The House of Favourite Newspapers

Ufahamu ugonjwa wa kifua kikuu (Tuberculosis- TB)

UGONJWA wa kifua kikuu kitaalamu huitwa Tuberculosis ambao kwa kifupi ni TB, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis.  Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ng’ombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na kadhalika.

Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system. Mycobacteria bovis ambayo huathiri ngombe, inaweza kumuambukiza binadamu kama atakula bidhaa zinazotokana na maziwa ya ngombe ambayo yameathirika na bakteria hawa kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream nk. Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.

Kuna aina kuu tatu za ugonjwa wa kifua kikuu: Kifua kikuu kinachosababisha madhara (Active tuberculosis) – Hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa bakteria wasisababishe madhara.

Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yeyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele; iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu. Ugonjwa usiosababisha madhara (Inactive tuberculosis) – Kwa kitaalamu pia unaitwa latent TB. Mtu mwenye latent TB, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kumuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu.

Aina hii inaweza kujirudia baadaye na kuathiri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadaye huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.

Ugonjwa uliosambaa mwilini (Milliary tuberculosis) – Hii hutokea pale ambapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo, mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system. Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.

Sababu za mtu kupata maradhi haya ni unywaji wa pombe kupindukia, kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kwenye mabasi ya mjini (daladala), kuwa na magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari nk.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.