The House of Favourite Newspapers

Tishio Ugonjwa Uliyomuua Seth Bosco

0

  ‘NI TISHIO’ ndivyo unavyoweza kuutafsiri ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo ambao wiki iliyopita uliongezea pigo lingine katika familia ya Flora Mtegoa ‘Mama Kanumba’ baada ya Seth Bosco kufariki Desemba 7, mwaka huu.

 

Seth ambaye ni mdogo wa aliyekuwa mwigizaji maarufu wa filamu nchini, marehemu Steven Charles Kanumba, alifariki dunia nyumbani kwao Kimara Temboni jijini Dar es Salaam baada ya kuugua tatizo la uti wa mgongo kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu.

 

Tatizo hilo lilitokana na uvimbe ndani ya uti wa mgongo uliosababisha apooze nusu ya mwili wake sehemu ya chini hata alipofanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe, hakupata nafuu.

 

Mshtuko wa kifo chake, umeelezwa kuacha simanzi huku kasi ya ukuaji wa tatizo la uti wa mgongo nchini ikizidi kutishia afya za Watanzania wengine.

 

Hali hiyo inachangiwa na idadi kubwa ya Watanzania wanaofika katika hospitali mbalimbali nchini kupata matibabu ya maumivu ya mgongo ambayo huchukua muda mrefu kubainika chanzo cha tatizo hilo kuwa ni homa ya uti wa mgongo.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa mwaka 2017, zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo nchini ni 7,363, ilhali duniani ugonjwa huo unasababisha vifo 33,000 sawa na asilimia 14.86 kwa mwaka.

 

Kasi ya ugonjwa huo inazidi kuongezeka kwa kuwa mwaka 2009 kulikuwa na vifo 2,000 lakini sasa vifo zaidi ya 40,000 hutokea kila mwaka duniani.

 

Homa ya uti wa mgongo ni nini?

Kwa mujibu wa Dk Godfrey Chale; ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aitwaye Neisseria meningitidis au vimelea wa fangasi ambao kitaalamu wanaitwa Coccoidiodomycosis na Cryptococci meningetides.

 

Dk Chale aliliambia gazeti hili kuwa, vimelea vingine vinavyoweza kusababisha ugonjwa huu ni Betastreptococci, Hemophilus influenza, Escherichia coli, Listeria monocytogenes, Streptococci pneumoniae na Mycobacteria tuberculosis, ambao pia ni maarufu kwa kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu.

“Mbali na bakteria hao, homa hii pia husababishwa na virusi aina ya Herpes simplex type 2, ambavyo husababisha Ukimwi (HIV).

Ugonjwa huu unapatikana kwa binadamu tu, ambapo asilimia 50 ya wagonjwa hupoteza maisha haraka iwapo hataanza matibabu mapema,” alisema.

 

Alisema huu ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayoua haraka kwa sababu hutokea baada ya utando unaofunika ubongo pamoja na uti wa mgongo kupata maambukizi.

“Homa ya uti wa mgongo inaweza kuathiri ubongo na kusababisha mgonjwa kupoteza uwezo wa kusikia au kuelewa na kunyumbulisha mambo mbalimbali,” alisema.

 

CHANZO CHAKE

Dk. Chale alisema ugonjwa huu unaweza kuambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia njia ya hewa au kwa kugusa majimaji kama mate ya mtu ambaye tayari ni mgonjwa.

Alisema kuwa, huwa unaambukizwa kwa urahisi na kwa kasi iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa mwenye maambukizi ya muda mrefu.

 

“Uambukizo unaweza kutokea iwapo mgonjwa atapiga chafya au kugusa mate yake. Kasi ya maambukizi pia inatokea iwapo mtu ataishi kwa karibu ndani ya nyumba moja na mgonjwa na kula naye chombo kimoja.”

 

DALILI ZA UGONJWA

Dk Chale ambaye amehudumu hospitali mbalimbali za serikali na pia ni mkurugen zi wa kliniki moja iliyopo Kwa Msuguri Dar, alisema dalili za ugonjwa huu huanza kujitokeza kuanzia siku ya pili hadi ya 10 baada ya kupata maambukizi.

 

Alizitaja dalili hizo kuwa ni pamoja na shingo kukakamaa na kuwa ngumu isivyo kawaida, homa kali, kutokupenda mwanga mkali, tatizo ambalo kitaalamu huitwa photophobia, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma, kutapika na wakati mwingine mgonjwa anaweza kupoteza fahamu.

 

Aliongeza viashiria vingine kuwa ni mgonjwa wa mgongo kuhisi maumivu kwenye uti.

“Wakati mwingine mgonjwa anapoelekezwa kujitahidi kukunja shingo, miguu, paja pamoja na goti navyo hujikunja – hii huitwa ishara ya Brudzinski au Brudzinski’s sign,” anasema Dk. Chale na kuongeza:

“Watoto ambao wana Kifua Kikuu (TB) wakati mwingine hupata TB ya ubongo na uti wa mgongo (meningitis) wakiwa na umri wa miezi michache tu,” alisema.

 

UCHUNGUZI

Alisema wakati wa uchunguzi damu pia inaweza kutumika kuotesha vimelea maabara ili kugundua aina ya vimelea na dawa gani nzuri zinazofaa kwa ajili ya matibabu (culture and sensitivity).

“Kipimo kingine ni cha kuchukua maji ya uti wa mgongo wa mgonjwa na kuyachunguza maabara ili kutambua uwepo wa vimelea, aina ya vimelea na dawa zinazofaa kuwatibu (Lumbar puncture).

 

“Kwa baadhi ya maeneo yenye vifaa kama CT-scan na MRI, mgonjwa anaweza kuchunguzwa kwa kutumia vifaa hivyo ili kufahamu uwepo wa ugonjwa, sehemu ulipo na madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huo,” anasema daktari huyo.

 

MATIBABU

Alisema kuwa kwa wagonjwa waliopoteza fahamu, ni vizuri kwanza kuhakikisha wanapumua vizuri na njia za hewa ziko wazi.

“Iwapo itathibitika kuwa bakteria ndiyo wanaosababisha ugonjwa huu, mgonjwa anaweza kupewa mojawapo ya dawa za antibiotiki kama Cefotaxime au Cefriaxone.

 

“Kuna baadhi ya madaktari hupendelea kuongeza dawa za steroids kama dexamethasone ambazo nazo husaidia kwenye matibabu,” anasema na kuongeza:

“Iwapo itathibitika ugonjwa huu umesababishwa na virusi, dawa aina ya Acyclovir inaweza kutumika, ikithibitika kuwa vimelea waliosababisha ugonjwa huu ni wa kundi la fungus, daktari hutoa dawa ya Amphotericin B au flucytosine.”

 

Alisema kuwa dawa hizo huambatana na za kushusha homa na kuondoa maumivu ya kichwa kama Paracetamol.

Alisema uti wa mgongo unaweza kusababisha kuamshwa kwa chembechembe za damu ambazo husababisha damu kuganda, ambapo kitaalamu huitwa Disseminated Intravascular Coagulopathy (DIC).

 

Daktari huyo alisema wakati mwingine ugonjwa huo unaweza kusababisha kuvuja damu katika tezi za adrenalin hatimaye kupata ugonjwa unaojulikana kwa jina la kitaalamu Waterhouse friderichsen syndrome.

Kwa upande wa watoto, alisema unaweza kumsababishia kuwa na kichwa kikubwa (hydrocephalus).

 

NAMNA YA KUJIKINGA

Aidha, Dakta huyo alisema kwa kuwa bakteria na virusi waletao homa ya uti wa mgongo waenezwa kupitia kukohoa, kupiga chafya, kubusiana na kushirikiana vyombo, mswaki au sigara, hatua zifuatazo zinaweza kusaidia;

 

Kuosha mikono. Osha mikono yako kwa makini kuzuia kuenea kwa vijidudu. Wafundishe watoto wako kuosha mikono ipaswavyo kila wakati, hasa kabla ya kula, baada ya kujisaidia, baada ya kuwa kwenye makundi ya watu na baada ya kuchezea wanyama.

 

Usafi. Usishiriki vinywaji, chakula, mirija, miswaki na mtu mwingine. Pia wafundishe watoto kutoshiriki vitu hivi.

Kutunza afya. Linda kinga za mwili wako kwa kupata muda wa kutosha wa kujipumzisha, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kula chakula bora chenye matunda mengi, mboga na nafaka nzima.

 

Kuziba mdomo. Unapokohoa au kupiga chafya ziba mdomo wako na pua.

Kama ni mjamzito, kuwa mwangalifu na chakula. Jilinde kwa kupika nyama kwa moto mkali (74C). Kuwa makini na jibini.

Hata hivyo, Dk. Chale alisisitiza watanzania kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kugundua dalili za mapema na kupatiwa tiba kabla madhara makubwa hayajatokea.

 

MAZISHI YA SETH

Mwili wa msanii huyo wa filamu ulizikwa juzi saa 10 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar.

Mazishi yake yalihudhuruwa na baadhi ya wasanii wenzake kama Blandina Chagula ‘Johari’ Maya, Steve Nyerere, Ray Kigosi, Chuchu Hans pamoja na viongozi wa Kampuni ya Global Publishers Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo, Meneja Mkuu, Abdalah Mrisho, na Mhariri Mtendaji, Saleh Ally ‘Jembe.’

Hata hivyo, baadhi ya wasanii wenye majina makubwa nchini hawakuhudhuria mazishia hayo ambapo baadhi ya watu waliuliza;

 

“Mbona Lulu, Wema, Uwoya, Aunt Ezekiel na wasanii wengine hatuwaoni na walikuwa karibu sana na Kanumba? Sasa kama waliweza kuja kwenye msiba wa Kanumba kwa nini wameshindwa kuja kwenye msiba wa mdogo wake, mm!,” alisikika mwandada mmoja akimuuliza mwenzake ambapo hata hivyo; hakuweza kupatiwa jibu la swali lake.

Stori: WAANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply