The House of Favourite Newspapers

Usiyoyajua kuhusu ugonjwa wa kisukari

WASOMAJI wengi wa safu hii wamenitumia sms na kutaka kujua chanzo cha mtu kuugua kisukari, wengine wanadhani kula sukari nyingi husababisha ugonjwa huo.  Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwavunjwa tumboni na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu.

Wakati chakula kinapoyeyushwa tumboni matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari inayoitwa glucosi ambayo ni chanzo cha nishati/ nguvu mwilini huingia katika damu. Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho, kitaalamu Pancrease kutengeneza kichocheo cha insulini.

Kazi ya insulini ni kuondoa glucosi katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumika kama nishati. Watu wenye kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu.

Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo; huenda kongosho zao haziwezi kutengeneza insulini ya kutosha au seli za mwili wao haziathiriwi na insulini kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili.

Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa wa kisukari lakini kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito wa kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti.

Ugonjwa wa kisukari umeitwa ni ugonjwa unaoathiri kiini cha nishati ya mwili. Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha kifo. Ugonjwa wa Kisukari kitaalamu hujulikana kama ‘DIABETES MELLITUS’.

Jina ‘Diabetes Mellitus’ linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha ‘kunyonya’ na neno la Kilatini linalomaanisha ‘tamu kama asali’.

Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari.

Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.

Watu walio katika makundi yafuatayo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kisukari: Wenye uzito uliozidi, wenye historia ya kuwa na wagonjwa wa kisukari katika familia zao, wanawake waliozaa watoto wenye kilo 4 au zaidi, watu wasiojishughulisha au wasiofanya mazoezi, wenye shinikizo la damu, wenye msongo wa mawazo na wenye matumizi makubwa ya pombe na sigara.

Kutokana na hili, watu hawa wanashauriwa kupima sukari yao kila mwaka wakiwa na umri wa miaka 45 na kuendelea. Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi katika tumbo na kiuno chake kuliko katika mapaja yake. Mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu.

Wavutaji wa sigara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani zoezi hilo hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu. Asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.

DALILI ZA KISUKARI

Dalili kubwa ni kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati, kwenda haja ndogo mara kwa mara, watoto kukojoa kitandani, kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.

Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri ni dalili nyingine pia kusikia njaa kila wakati na kula sana, kutoona vizuri, wanaume kupungua nguvu za kiume na wanawake kuwashwa ukeni, au kukosa hamu ya kujamiiana kwa wanawake.

Dalili nyingine ni kuhisi ganzi miguuni, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole. Miguu kuoza, kukaukwa na ngozi. Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka, majipu mwilini.

TIBA NA USHAURI

Kuna dawa za kisukari ambazo husaidia kupunguza tatizo au kuondoa ikiwa utawahi kupima na kuanza kutumia dawa. Wenye dalili hizo wanashauriwa kupima sukari ili kubaini kama wana kisukari.

Comments are closed.