The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 80

7

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa msichana huyo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.

Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India.

Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Wanafunga safari ya kurejea Tanzania huku mara kwa mara Anna akitafuta upenyo wa kumpa mapenzi Jafet lakini inashindikana. Hatimaye wanaianza safari ya kuelekea Mwanza.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Muda mfupi baadaye, ndege waliyopanda ilianza kuondoka na safari ya kuelekea jijini Mwanza ikapamba moto.

“Jafet! Unanipenda kweli?”

“Kwa nini unapenda kuniuliza hilo swali Anna? Nikwambie mara ngapi ili uamini?”

“Sijiamini tena Jafet, najua katika kipindi ambacho nilikuwa mbali na wewe ulimkabidhi mtu mwingine moyo wako na inaonesha anakupenda sana,” alisema Anna kwa huzuni.

“Lakini kama suala ni hilo hata wewe uliniacha na kwenda kuwa na mwanaume mwingine, tena kibaya zaidi mkafikia hatua ya kupeana ujauzito. Kama kuumia mimi ndiyo napaswa kuumia zaidi yako.”

“Unachokisema ni kweli Jafet lakini tofauti yetu mimi niliangukia kwa mtu asiye sahihi na sijawahi kuacha kukupenda lakini wewe ni tofauti kwa sababu umempata mtu anayekupenda kwa dhati na wewe unampenda, huoni tofauti hapo?” alisema Anna na kumfanya Jafet akose cha kujibu kwa sababu alichokuwa anakisema kilikuwa na ukweli kwa kiasi fulani ndani yake.

Akashusha pumzi ndefu na kumtazama Anna usoni, akionesha kuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake. Sauti ya mhudumu wa ndege hiyo waliyokuwa wamepanda iliyokuwa ikiwataka abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye uwanja wa jijini Mwanza ndiyo iliyowazindua kutoka kwenye mazungumzo hayo.

Jafet akamsaidia Anna kufunga mkanda kwenye siti yake kisha akambusu mdomoni na kukaa kwenye siti yake, kitendo kilichomfurahisha sana msichana huyo. Ndege ikaanza kuinama upande wa mbele, ikaendelea kushuka kwa kasi kubwa na hatimaye ikatua kwenye Uwanja wa  Ndege wa Mwanza.

“Finally we are back home, with someone I love the most! Thanks be unto God,” (Hatimaye tumerejea nyumbani, nikiwa na mtu ninayempenda kuliko kitu kingine chochote! Shukrani zimuendee Mungu) alisema Anna wakati akiinuka kwenye siti aliyokuwa amekaa, akasimama na kumkumbatia Jafet kwa nguvu.

“Nakupenda sana Jafet, hicho ndiyo kitu pekee ambacho hakiwezi kuja kubadilika kwenye maisha yangu. Nilishaweka nadhiri kwamba nitakupenda kadiri ya uwezo wangu wote mpaka siku naingia kaburini,” alisema Anna na kumbusu Jafet mdomoni, bila kujali abiria wengine wa ndege hiyo waliokuwa wakiwatazama.

Wakatoka na kushuka kwenye ngazi za ndege hiyo mpaka chini, wakaungana na wazazi wao ambao tayari walishateremka kabla yao, wakaelekea kwenye jengo la uwanja huo na kuchukua mizigo yao, wakatoka mpaka nje walikokuta ndugu zao wengi wakiwa wanawasubiri, wengi wakiwa na shauku kubwa ya kumuona Anna kwa sababu hali aliyoondoka nayo ilikuwa tete.

“Karibu nyumbani Anna!” lilisomeka bango lililokuwa limeshikwa na mmoja wa ndugu wa familia hiyo, wengine wakiwa wamebeba maua na kadi za kuwakaribisha wote na kuwapa pole kwa safari ndefu.

Mwonekano wa Anna ulikuwa tofauti kabisa na wakati anaondoka, jambo lililowaacha midomo wazi watu wote waliokuja kuwapokea uwanjani hapo.

“Tulitegemea utashushwa kwenye ndege ukiwa juu ya kitanda au kiti cha magurudumu lakini unatembea mwenyewe, tena unaonesha kuwa na nguvu zako kweli Mungu ametenda miujiza,” ndugu mmoja alishindwa kujizuia na kuongea kwa sauti, kauli iliyosababisha ndugu wengine wote kulipuka kwa shangwe na vigelegele kwani ni kweli Anna alikuwa amepona kabisa.

Baada ya dakika kadhaa za shangwe na furaha uwanjani hapo, msafara wa magari matatu ulianza safari ya kuelekea nyumbani kwa akina Anna huku kila mmoja akionesha kuwa na furaha kuliko kawaida. Uwepo wa Jafet kwenye msafara huo lilikuwa ni jambo jingine lililowaacha wengi midomo wazi.

Hakuna aliyeelewa nini kimetokea mpaka kijana huyo awepo kwenye msafara huo kwa sababu wengi walikuwa wanajua kilichomtokea baada ya mama yake Anna kumkataa kwa sababu alikuwa akitokea kwenye familia ya kimaskini.

Baada ya kuwasili nyumbani, wageni walipata muda wa kupumzika huku kukiandaliwa tafrija fupi kwa ajili ya kumshukuru Mungu. Ndugu wa karibu, majirani na marafiki wa familia hiyo wakajumuika kula, kunywa na kucheza muziki. Baadaye walitawanyika na kuwapa nafasi ya kupumzika.

“Inabidi kesho tufunge safari kuelekea nyumbani kwa akina Jafet, kijijini Rwamgasa kisha baada ya hapo tumruhusu Jafet arudi chuoni maana anazidi kukosa masomo,” alisema baba yake Anna, wote wakiwa wamepumzika sebuleni baada ya chakula cha usiku.

Anna ambaye alikuwa amejilaza kwenye miguu ya Jafet, aliposikia kwamba Jafet anatakiwa kuondoka, harakaharaka aliinuka na kuleta hoja iliyowaacha wote midomo wazi.

“Na mimi nataka nikasome Dar es Salaam kwenye chuo anachosoma Jafet, sitaki tena kwenda Marekani.”

“Lakini Anna…”

“Lakini nini mama? Mi nimeshasema nataka kwenda kusoma na Jafet, mtanishughulikia masuala ya uhamisho, sitaki kukaa mbali na Jafet,” alisisitiza Anna na kuwafanya wazazi wake wabaki wakitazamana.

“Hebu njoo mara moja ndani mke wangu,” alisema baba yake Anna huku akiinuka, muda mfupi baadaye mkewe naye akainuka na kumfuata mumewe.

“Umemsikia Anna, sasa tutafanyaje?”

“Mh! Hata sielewi mume wangu.”

“Unakumbuka kwamba Jafet tayari alikuwa na uhusiano na msichana mwingine na tulifanya kwenda kumuomba tu ‘aekti’ kumpenda Anna kwa ajili ya kumsaidia apone haraka, jambo ambalo limetimia. Sasa tutafanyaje?”

“Tukisema Anna aende na Jafet Dar, tutasababisha matatizo makubwa kwa sababu yule msichana mwingine wa Jafet wanasoma wote chuo kimoja.”

“Unaonaje kama tukiwapeleka wote Marekani kwenye chuo alichokuwa anasoma Anna ili wakaendelee pamoja?”

“Mazingira hayo ya chuoni si ndiyo yamesababisha Anna akapatwa na matatizo makubwa? Siwezi kuruhusu mwanangu arudi kwenye kile chuo tena.”

“Basi tuwatafutie chuo kingine hukohuko nchini Marekani wakasome pamoja kwa sababu naona kama Jafet haigizi tena kumpenda Anna bali anampenda kwa dhati. Gharama zote za Jafet tutagharamia sisi na hili ni miongoni mwa mambo tutakayoenda kuzungumza na wazazi wake.”

“Sawasawa, wazo zuri sana.”

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

7 Comments
  1. winnie lucas says

    Dah naumia kuhusu sulhea but mapenzi ndivyo yalivyo….pole sana sulhea ndiyo ushaachwa

  2. Makongoro says

    Wazaz wa Anna ni wabinafsi…wanafany hayo yote il mtoto wao awe salam bt angekuw jafet anayeumwa wacngethubutu…

  3. mpajiel says

    kwaheri suleikha

  4. LADY SUBY says

    Daah it’s real unending love…napenda Japhet aendelee na Anna coz si dhumuni la Anna kusaliti ni ushawishi tu ila alikuwa na true love kwa japhet

  5. Deborah says

    Ipo vizur. . .

  6. Bullah says

    safi jamni story tamu sanaa uwii….

  7. Bullah says

    story tamu jamn anna anavishawishi khaa…..

Leave A Reply