Tshishimbi, Yondani Wafanya Kikao Kizito Yanga

NAHODHA Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Papy Tshishimbi, amepanga kukutana na mabeki wa timu hiyo kwa ajili ya kufanyia kazi changamoto ya kuruhusu mabao kila mchezo na anaamini watarekebisha tatizo hilo haraka.

 

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba utakaopigwa Januari 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Yanga katika mchezo uliopita wa ligi iliruhusu bao la saba tangu kuanza msimu huu katika ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Alliance Schools ikiwa imeshuka uwanjani mara saba. Yanga ina wastani wa kufungwa bao moja katika kila mchezo, hali inayofanya wakutane kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuhakikisha hawaruhusu mabao kwenye michezo ijayo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Tshishimbi alisema kuwa kaimu kocha wao Charles Mkwasa anawaelekeza jinsi ya kuzuia ili wasifungwe, lakini bado wanaendelea kuruhusu mabao, hivyo hawataki kuona hilo likiendelea.

 

“Kocha anatuelekeza jinsi ya kuzuia ili tusifungwe lakini sisi kama wachezaji pia tunazungumza turekebishe makosa haya mnayoyaona yakitokea katika michezo yote ya ligi tuliyocheza.

 

“Hivyo, tumepanga kukutana mabeki na viungo wakabaji kwa ajili ya kuweka mikakati hiyo ya kutofanya makosa ya kizembe yatakayotufanya turuhusu mabao kizembe golini kwetu,” alisema Tshishimbi.


Loading...

Toa comment