The House of Favourite Newspapers

Unending Love -54

1

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Hata hivyo, licha ya yote hayo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana naye, jambo linalomuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, mtoto wa balozi wa Tanzania nchini Marekani aliyekuwa akisoma chuo kimoja na Anna. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna anaanza kuona dalili zisizo za kawaida. Anapoenda kupima anagundulika ni mjamzito.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Haiwezekani! Haiwezekani, nasema haiwezekani,” alisema William kwa sauti ya juu huku akianza kuzunguka huku na kule kama mtu aliyechanganyikiwa, kitendo kilichozidi kuivuruga akili ya Anna.

Alishindwa kuelewa ni kwa sababu gani William alionesha ‘kupaniki’ kiasi kile baada ya kupewa taarifa hizo za ujauzito, akajiinamia na kuanza kulia kwa uchungu.

“Huo ni uzembe! Kwani wewe ulikuwa hujui kwamba upo kwenye siku zako za hatari?”

“Lakini William…”

“Lakini nini? Sipo tayari kuzaa na wewe, naomba hilo ulitambue.”

“Wewe si ulisema unanipenda na utanipenda katika hali zote? Kwa nini leo unabadilika na kuwa mkali badala ya kukaa chini ili tujue tunafanya nini na huu ujauzito?”

“Nimeshakwambia, sipo tayari kuzaa na wewe!” alisema William na kuondoka huku akionesha kuwa na jazba kali. Anna alishindwa kuamini kilichotokea, akazidi kulia kwa uchungu huku akijilaumu sana kukubali kumpa William nafasi ya kuwa mwanaume wa kwanza kuujua mwili wake.

Tangu William aondoke kwa hasira, ulipita muda mrefu sana bila kurejea nyumbani hapo, jambo ambalo halikuwa la kawaida tangu alipoenda kumchukua Anna nyumbani kwao, Mwanza kwa ahadi ya kuja kumtembeza jijini Dar es Salaam.

Kwa muda wote huo, Anna alikaa peke yake kwenye jumba la kifahari la akina William, hakuwa na hamu ya kufanya chochote zaidi ya kujifungia chumbani muda wote, hisia chungu zikiendelea kupita ndani ya kichwa chake.

William alirejea nyumbani usiku, majira ya saa nne akiwa amelewa chakari, jambo lililozidi kumchanganya Anna. Haikuwa kawaida ya William kuondoka peke yake na kwenda kulewa kiasi hicho. Pale alipohitaji waende kustarehe, alikuwa akimchukua Anna na kuondoka naye na hakuwa na kawaida ya kunywa pombe na kulewa kiasi hicho.

“Anna! Umekula?” alihoji William kwa sauti ya kilevi huku akipepesuka, macho yake yakijifumba yenyewe kutokana na kuzidiwa na kilevi. Anna alitingisha kichwa kukubali kwamba ameshakula wakati haikuwa kweli.

“Sasa nataka tuzungumze kuhusu huo mzigo wako,” alisema William huku akikaa pembeni ya kitanda cha Anna.

“Nimeshakwambia kwamba mimi sipo tayari kuzaa na wewe kwa sasa. Jambo la msingi nataka nikupeleke hospitali ukatoe huo ujauzito,” alisema William huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara, kauli ambayo ilimshtua mno Anna.

Ni kweli na yeye hakuwa tayari kubeba ujauzito kwa kipindi hicho lakini hakutegemea kwamba William anaweza kuzungumza suala hilo kwa urahisi namna hiyo, bila hata wawili hao kukaa na kuzungumza kwa kirefu juu ya nini cha kufanya na athari zinazoweza kutokea.

Kauli hiyo ilipenya kwenye moyo wa Anna kama mkuki wenye ncha kali, akashindwa cha kujibu zaidi ya kuendelea kujiinamia, machozi mengi yakimtoka na kuulowanisha uso wake.

“Nimeshazungumza na daktari, jiandae kesho asubuhi na mapema nitakupeleka tukamalize kazi,” alisema William na bila hata kusubiri kusikia Anna atazungumza nini, alitoka na kuelekea chumbani kwake, akajitupa kitandani bila hata kuvua viatu na muda mfupi baadaye, alianza kusikika akikoroma kwa nguvu.

Usiku huo ulikuwa mrefu mno kwa Anna, hakuwahi kufikiria hata mara moja kwamba ipo siku na yeye ataingia kwenye orodha ya wanawake makatili wanaotoa mimba na kuviua viumbe vilivyomo ndani ya matumbo yao.

“Hapana! Haiwezekani! Sipo tayari kutoa ujauzito hata kwa mtutu wa bunduki,” alijisemea Anna na kuinuka pale kitandani. Alipotazama saa kwenye simu yake, ilionesha kuwa tayari ilikuwa imetimia saa tano za usiku.

Bila kupoteza muda, alianza kukusanya kila kilichokuwa chake kwani alishaona William hana nia nzuri, akafungasha vitu vyake vyote kwenye begi lake na kujiandaa kwa safari ya kurejea jijini Mwanza asubuhi ya siku iliyokuwa inafuatia.

Kwa kuwa wakati aliposafiri na William kutoka Mwanza kuja jijini Dar es Salaam wazazi wake walimkatia tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi (go and return), hakupata shida kuhusu usafiri.

Alichokifanya ilikuwa ni kupiga simu kwenye ofisi za shirika la ndege alikokatiwa tiketi na kuwataarifu kwamba alikuwa akihitaji kurejea Mwanza asubuhi ya siku iliyokuwa inafuatia. Kwa bahati nzuri, alipata nafasi kwenye ndege ya saa tatu asubuhi, akamshukuru Mungu wake.

Hakutaka kumwambia chochote William na kwa jinsi alivyokuwa amelewa, alikuwa na uhakika kwamba atachelewa sana kuzinduka asubuhi, akapanga kutumia muda huo kuondoka kuelekea uwanja wa ndege.

Saa kumi na mbili asubuhi, tayari Anna alishaamka na kujiandaa kwa kila kitu, akabeba begi lake na kutoka kimyakimya, William akiwa amelala fofofo akiendelea kukoroma. Alitoka mpaka nje ambapo alisimamisha teksi na kumuelekeza dereva kumpeleka uwanja wa ndege.

Kama ilivyo kawaida ya Jiji la Dar es Salaam, asubuhi hiyo kulikuwa na foleni kubwa ya magari barabarani, hali iliyomlazimu dereva kuanza kutafuta njia za mkato ili amuwahishe mteja wake uwanja wa ndege.

Kwa kuwa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ilikuwa haipitiki kabisa, ilibidi aingie kwenye barabara za mitaani na hatimaye akatokezea kwenye Barabara ya Umoja wa Mataifa ambayo angalau haikuwa na foleni kubwa, safari ikaendelea.

“Dereva hebu simama! Simama mara moja,” Anna alisema kwa sauti kubwa, dereva akawasha ‘indiketa’ ya upande wa kushoto, akapunguza mwendo na kulitoa gari pembeni ya barabara, akasimama jirani kabisa na Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).

Gari liliposimama tu, harakaharaka Anna alifungua mlango wa gari na kuteremka, akavuka barabara bila hata kutazama magari na kukimbilia upande wa pili ambapo kundi la wanachuo wa chuo hicho cha udaktari, waliokuwa wamevalia makoti meupe walikuwa wakitembea pembeni ya barabara.

“Jafet! Jafet!” sauti ya msichana iliyoonekana kutokuwa ngeni masikioni mwake, ndiyo iliyomshtua Jafet aliyekuwa amezama kwenye mazungumzo ya kawaida na wanachuo wenzake.

Harakaharaka akageuka nyuma na kutazama sauti hiyo ilikokuwa inatokea, Jafet akashindwa kuyaamini macho yake kwa alichokuwa anakiona. Ilibidi afikiche macho yake, akihisi labda yupo kwenye ndoto ya kusisimua.

“Anna! Ni wewe?”

Je, nini kilifuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi. 

1 Comment
  1. stellah says

    hadithi tamu sana naomba ucwe unachelewa kuitupia huku

Leave A Reply