The House of Favourite Newspapers

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-9

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Walishuka wote, wakawa wanaingia huku wameshikana mikono na kutafuta mahali pa kukaa…
“Shemeji Bony,” aliita Nancy ambaye kwenye ndoa ya Bony na Neema yeye alikuwa matroni…
Bony aliachia mkono wa Aisha haraka sana…
SHUKA NAYO MWENYEWE…

“Vipi shem, za siku?” Bony alimsalimia Nancy huku macho yake yakijaa aibu na moyo ukimdunda kwa wasiwasi, alijua amechemsha na mambo yameharibika…
“Nzuri shem…za siku na wewe..? Anti mzima..? Yaani namshukuru Mungu nimekuona shem, juzi nilipoteza simu yangu, nimenunua nyingine na kurinyuu laini, nipe namba yako na ya Neema,” alisema Nancy akimwangalia Aisha kwa macho yaliyojaa maswali juu yake kwani baada ya kumsalimia ‘anti mzima?’ Aisha hakumjibu kitu.

Naye Aisha aliposikia Nancy amemuita Bony shemeji, alijiongeza na kujua kuwa, mrembo huyo na Neema ni ndugu, hakujua kuwa ni marafiki tu na alikuwa matroni wake…
Bony alimtajia namba zote, zake na za Neema huku mikono ikimtetemeka kwa mbali…
“Asante shemeji, mimi namsubiri rafiki yangu,” alisema Nancy huku akimkazia macho Aisha.
Bony na Aisha walikwenda kukaa kwenye meza nyingine. Baada ya kukaa tu, Bony akaanza…

“Aisha,” aliita…”
“Abee…”

“Tumekwisha mpenzi wangu…yule alikuwa matroni kwenye harusi ya Neema, pale kaomba namba za simu nilitamani nimwambie ya Neema sina, basi tu.”
Aisha alihema kwa nguvu, akaangalia upande aliokaa Nancy, akamwangalia Bony na kusema…
“Ina maana anaweza kusema?”
“Hilo nalipa mia kwa mia kwani ni rafiki wa siku nyingi wa Neema na amekuwa akimlalamikia kwa umbeya…”

“Mh! Na mimi na mtu mwongomwongo simpendi,” alisema Aisha…
“Yule si mwongomwongo Aisha, ni mbeya.”
“Kwani kuna tofauti?” aliuliza Aisha…
“Kubwa tu Aisha! Mwongo ni mtu anayesema habari za watu ambazo hazipo, mbeya ni yule anayesema habari za watu ambazo zipo lakini hakutumwa kusema.”
***
Nancy alipomaliza kusevu namba za simu za wawili hao, palepale alimpigia simu Neema…
“Nancy,” Neema alipokea kwa staili ya kuita jina.
Waliongea mengi kama marafiki na kama mtu na matroni wake, kisha Nancy akaanika kuhusu kupoteza simu na namba yake na namna alivyozipata siku hiyo.

Baada ya kukata simu na Neema, Nancy alijifikiria sana kuhusu mwanamke aliyekuwa na Bony na kwa nini walikuwa wameshikana mikono…

“Au mchepuko wake? Itakuwa mchepuko, mimi sijawahi kumwona nyumbani kwa Neema hata siku moja…halafu aliponiona tu, akamwachia mkono, kwa nini?” alijiuliza Nancy huku akiinua shingo ili kuona kama anaweza kuwaona walikokaa.
Moyo haukutulia, akamtumia meseji Bony…
“Shem…”

“Shem,” Bony alijibu haraka sana…
“Huyo ndiyo mke mwenzetu au?”
Bony alitetemeka, hakujua kama Nancy ameshaongea na Neema, akajua anauliza ili kuweka sawa mizani ya habari kisha awasiliane na Neema…
“Shem please! Please! Please! Usije ukamwambia Neema kuhusu huyu dada wala tulipokutana, please!” alituma meseji Bony akijilipua kwani mwelekezo wa alikoaga anakwenda ni mwingine kabisa na alikokutwa na Nancy…

“Haa! Shem, mbona nimeshaongea naye,” alijibu Nancy.
Palepale, Bony alisimama huku akimwambia Aisha…
“Yule demu ameshatibua kila kitu, kanitumia meseji hapa eti amemwambia Neema mimi niko na mwanamke, ngoja nikamuweke sawa.”

Aisha hakujibu lakini moyo haukuwa sawa. Mapigo yake yalikuwa yakipiga kama midundo ya ngoma kwenye sherehe. Moyoni aliwaza…
“Kama amemwambia nilivyovaa siri yote nje, amejua ni mimi tu ndiyo niko na mumewe.”
Kila sekunde, Aisha alikuwa akitupia macho simu yake akijua Neema atapiga au atatuma meseji ya kumuuliza aliko.

***
“Vipi tena shem?” Nancy alimuuliza Bony baada ya kumwona akifika kwenye meza yake na kukaa huku uso wake ukikosa uchangamfu anaoujua…
Itaendelea kwenye Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa ijayo.

Leave A Reply