Un- Ending love 85
ILIPOISHIA
Waliosema kwamba ukiona giza linaongezeka ujue mapambazuko yamekaribia hawakukosea. Msemo huo wa wahenga unaonekana kuanza kutimia kwa Jafet Lubongeja na msichana aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote, Anna.
Baada ya kupitia kwenye misukosuko mingi, penzi lao likitawaliwa na machozi, maumivu ndani ya moyo, usaliti na kukataliwa, hatimaye mapambazuko yameanza kuonekana.
Wawili hao walikutana wakiwa bado wadogo, Jafet akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kwimba, Mwanza huku Anna akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru.
Penzi zito likachanua kati yao kiasi cha kumfanya Jafet afikie hatua ya kutoa figo yake moja na kumpa Anna aliyekuwa anasumbuliwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, licha ya wema mkubwa alioufanya Jafet, baadaye wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet baada ya Anna kupona kabisa. Sababu kubwa ya kumchukia ni baada ya kugundua ukweli kwamba kijana huyo alikuwa akitokea kwenye familia maskini sana, wakaona hana hadhi ya kuwa mkwe wao.
Wakafanya kila kilichowezekana na hatimaye wakafanikiwa kuwatenganisha wawili hao. Hata hivyo, baadaye mambo yanaanza kumwendea kombo Anna, anapewa ujauzito na mwanaume mwingine na wazazi wake wanapoamua kuutoa, maradhi yake ya figo yanarudi upya.
Mtu pekee anayekuja kusaidia kumrudishia Anna furaha, akiwa hoi kitandani ni Jafet. Uwepo wake unasababisha msichana huyo apone maradhi yote yaliyokuwa yanamsumbua, jambo linalomshangaza kila mmoja. Mwisho wanatafutiwa chuo nchini Marekani wanakoendelea na masomo kwa bidii.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
ENDELEA
Maandalizi ya mitihani ya kuhitimu chuo yalienda sambamba na maandalizi ya mahafali, wazazi wa pande zote mbili nao kwa upande wao wakaanza kujipanga kwa ajili ya kufanikisha mahafali ya watoto wao. Mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana na Jafet na Anna na kupeana utaratibu wa jinsi mahafali hayo yatakavyokuwa.
Hatimaye siku ya mahafali iliwadia, kutoka nyumbani Tanzania, baba na mama yake Anna walisafiri sambamba na mama yake Jafet ambaye walimlipia kila kitu, kuanzia gharama za kupata hati ya kusafiria, visa mpaka nauli ya ndege ya kwenda na kurudi.
Jafet hakuamini siku hiyo alipopigiwa simu na kuambiwa wajiandae kuwapokea wageni kutoka Tanzania. Awali alihisi lazima watakuwa ni baba na mama yake Anna tu lakini hakuyaamini macho yake alipomuona mama yake akiwa miongoni mwao, akiwa amependeza mno.
“Mama! Siamini macho yangu!”
“Ni mimi mwanangu, Mungu kweli mkubwa, na mimi nimepanda ndege,” alisema mama yake Jafet kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kisukuma, wote wakacheka na kukumbatiana kwa furaha. Jafet na Anna waliwaongoza wageni wao mpaka kwenye ukumbi yalipokuwa yakifanyikia mahafali hayo.
Ilikuwa siku ya furaha sana kwa Anna, Jafet na wazazi wao kwa sababu hatimaye ndoto yao ya miaka mingi ilikuwa ikielekea kutimia.
“Siku ulipokataa kwenda kusomea upadri ulinikasirisha sana moyo wangu, wala sikuwa najua Mungu amekuandalia nini maishani mwako, wabheja gete bhabha! (hongera sana baba!) alisema mama yake Jafet na kumkumbatia tena mwanaye aliyekuwa amevalia joho lililompendeza sana.
Shamrashamra ziliendelea mpaka jioni, ikabidi wazazi wao waende kutafuta hoteli ya kupumzika, tayari kwa maandalizi ya kurudi Tanzania siku iliyokuwa inafuatia, Jafet na Anna wakawasindikiza na kukubaliana kuonana tena asubuhi, wakarudi chuoni kuendelea na sherehe kwani usiku huo kulikuwa na disko maalum kwa ajili ya wanachuo wote.
“Niambie kama kweli utanioa!”
“Lazima nikuoe Anna, tena tukirudi nyumbani tu jambo la kwanza itakuwa ni kukuvalisha pete ya ndoa, hata mama yangu nimeshamwambia na amesema atazungumza na wazazi wako,” alisema Jafet, akamkumbatia Anna na kumbusu, kisha wakagusanisha ndimi zao wakati muziki laini ukiendelea kupigwa ndani ya ukumbi huo, wanachuo wengi wakiendelea kufurahia mahafali.
“Nitafurahi sana Jafet, nimeshasubiri kiasi cha kutosha, nataka kuwa mkeo wa ndoa, nataka nikuzalie watoto wazuri kama baba yao,” alisema Anna kwa hisia za hali ya juu, wakaendelea kukumbatiana huku wakicheza muziki mpaka baadaye kila mmoja alipoanza kuonesha dalili za kuchoka.
Wakaondoka na kwenda kulala, kila mmoja kwenye hosteli yake ambapo asubuhi waliamshana na kwenda mpaka kwenye hoteli waliyofikia wazazi wao. Maandalizi ya safari yakaendelea ambapo baadaye, waliagana na wazazi wao waliofunga safari kuelekea uwanja wa ndege wakati wao wakirudi chuoni.
Siku zilizidi kusonga mbele, hatimaye wakafanya mitihani yao ya mwisho na kusafiri kurejea nchini Tanzania ambapo walipokelewa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na wazazi wa pande zote mbili.
Breki ya kwanza ilikuwa nyumbani kwa akina Anna ambapo kwa kuwa tayari Jafet alishawaambia wazazi wake, iliandaliwa sherehe ndogo ya kuwapongeza wawili hao, Jafet akaitumia nafasi hiyo kumvalisha pete ya uchumba Anna, wawili hao wakaanza ukurasa mpya wakiwa wachumba rasmi.
Walikaa jijini Mwanza kwa siku kadhaa, baadaye wakaondoka pamoja kuelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa akina Jafet. Kutokana na kukaa Marekani kwa kipindi kirefu, mfumo wao wa maisha ulibadilika kabisa, wakawa wanaishi kama Wamarekani weusi.
Baada ya kukaa kijijini kwa siku kadhaa, walirejea jijini Mwanza ambako tayari baba yake Anna alishawafanyia mipango ya kupata kazi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Wakaanza kazi katika hospitali hiyo, Anna akiwa daktari wa figo, Nephrologist, wakati Jafet yeye akiwa ni mtaalamu wa mishipa ya fahamu.
Japokuwa walikuwa wakifanya kazi, bado walikuwa wakiishi nyumbani kwa akina Anna walikotengewa vyumba vyao, huku mipango ya ndoa yao ikizidi kupamba moto.
MIEZI 7 BAADAYE
Jafet alikuwa amevalia suti maridadi ya rangi ya maziwa, huku Anna akiwa amevalia shela kubwa jeupe lililomfanya apendeze kuliko kawaida. Nyuma yao, kulikuwa na wapambe wao ambao nao walivaa nguo zinazofanana na za kwao, muziki wa taratibu ukawa unapigwa huku wakitembea taratibu kuingia ukumbini, shangwe na vifijo vikisikika kila upande.
“Wanameremetaaa! Wanameremetaaa! Wanameremetaaa!” watu wote ukumbini walikuwa wakiimba huku wakipiga vigelegele na shamrashamra za kila aina. Jafet na Anna walikuwa wakiingia ukumbini, baada ya mchana wa siku hiyo kufunga ndoa takatifu katika Kanisa la Kristo Mfalme jijini Mwanza, harusi iliyohudhuriwa na watu wengi na kuweka rekodi ya kipekee jijini humo.
Baada ya kuingia ukumbini, maharusi walienda kukaa sehemu waliyoandaliwa, watu wote wakakaa kwenye siti zao na ratiba zikaendelea kama kawaida. Muda wote mama yake Jafet alikuwa akitokwa na machozi kwani hakuamini kwamba mwanaye huyo, aliyekulia katika mazingira magumu kiasi kile, alikuwa akifunga ndoa ya kifahari kama hiyo, tena akiwa anamuoa msichana mrembo kutoka familia ya kitajiri, Anna. Muda wote akawa anainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake.
Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Anna, alikuwa haamini kwamba hatimaye amekuwa mke halali wa Jafet. Muda wote alikuwa akitazama kidole chake kilichokuwa na pete mbili, ya uchumba na ya ndoa, akawa anajihisi kama yupo ndotoni. Taratibu za ukumbini ziliendelea mpaka saa sita za usiku ambapo maharusi walitoka na kwenda hotelini.
Kesho yake asubuhi wakasafiri kwenda kwenye Visiwa vya Shelisheli kwa ajili ya kula fungate lao.
“Siamini Jafet! Siamini kama kweli leo nimekuwa mke wako, nakupenda sana mume wangu,” alisema Anna, wakiwa wamejilaza kwenye vitanda maalum vya kamba, wakipunga upepo wa baharini, kwenye hoteli ya kitalii ya Coconut Empire kwenye Visiwa vya Shelisheli.
“Nilikuahidi Anna kwamba lazima nitakuoa, namshukuru Mungu kwamba hatimaye umekuwa mke wangu,” alisema Jafet, akamkumbatia Anna na kugusanisha ndimi zao. Muda mfupi baadaye, walibebana msobemsobe mpaka chumbani, wakapeana haki yao ya ndoa.
Siku tatu baadaye, Jafet alipokea simu iliyoonesha kwamba ilikuwa inapigwa kutoka nje ya nchi hiyo, harakaharaka akapokea ambapo sauti ya mwanamke ilimtaarifu kwamba anatakiwa kusoma barua pepe aliyotumiwa kwani ilikuwa muhimu sana.
Harakaharaka Jafet alichukua laptop yake na kuiwasha, Anna akiwa pembeni yake wakafungua upande wa barua pepe.
“Whaaat?” (Niniii?) alisema Jafet akiwa ni kama haamini. Ilikuwa ni barua iliyomtaarifu kwamba alikuwa amechaguliwa kuwa miongoni mwa madaktari watakaoenda kufanya kazi makao makuu ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) jijini Geneva, Uswisi. Barua pepe hiyo ilimueleza kwamba atagharamiwa kila kitu yeye na mkewe, kuanzia nauli, makazi, malazi na atakuwa analipwa mshahara mzuri.
Jafet alibaki amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini, akakaa na mkewe na kujadiliana ambapo walikubaliana kwamba wakubali wito huo. Badala ya kukaa siku thelathini kwenye fungate lao, walikaa siku kumi tu, wakarejea Tanzania ambapo walizungumza na wazazi wa pande zote mbili ambao nao walifurahi sana kusikia taarifa hizo na kuwapongeza wanandoa hao.
Wiki moja baadaye, mipango yote ya safari ilishakamilika, wakasafiri mpaka jijini Geneva, Uswisi na kuyaanza maisha mapya huku Anna akiwa na dalili za ujauzito. Miezi tisa baadaye, alijifungua watoto wawili mapacha, wa kiume na wa kike ambao walizidisha furaha kwenye ndoa yao.
Maisha yakaendelea kwa raha mustarehe huku kila likizo wakifunga safari mpaka nchini Tanzania kuwasalimu wazazi wao. Jafet aliyabadilisha kabisa maisha ya nyumbani kwao. Ile familia ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikidharaulika kwa sababu ya umaskini, ikageuka na kuwa gumzo kutokana na utajiri na mafanikio yaliyopatikana.
Mwisho.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/
nice story
true love does not die
A very nice story….natamani mapenzi kama ya Jafet yangekuwepo kwa ulimwengu wa leo
jamani mapenzi!!!!!!!Uwa yana uwanja mpana saaaaasna uwa ayaelezeki kiraisi,rais
so amazing story!
Nice story ila suleikha kaishia hewani
Naamini mungu atanipa mume mwenye sifa za Japhet
Very amazing!! That is how were are suppossed to be we must show true love to our partiners and fiance’s, may God be with me in selecting girl friend.
inavutia