The House of Favourite Newspapers

Ukawa kutikisa bungeni leo

0

ukawa_4Na Daniel Mbega, Dodoma

Wapanga kufanya zomeazomea yao wakati rais akihutubia

WABUNGE wanaotokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanalitikisa bunge leo hii kwa kupanga kuisusia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli lakini wanaweza kufanya kituko cha mwaka ikiwa wataendelea na mipango yao ya kumzomea rais huyo.

Taarifa zinaeleza kwamba, wabunge hao wamepanga kumzomea Rais Magufuli katika hotuba yake hiyo ya kwanza kwa Bunge la 11 huku wakidai hakuna uhalali wa yeye kuhutubia wakati Zanzibar hali siyo shwari.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Ukawa kimedai kwamba, kususia hotuba ni jambo ambalo lilikuwa wazi hata kama kusingekuwa na suala la Zanzibar kwa sababu hawakuridhika na matokeo ya kura zilizompa ushindi Dk. Magufuli dhidi ya mgombea wao, Edward Lowassa lakini kitendo cha kumzomea kabla hawajatoka ukumbini ndicho kitakacholeta mtikisiko mkubwa.

“Wamepanga kumzomea Rais Magufuli mara atapoanza kuhutubia, hii ni hatari kwa sababu itatikisa nchi pia kutokana na ukweli kwamba hata viongozi wa nje wanaweza kuwepo,” kilisema chanzo hicho.

Gazeti hili liliwatafuta baadhi ya wabunge kutoka kambi hiyo lakini wengi waligoma kuzungumzia kitakachotokea leo hii mara walipomaliza kikao chao baada ya bunge kuahirishwa majira ya saa 7:45 jana mchana.

Hata hivyo, mapema kabla ya shughuli za kumthibitisha Waziri Mkuu Mpya, Kassim Majaliwa, wabunge hao walisema msimamo wao ni wa kupinga hotuba ya Rais Magufuli kama walivyoazimia juzi.

“Tumeshasema tangu jana (juzi) hatukubali Rais Magufuli ahutubie bunge wakati Zanzibar hakujapatikana suluhu, (Dk. Ali Mohammed) Shein anaongoza kwa Katiba ipi?” alihoji Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.

Jumatano jioni, wabunge wanaounda Ukawa walieleza kwamba walikuwa wamemwandikia barua Spika wa Bunge Job Ndugai kueleza msimamo wao wa kupinga hotuba ya Rais Magufuli na kupinga Dk. Shein kuingia bungeni kwa kuwa si rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, wabunge hao walisema walitaka kujua uhalali wa Rais Magufuli kuhutubia Bunge bila matokeo ya Rais wa Zanzibar kujulikana.

“Hatutakubali katiba ivunjwe kwa kumruhusu Dk. Shein kuingia bungeni wakati muda wake wa kushika madaraka ulishapita,” alisema Mbowe akiwa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015, huku matokeo yakiwa bado kutangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema baada ya chama chake kukusanya fomu za matokeo vituoni na kufanya majumuisho, yeye alipata kura 200,007 hivyo alishinda kwa asilimia

52.87.

“Hakuna shaka yoyote, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanguka kwa mara ya kwanza tangu kilipoanzishwa mwaka 1977,” alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa matokeo hayo, mgombea wa CCM anayetetea nafasi yake, Dk.

Shein, alipata kura 178,363, sawa na asilimia 47.13. Hata hivyo, Zec iliamua kufuta matokeo ya uchaguzi huo kwa maelezo kwamba kulikuwa na dosari mbalimbali hasa katika majimbo ya kisiwani Pemba.

Pamoja na shinikizo kutoka sehemu mbalimbali kwamba uamuzi huo wa Zec ubatilishwe, bado tume hiyo imeshikilia msimamo wake huo na sasa uchaguzi utarudiwa tena.

Jitihada za mazungumzo baina ya pande zinazolumbana bado hazijazaa matunda, jambo ambalo limevifanya visiwa hivyo kuwa katika hali ya sintofahamu.

HISTORIA YA WAPINZANI KUTOKA NJE

Kwa vipindi tofauti wabunge wa upinzani wamekuwa na desturi ya kutoka nje ya bunge kutokana na kutokukubaliana na baadhi ya mambo:

Kwa mara ya kwanza Wapinzani wakiongozwa na Chadema wakiwa ndicho chama kikuu cha upinzani, walitoka nje ya ukumbi wa Bunge, Novemba 18, 2010 wakipinga hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, waliyemuelezea kuwa ushindi wake wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huo, haukuwa halali.

Hata hivyo, Rais Kikwete aliendelea na hotuba yake na wapinzani hao walirejea bungeni na kuungana na wabunge wa vyama vingine kujadili hotuba hiyo kama kanuni za Bunge zinavyosema.

Mara ya pili Wabunge wa Chadema walitoka bungeni Februari 9, 2011 wakipinga kubadilishwa kwa kanuni ya Bunge iliyokuwa ikikitambua chama hicho kama ndicho kinachounda kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Kanuni hiyo ilitakiwa kusomeka kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni wabunge wote wa vyama vya upinzani isipokuwa chama tawala, kitu ambacho Chadema walipinga na kutaka chama kikuu cha upinzani kiwe ni kile kilichokidhi vigezo vya kupata asilimia 12.5 ya wabunge wote mwaka huo.

Mara ya tatu Wabunge wa upinzani walitoka nje ya ukumbi wa Bunge Novemba 14, 2011 kwa madai ya kutoafikiana na kile walichodai kuendelea kujadiliwa kwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wakati ukiwa haujatimiza masharti ya kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

Wabunge hao walitoka mara baada ya Mbunge wa Singida Mashariki na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wakati huo, Tundu Lissu kuhitimisha kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyopendekeza kusitishwa kwa mjadala huo ili maoni ya wananchi yakusanywe kwanza.

Kwa mara ya nne Wapinzani wa vyama vya Chadema na Cuf, walitoka nje ya ukumbi wa Bunge Jumatano ya Septemba 4, mwaka 2013, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa

Leave A Reply