The House of Favourite Newspapers

Ubora wa radio iwe na pa kuzimia

SHOGAANGU miye upooo? Nishaupiga mswaki tena, ruksa kukupasha; ukiwa na nongwa ya senene kuficha kichwa watu watakuchezea mkia, heee heeeyaaa.  Cheko hilo shogaangu usiseme ni la heri, hapa michambo ni nyumbani kwake; Pwani hakuchumwi maembe bibiye hivyo usinibebee chumvi miye, huku kwetu ni mwendo wa chokochoko za pweza kwenye miamba. Kama siku kumekucha vibaya ni leo; ila raha ya kero uitapike panapohusika, upooo?

Maana kuna watu kila siku wananiona mswahiliswahili, basi hawachambiki hata wakichambwa kwa dodoki. We toka lini radio ikakosa pa kuzimia? Kuna watu wanavamia shoo zisizowahusu, wametoka wanakotoka kuja mjini, basi wanakopi na kupesti kila kitu bila kujua kanuni zake.

Haya shogaangu weye hayo makelele ya uwanjani unayaletaje sebuleni walipoketi watu; unataka kuwajulisha kuwa umefungwa la pili? Heeh heeee!! Majirani zako wamekata lini tiketi za kuingia kwenye mpambano wenu mpaka uwaletee mayowe ya uwanja wako wa sita kwa sita. Shogaangu si kila mchezo unahitaji kelele michezo mingine ni gofu inachezwa kistaarabu.

We watu wako sebuleni au nyumbani kwao wana mambi yao halafu wewe kwa kukosa kwako haya unaanza kuwawangia na staili zako za ‘oooshi, hayaaa’; wamekutuma uwaambie unachojisikia? Koma bibieee, tena ukomeke hasa! Hiyo radio yako kama imetengenezwa bila sehemu ya kuzimia basi ni feki; teeenaaa ni mchina orijino; upoooo?

Usinikazie meno sijakulisha ndimu miye; nimekupa mambo ya kikubwa shurti uyapokee na yakuingie sehemu yake haswaaaa, utulieee kama maji mtungini. Mjini hapa usije pupa ukadhani kila mchezo unataka mayowe; ukijua pa kuwashia pa kuzimia napo upajue.

Ifike mahali uchague mchezo gani unataka kelele na upi hauhitaji kelele. Siyo watoto hawajalala wewe kuguswa kiuno kidogo tu unaanza kero zako unashangilia kila pasi hata mipira ya faulo, loooh! Shogaangu kuna wakati mambo yanataka kimyakimya, ndizi tamu tena tamu kwelikweli lakini haitafunwi kama mhogo, upooo?

Usijisahaulishe mimi naitwa Shangingi mstaafu unaweza kuniita Nasra; hivyo usijione mjuzi nimeyajua hayo kabla wewe hujaja mjini, hivyo tuheshimiane shogaangu! Leo naomba niishie hapa, waliokufundisha kuwasha radio wakuoneshe na pa kuzimia ili usikere watu; upooo?

Comments are closed.