The House of Favourite Newspapers

Umepoteza matumaini ya ndoa? Elimika!

UKIFANYA tathmini ya ndoa nyingi, ni wachache sana ambao watakuambia wanazifurahia. Wengi watakuambia wapo kwenye mateso mazito, wanatamani kutoka. Matatizo ni mengi kuliko mazuri, waliopo wanatamani kutoka leo au kesho. Kinachobakia ni watu tu kuamua kuvumiliana, wanaogopa aibu ya kuvunja ndoa kwa kuona kwamba watawaambia nini watu ambao walikusanyika na kufanya sherehe kubwa, lakini ndoa imewashinda ndani ya muda mfupi au mrefu kidogo.

Huo ndiyo mtihani, utaona kuna wengine bado hawajaingia kwenye ndoa na wanatamani kuingia, lakini wakizisikia changamoto za ndoa wanaogopa. Wanakosa imani na kitu kinachoitwa ndoa na ndiyo maana wanaamua kuishi bila ndoa kwa muda mrefu.

Katika kipindi cha kuelekea kwenye ndoa, vijana wanakutana na mambo mengi sana ambayo wasipokuwa makini, wanaweza kujikuta wameshindwa hata kuamini falsafa hii ya ndoa. Unakutana na mtu, anakuwa amekata tamaa kabisa ya kuolewa au kuoa.

Mwanamke atakuambia wanaume hawaaminiki, wanaume ni matapeli. Huyo ni mwanamke ambaye anakuwa ameshapata maumivu ya mapenzi ya kutosha. Vivyo hivyo kwa mwanaume, naye anakuambia; ‘wanawake wa sasa ni pasua kichwa’.

Mwanamke wa sasa haaminiki, anakuwa na wewe sasa hivi, lakini ukiondoka anakuwa na mtu mwingine. Wapo wanawake ambao wanaishi kama vile wafanyabiashara ya ngono. Ukimuona unaweza usimdhanie, mpole machoni na mnyenyekevu, lakini kumbe upande wake wa pili ni balaa!

Mambo kama haya  ndiyo yanatengeneza chuki, yanatufanya tukinahi kabisa masuala ya uhusiano wa kimapenzi. Inafika mahali mtu anaamua bora tu awe yeye. Haoni tena faida ya kuingia kwenye ndoa maana anayoyaona, anayoyasikia kwa watu yanakatisha tamaa. Wakati ninaandika haya  najua wapo watu ambao wamekata tamaa, mioyo yao imeshakinahi kupenda. Mioyo yao imeshaamua kutopenda tena, zaidi ni kutafuta furaha ya muda tu. Mwanamke anatafuta mtu wa kuburudishana naye kwa muda tu, biashara inaishia hapo.

Mwingine anatafuta tu mwanaume wa kumzalisha, akishapata mtoto, basi anaendelea na maisha yake. Hana muda wa kusema tena anatarajia kuingia kwenye ndoa, haipo kwenye mpango wake maishani.

Na mwanaume vilevile, anatafuta tu mtu wa kuburudishana naye kwa kipindi fulani basi. Kama akipata watoto wawili au watatu hata kama ni kwa wanawake tofauti, kwake hilo ni suala la msingi. Akili yake haiwazi tena kuhusu kufunga ndoa.

Marafiki zangu, leo nataka niwaambie, mnapokutana na changamoto kama hizi kwenye uhusiano msikate tamaa kwani haya ni mapito tu. Kila mtu ana namna ya kufikia kilele cha mafanikio. Kuna wakati ambao tunauita wa Mungu, huo upo tu!

Wewe unaweza kuona kwamba una bahati mbaya, kwamba hukutani na mtu sahihi, lakini nataka nikuhakikishie kwamba wakati wako upo. Wakati wako utakapofika, yaani utashangaa tu mambo yanakuwa mepesi sana.

Umezoea kwamba ili uingie kwenye uhusiano na mtu, lazima upitie mlolongo mrefu sana wa kufahamiana, kujuana vizuri na kuaminiana, lakini wakati wako unapofika wala hakutakuwa na mlolongo mrefu sana.

Mambo yanakwenda yenyewe tu kwenye mstari, unashangaa mnaamua kufunga ndoa, mnaingia kwenye ndoa na kusema; ‘sio kwa akili zetu, bali ni kwa neema na rehema zake Mungu’.

Utasahau mapito yote uliyopitia na kimsingi hayo mapito ilikuwa ni lazima uyapitie ili uweze kufika kwenye kilele cha mafanikio! Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifauta Instagram & Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Comments are closed.