The House of Favourite Newspapers

The Beginning of My End (Mwanzo wa mwisho wangu)-14

4

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.

Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani, anafaulu kwa kiwango cha juu na baada ya kuhitimu kidato sita, anaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa chuoni hapo, anakutana na msichana mrembo, Gladness anayetokea kumpenda sana na baada ya kumficha kwa muda mrefu historia juu ya familia yake, msichana huyo anambana na anaeleza ukweli na kwa pamoja wanasafiri kwa ndege kuelekea Tunduma, nyumbani kwa akina Ben.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Ben alikuwa amebadilika mno, tofauti kabisa na wakati anaondoka kwenda kuanza chuo. Usingeweza kuamini kwamba hapo ndiyo palikuwa nyumbani kwao na huyo ndiye mama yake mzazi.
Kwa muda wote huo, Gladness alikuwa amesimama pembeni huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Bila hata kusubiri kutambulisha, alimtambua mama yake Ben kutokana na jinsi walivyokuwa wakifanana.
“Na huyu msichana mzuri hivi ni nani mwanangu?” alihoji mama yake Ben huku akimtazama Gladness, wakawa wanatazamana.

“Ni rafiki yangu mama! Tunasoma naye chuoni,” alisema Ben huku akijisikia aibu. Tangu akiwa mdogo, hakuwahi kuonekana kuwa karibu na msichana yeyote, Gladness ndiye aliyekuwa wa kwanza maishani mwake, mama yake akampokea kwa uchangamfu na kumkaribisha.

Muda mfupi baadaye, wadogo zake Ben waliokuwa wameenda kuchota maji walirejea na walipomuona kaka yao akiwa na mgeni, walitua ndoo zao haraka na kuwakimbilia, wakamrukia Ben mwilini kwa furaha kwani zilikuwa zimepita siku nyingi bila kuonana naye, wakawa wanamshangaa kwa jinsi alivyokuwa amebadilika.

“Na huyu ndiyo wifi yetu?” alisema Jackline, mdogo wake Ben ambaye ndiye aliyekuwa mdogo baada ya wa mwisho kufariki miaka kadhaa iliyopita. Badala ya kujibu, Ben na Gladness waliishia kucheka. Wakasaidiana kuingiza mizigo kwenye kibanda chao kikuukuu na kumkaribisha mgeni.
Tofauti na Ben alivyotegemea kwamba msichana huyo ataonesha dharau kutokana na maisha aliyoyakuta, Gladness hakuonesha kujali chochote. Akajitahidi kuyazoea mazingira kadiri ya uwezo wake, jambo lililomfariji sana Ben.

Hata wadogo zake Ben walipoanza kufanya kazi ndogondogo za nyumbani hapo, ikiwemo kuosha vyombo, kufanya usafi na kupika, japokuwa bado alikuwa mgeni, Gladness naye aliwasaidia na kuwafanya wote wafurahi sana.
Kwa mwonekano wake jinsi alivyokuwa mrembo, akionesha dhahiri ametoka kwenye familia ya kitajiri, mama yake Ben na wadogo zake walitegemea kumuona akiwa na maringo lakini haikuwa hivyo.
Alionesha ushirikiano mkubwa na kwa sababu walibeba zawadi mbalimbali za vyakula, siku hiyo walishirikiana kuandaa chakula kizuri, jogoo mkubwa akaenda kununuliwa na kuchinjwa, Gladness akashiriki kwenye kila hatua ikiwemo kuchagua mchele na kupika mpaka chakula kilipoiva.

Kwa muda wote huo, Ben alikuwa akimfuatilia msichana huyo kwa karibu, ile hofu aliyokuwa nayo awali ndani ya moyo wake, ikawa inapungua taratibu na kujikuta akizidi kumpenda.

“Mh! Chakula cha leo kizuri sana, nani alikuwa kiongozi wa mapishi?” Ben aliuliza wakati wakiendelea kupata chakula cha usiku kwenye sebule yao ndogo iliyokuwa imejazwa makorokoro kibao.

“Ni wifi Glad ndiyo aliyepika,” alijibu Jackline na kuwafanya wote wacheke, kila mmoja akawa anamsifia msichana huyo, Ben akazidi kumpenda. Waliendelea kula na baada ya chakula, waliendelea na mazungumzo ya hapa na pale, Ben akiwasimulia mambo mbalimbali aliyokutana nayo mjini kwa kipindi chote ambacho hakuwepo.

Nao walimsimulia mambo mbalimbali yaliyotokea akiwa masomoni, vikiwemo vifo vya majirani zao kadhaa. Hatimaye muda wa kulala uliwadia. Kutokana na udogo wa nyumba hiyo, ilibidi mama yake Ben na wadogo zake kwa kuwa wote walikuwa wa kike, walale chumba kimoja na mgeni wakati Ben yeye alilala kwenye chumba chake cha siku zote.
Mama yake Ben na Gladness ndiyo waliolala juu ya kitanda kikuukuu kilichokuwa na godoro jembamba, wengine wakatandika mkeka chini na kulala.

Ben alichelewa sana kupata usingizi usiku huo, aliendelea kufikiria mambo mengi yaliyokuwa yakikisumbua kichwa chake, kubwa likiwa ni hali ya maisha hapo nyumbani kwao.

Alijiapiza kwamba atakapohitimu masomo na kuajiriwa, lazima mishahara yake ya mwanzomwanzo itumike kurekebisha maisha ya nyumbani kwao ili angalau familia yao nayo iwe na hadhi.

Siku hiyo ilipita, kesho yake wakashinda pamoja na Gladness ambapo majira ya jioni walitoka na kwenda kumtembeza kwenye mitaa ya Mji wa Tunduma, ikiwa ni pamoja na kununua baadhi ya bidhaa za kurudi nazo jijini Dar es Salaam.
Kwa kuwa walibakiza muda mfupi tu kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam, ilibidi Ben autumie usiku huo, baada ya kuwa wamesharejea nyumbani, kumtambulisha rasmi Gladness kwa mama yake kwamba anatarajia wakishamaliza masomo ya chuo, atamchumbia ili baadaye amuoe na kuwa mkewe halali wa ndoa.

Mama yake Ben alifurahishwa mno na taarifa hizo, akazungumza nao kwa kirefu akiwapa nasaha za namna ya kuishi pamoja lakini akawasisitiza kutokutana kimwili mpaka watakapofunga ndoana kuwa mume na mke halali, jambo ambalo wote wawili waliliahidi mbele yake.

Mwisho aliwaomba wote wapige magoti kisha akawaongoza kwenye sala maalum, akawaombea kwa Mungu awaongoze katika masomo yao ili hatimaye watimize ndoto zao za kuja kuishi kama mume na mke.

Usiku huo nao ulipita na kesho yake, maandalizi yalianza kufanyika kwa safari ya kurejea jijini Dar es Salaam. Ilikuwa siku ya huzuni sana kwa familia hiyo ambayo uwepo wa Ben na Gladness, uliwachangamsha sana.
Kwa kuwa Gladness alikuwa na akiba ya fedha za kutosha, alimuachia mama yake Ben fedha za kutosha huku akimsisitiza kwenda hospitalini kupima kwa sababu alikuwa akikohoa sana.

Mama yake Ben alimshukuru sana na kuendelea kuwaombea kwa Mungu, wakawasindikiza mpaka stendi ya mabasi ya Tunduma ambapo walipanda gari lililowasafirisha mpaka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.
S
aa sita juu ya alama, safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Precision Airways ilianza ambapo njia nzima Ben na Gladness walikuwa wakipiga stori na kufurahi pamoja.

Kitendo cha msichana huyo kufika nyumbani kwa akina Ben na kuwaona mama na wadogo zake, kilizidi kuimarisha uhusiano wao na sasa kila mmoja akawa na uhakika kwamba lazima ndoto yao ya kuja kuishi pamoja kama mume na mke itatimia.
Baada ya safari ndefu angani, waliwasili jijini Dar es Salaam na kwenda moja kwa moja mpaka chuoni ambapo kutokana na uchovu aliokuwa nao kila mmoja, walipitiliza hosteli kupumzika.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

4 Comments
  1. Hamis Mwenda says

    wow it’s so nce story good work author

  2. Gracious says

    Jaman mnatunyanyasa tulioko nje ya Tanzania. Mmeacha ku-upload hadithi humu na pia hata MPAPER hamuweki tena gazeti zenu

  3. fadhili malaki says

    kaka shigongo hadithi zako ni nzuri sana tangu enzi hizo na The rotten deal

  4. merceys says

    habari yako shingongo ni muda mrefu sana huweki hadithi zako humu hata sijui ni kwa nini au kuna njia ambay tunatakiw kufany ili tuendelee kusoma hadithi?? mimi ni msomaji mzuri sana wa hadithi zako tangia niko primary miaka hiyo nilikuw nikishika kitabu chako nakumbuka cha machozi siku ya valentine ,rais anampenda mke wangu kuna kingine nimesahau jina walifunga ndoa kwenye ndege yani ni vingi sana nasoma mpka ss nilikuw sitak kuviacha bt nw nashangaa sijui kw nini huweki naomba utuambie n nini shida uko bussy ama…

Leave A Reply