The House of Favourite Newspapers

Unending Love -(Penzi lisiloisha)-80

4

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.
Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.
Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa msichana huyo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.
Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.
Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India.
Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Wanafunga safari ya kurejea Tanzania na hatimaye wanawasili jijini Mwanza ambapo mjadala mkubwa unaendelea kuhusu hatima ya wawili hao.

Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
“Basi tuwatafutie chuo kingine hukohuko nchini Marekani wakasome pamoja kwa sababu naona kama Jafet haigizi tena kumpenda Anna bali anampenda kwa dhati. Gharama zote za Jafet tutagharamia sisi na hili ni miongoni mwa mambo tutakayoenda kuzungumza na wazazi wake.”
“Sawasawa, wazo zuri sana.”
Baada ya majadiliano hayo, wazazi wa Anna walitoka hadi sebuleni walikoowaacha Anna na Jafet. Baba yake Anna akamuita Jafet na kutoka naye nje, wakawaacha mama na mwanaye nao wakizungumza yao.
“Anna mwanangu.”
“Abee mama.”
“Kwani unampenda sana Jafet eeh?”
“Kuliko kitu chochote mama, yaani hata ukiupasua moyo wangu utakuta amejaa yeye.”
“Lakini si unajua kwamba umri wako bado ni mdogo na unapaswa kuelekeza nguvu zako kwenye masomo?”
“Mama mimi nimeshakuwa mkubwa. Halafu isitoshe mbona mimi na Jafet tulifahamiana tangu tuko sekondari na tuliweza kusoma vizuri mpaka wewe ulipokuja kutuingilia kati? Umesahau kwamba Jafet ndiye aliyesababisha hata darasani nianze kuelewa na kufaulu mitihani yangu?”
“Ni sawa unachokisema lakini unafikiri kuna mzazi anayeweza kumruhusu mwanaye kuwa na uhusiano wa kimapenzi kabla ya kuingia kwenye ndoa? Umeona matatizo uliyoyapata baada ya kunasa ujauzito? Unataka kurudia tena mambo yaleyale?”
“Lakini ujauzito haukuwa wa Jafet, isitoshe mimi na Jafet hatujawahi kukutana kimwili na tuliwekeana ahadi kwamba hatutafanya hivyo mpaka siku tutakayofunga ndoa. Naomba usifanye kama ulivyofanya mwanzo mama ukasababisha nikatengana na Jafet wangu, sitakubali,” alisema Anna huku sauti yake ikianza kubadilika, akajiinamia chini huku machozi yakianza kumtoka.
“Basi usilie, si unakumbuka madaktari India wamekwambia hutakiwi kuwa na msongo wa mawazo?”
“Wewe unasababisha niwe na msongo wa mawazo mama, hata sijui nilikukosea nini.”
“Siyo hivyo mwanangu, haya yote ninayoyafanya ni kwa ajili yako, nakupenda ndiyo maana nakulinda.”
“Hunipendi mama, usingenifanyia haya uliyoyafanya, kama Jafet asingekubali kuja India si tayari ningeshakuwa nimekufa? Hunipendi,” alisema Anna, safari hii kilio kikawa kinasikika kwa nguvu, hali iliyomfanya mama yake ajiinamie kwani nafsi yake ilikuwa ikimsuta.
“Basi mwanangu usilie, naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea,” alisema mama yake Anna huku nafsi yake ikimsuta kwani alishayajua makosa yake. Akamsogelea mwanaye na kumkumbatia, akawa anambembeleza na kumuahidi kwamba kuanzia siku hiyo, atamuunga mkono kwa chochote atakachokuwa anakitaka.

Upande wa pili, Jafet na baba yake Anna nao waliendelea na mazungumzo yao ya kiume, mzee huyo akamueleza kuwa wameamua kuwatafutia chuo kingine nchini Marekani ambako wote wawili wataenda kuendelea na masomo yao kuanzia pale walipokuwa wameishia.
“Kwangu mimi hakuna tatizo, lakini unafikiri wazazi wangu watakubali? Na pia vipi kuhusu Suleikha?”
“Kuhusu wazazi wako hilo niachie mimi lakini kuhusu huyo Suleikha, wewe ni mwanaume, utajua mwenyewe cha kufanya. Cha msingi tunakuomba sana utusaidie kuhusu hili suala la Anna,” alisema baba yake Anna na kumfanya Jafet ashushe pumzi ndefu na kujiinamia.
“Ok sawa nimekuelewa baba, nipo tayari kwa chochote ilimradi nimuone Anna akiwa na furaha.”
“Nimefurahi sana kusikia hivyo Jafet, maisha ya Anna yapo mikononi mwako, nakuomba umlinde,” alisema baba yake Anna na kumkumbatia kwa nguvu Jafet huku akimpigapiga mgongoni kwa furaha. Baada ya kufikia muafaka, walirejea ndani ambako walishangaa kuwakuta Anna na mama yake nao wakiwa wamekumbatiana wakibembelezana.
Ikabidi baba yake Anna ampe ishara mkewe, akainuka na kuelekea chumbani, na yeye akamfuata na kuwaacha Anna na Jafet sebuleni.
“Nini kimetokea tena jamani, kwa nini unalia?”
“Mama ndiyo amesababisha yote haya, lakini leo nimemueleza ukweli.”
“Amesababishaje na umemueleza ukweli gani?”
“Yeye ndiye aliyesababisha mimi na wewe tukatengana. Nimemueleza ukweli kwamba sitakubali kumuona akitutenganisha tena,” alisema Anna, kauli iliyomfanya Jafet acheke sana.
“Sasa mimi naongea na wewe unacheka. Kwa hiyo mimi nimekuwa katuni si ndiyo?”
“Sijamaanisha hivyo Anna, baba yako alikuwa ananiambia kitu hapo nje, si unaona tumekaa muda mrefu sana,” alisema Jafet, Anna akakaa vizuri huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ataambiwa nini.
Jafet alipomuelekeza walichokuwa wakizungumza, msichana huyo alishindwa kuficha hisia zake, akafurahi mno na kumkumbatia Jafet kwa nguvu huku akimuaangushia mvua ya mabusu.
“Huyo si ndiyo muda mfupi uliopita alikuwa analia? Unasikia anavyofurahi? Kila shetani ana mbuyu wake,” alisema baba yake Anna na kumfanya mkewe akose cha kujibu.
“Hawa wanapendana kwa dhati, hakuna kinachoweza kuja kuwazuia kwa sababu penzi lao halina mwisho, cha msingi ni kuwaongoza ili hatimaye waje kuishi kama mume na mke.”

“Mh! Nimeanza kuamini unachokisema, watoto wana mambo hawa!” alisema mama yake Anna na kumkumbatia mumewe kwa furaha. Siku hiyo ilipita vizuri, kama walivyokubaliana, kesho yake waliianza safari ya kuelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa wazazi wa Jafet. Kama kawaida, baba yake Jafet ndiye aliyekuwa akiendesha huku mkewe akiwa pembeni yake.
Siti za nyuma walikaa Anna na Jafet ambao muda mwingi walikuwa wakipiga stori za hapa na pale, huku mizigo mingi ikiwa imehifadhiwa kwenye buti kama zawadi kwa wazazi wa Jafet.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

4 Comments
  1. david moses says

    Tht’s what love is,i wl b happy kama japhet atamuoa anna

  2. Queengunda Stephee says

    Hongera baba Anna kwa kuweza kuwaweka Japhet na Anna pa1 na pia kumbadilisha mkeo ili ajuw what true love is. “”

  3. Sylvester says

    itakuwa poa Sana wakioana

  4. alex rodrick says

    penzi la kweli alijifichi? jamani

Leave A Reply