikuwa akishangaashangaa kila kitu.

Akamshika mkono na kumrudisha chumbani, akataka kumsaidia kumfungua vifungo vya gauni refu la heshima alilokuwa amevaa lakini msichana huyo alimtoa mikono, Msuya akazidi kupigwa na butwaa.
“Basi chukua taulo kabadilishie nguo hukohuko bafuni,” alisema Msuya, msichana huyo akachukua taulo na kuingia nalo bafuni, akafunga mlango kwa komeo ili kuhakikisha Msuya hamfuati. Akavua gauni lake na kumalizia na nguo za ndani, akazitundika kwenye sehemu maalum ya kutundikia nguo na kuanza kuoga.

Ilimchukua dakika kadhaa kujua namna ya kuchanganya maji ya moto na ya baridi ili kupata ya uvuguvugu na jinsi ya kufungulia ‘bomba la mvua’ kwani maisha aliyokulia hakukuwa na vitu kama hivyo. Ilikuwa akitaka kuoga, anachota maji kwenye ndoo ndogo na kuingia nayo kwenye bafu la ‘passport size’ ambalo juu halijaezekwa, anaoga kisha anatoka na kuendelea na shughuli nyingine. Maisha hayo ya Kizungu hakuyazoea kabisa.

Baada ya kuhangaika sana, hatimaye alifanikiwa kuoga, baada ya kumaliza alijifuta maji kwa kutumia taulo alilopewa kisha akavaa tena nguo zilezile alizokuwa amevaa awali, akatoka na kurudi chumbani.
Msuya alishindwa kujizuia, akaangua kicheko huku akiinuka na kwenda kumfungulia kabati la nguo kwa lengo la kumchagulia nguo za kuvaa kwani aliamini akili zake hazipo sawa.

Alichukua blauzi nyepesi na suruali ya mpira (skin jeans) alizokuwa anapenda kuvaa mkewe hasa nyakati za jioni, akampa avae lakini haikuwa rahisi kwa msichana huyo kukubali kuvua nguo mbele ya Msuya. Ilibidi atoke na kumpisha abadilishe, yeye akaenda sebuleni kuangalia kama maandalizi ya chakula yalikuwa yakiendelea vizuri.

Huku nyuma, Brianna alibadilisha nguo na kuvaa alizopewa. Haikuwa kawaida yake kuvaa suruali nyepesi tena iliyomshika maungo yake kama ile aliyovaa siku hiyo. Hakuwahi pia kuvaa blauzi nyepesi iliyokuwa inaonesha mpaka chuchu zake, akajihisi aibu kubwa ndani ya moyo wake.

Alichokifanya, alichukua mtandio wake na kujifunga juu ya nguo hizo. Akawa anaendelea kushangaa vitu mbalimbali vilivyokuwa ndani ya chumba hicho cha kifahari.

Muda mfupi baadaye, Msuya alirejea lakini alipomuona amejifunga mtandio juu ya nguo alizompa, ambazo Arianna alikuwa akizivaa bila wasiwasi wowote, alizidi kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Ikabidi amwambie autoe mtandio huo, baada ya kuvutana kwa muda, alitii alichoambiwa.

Macho ya Msuya yakatua kwenye kifua cha msichana huyo, akaona kitu ambacho kilimshtua sana moyo wake, mapigo ya moyo yakawa yanamuenda mbio mithili ya fisi aliyeona mfupa, akameza funda la mate.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply