The House of Favourite Newspapers

The Beginning Of My End (Sehemu: 037)

4

NA ERIC J. SHIGONGO

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kesi kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.

Hata hivyo, licha ya watu wote kuamini kwamba ni kweli Ben ameua, na yeye mwenyewe kukiri kuhusika na mauaji hayo, rafiki yake mmoja haamini suala hilo na kuhisi kuna kitu Ben alikuwa anakificha.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inamulikwa tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.

Analelewa kimaskini lakini uwezo mkubwa aliokuwa nao darasani unamfanya afaulu na kuendelea na masomo mpaka ngazi ya chuo kikuu ambapo anajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akiwa chuoni hapo, anakutana na msichana mrembo, Gladness wanayeanzisha safari ya kimapenzi na kufikia hatua ya kuvalishana pete lakini huo unakuwa mwanzo wa safari ya matatizo makubwa kwenye maisha ya Ben.

Baada ya kunusurika kifo, anasafiri na mchumba wake mpaka visiwani Zanzibar lakini huko pia mambo yanazidi kuwa magumu na kuwafanya wakatishe ratiba yao na kurejea jijini Dar es Salaam. Bahati mbaya zaidi, wanashambuliwa vikali na majambazi baada ya kutua uwanja wa ndege na Gladness anatekwa.

Anapelekwa mafichoni ambapo katika hali ambayo hakuitegemea, rafiki yake wa siku nyingi waliyekua pamoja tangu wakiwa watoto, Gibson anajitokeza na kukiri kwamba yeye ndiye aliyetuma watu wamteke kwa sababu anampenda na anataka kumuoa.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu.

Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.

Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi.

Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu. Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

HALI ilikuwa ya simanzi mno nyumbani kwa wazazi wa Gladness ambapo mama yake aligoma kula wala kufanya chochote, akishinikiza kifanyike kila kinachowezekana mpaka Gladness apatikane.

Wakiwa katika taharuki, simu ya mezani ya nyumbani kwa akina Gladness, ilianza kuita mfululizo. Baba yake akaenda kuipokea, watu wote wakatulia kutaka kusikia ni nani aliyekuwa akipiga.

“Hapo ni nyumbani kwa akina Gladness?” sauti nzito ya kiume ilisikika baada ya baba yake Gladness kupokea simu.

“Ndi…yo, nani mwenzangu?”

“Hakuna umuhimu wa kunijua, kuna jambo nataka kukwambia kuhusu binti yenu.”

“Ndi… ndiyo nakusi…kiliza” baba yake Gladness alisema kwa kubabaika.

“Msihangaike kumtafuta binti yenu, niko naye.”

“Kwani wewe ni nani? Uko naye wapi?”

“Wewe elewa tu kwamba niko naye, hayo maswali mengine sitaki kuyasikia,” ilisikika sauti hiyo kisha simu ikakatwa.

“Ni nani? Anasemaje? Gladness amepatikana?” maswali mfululizo yalimtoka mama yake Gladness, wote wakamsogelea baba yake Gladness ambaye alishindwa cha kujibu, akavua miwani yake na kuifuta vumbi kisha akaivaa na kuishusha chini kidogo.

“Mbona hujibu mume wangu?”

“Hata sijui nianze wapi kueleza,” alisema baba yake Gladness, ukimya ukatawala katikati yao kisha akaendelea kueleza kuhusu ile simu.

Kama walivyokuwa wamepewa maagizo na polisi ya kuhakikisha wanawataarifu kuhusu kila kinachoendelea, baba yake Gladness alitoka mpaka kituo cha polisi na kueleza kuhusu simu hiyo aliyopigiwa lakini haikuwa rahisi kujua chochote kwa sababu mpigaji alitumia simu ya mezani.

Taarifa hizo ziliamsha upya juhudi za kumtafuta Gladness, askari wengi zaidi wakaongezwa kwa ajili ya kazi hiyo, wakiwemo kutoka kitengo cha teknolojia ya mawasiliano (IT) ambao walianza kufuatilia mawasiliano yake ya simu.

“Kwani simu yake anayotumia siku zote iko wapi?”

“Wakati anatekwa simu alikuwa nayo mfukoni lakini haikuwa na chaji ya kutosha nadhani ilizima muda mfupi baadaye maana mpaka leo haipatikani hewani.”

“Hebu taja namba zake,” alisema askari mmoja akiwa nyuma ya mtambo mkubwa wa mawasiliano uliokuwa umeunganishwa na kompyuta. Baada ya Ben na baba yake Gladness kuitaja namba hiyo, askari yule alianza kazi ya kuitafuta simu hiyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya GPS (Global Positioning System), ramani kubwa ya satellite ikafunguka huku kitufe chekundu kikizunguka katikati ya ramani hiyo na muda mfupi baadaye, mlio kama wa kubipu ulisikika kisha kile kitufe chekundu kikawa kinawaka na kuzima.

“Huyu hapa! Tumempata,” alisema askari huyo huku akiisogeza karibu ile ramani, akawa anasoma namba na muda mfupi baadaye, aliwaambia kwamba inaonesha simu ya Gladness ipo ndani ya msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe mkoani Pwani.

“Inaonesha ipo ndani ya jengo lisilokaliwa na watu, ndani kabisa ya msitu huo, alisema askari huyo huku akichukua simu ya upepo na kuanza kuto taarifa kwa wenzake, pilikapilika zikaongezeka ndani ya kituo hicho na muda mfupi baadaye, askari wenye silaha wakaondoka wakiwa kwenye magari mawili ya polisi.

Baada ya kufika kwenye msitu huo, walifuata maelekezo ya wenzao waliokuwa kwenye mitambo na kufanikiwa kumuokoa Gladness aliyekuwa amefungiwa ndani ya jengo chakavu, ndani ya chumba kichafu kisicho na mwanga wala hewa ya kutosha, akiwa hajitambui.

“Gladness! Gladness my daughter! Wake up my love, wake up,” alisema baba yake Gladness ambaye aliongozana na askari hao, akawa anamtingisha mwanaye ambaye bado hakuwa akijitambua.

Machozi yakawa yanamtoka akiwa ni kama haamini macho yake, harakaharaka Gladness akatolewa ndani ya jengo hilo na kupandishwa kwenye gari, akakimbizwa hospitali huku askari wengine wakibaki eneo hilo kuendelea na msako mkali wa kuwatafuta wote waliokuwa nyuma ya tukio hilo.

Gladness alipelekwa moja kwa moja mpaka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alipokelewa na kukimbizwa wodini, akalazwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

4 Comments
  1. ester mwaisyula says

    Mbona hadithi haziendelei jaman

  2. neyma says

    me naacha hata kuingia huku sijui mmepatwa na nn global hakuna muendelezo wa hadithi

  3. merceys says

    yani sikuiz shigongo hatukuelewi mashabiki zako huja post hadithi za muendelezo takriban mamiez kadhaa sasa ni nini tatizo

  4. abubakari makumbusya says

    Hadithi tamu ila muendelezo tu ndo tatizo

Leave A Reply