The House of Favourite Newspapers

Utatakaje upendwe wakati mwenyewe hujipendi?-2

0

vegeterians-couple-bedUhali gani msomaji wangu, nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu kwenye ukurasa wetu huu mzuri.

Wiki iliyopita tulianza kujadiliana kuhusu mada hii kama inavyojieleza. Nilikwambia kwamba nimeamua tujadiliane kuhusu umuhimu wa kujipenda kwanza kabla hujaanza kumpenda mtu mwingine kutokana na malalamiko niliyokuwa nikiyapokea mara kwa mara kutoka kwa wasomaji wangu.

Leo tuendelee na mada yetu kuanzia pale tulipoishia. Bila shaka umeelewa kujipenda maana yake nini. Nasisitiza tena, itakuwa sawa na kazi bure kujitahidi kumpenda mwenzi wako kwa moyo wako wote wakati wewe mwenyewe hujipendi.

Kitu kinachowasumbua wengi, anataka akimpenda mwenzi wake na kumuonesha mapenzi ya dhati na yeye arudishiwe mapenzi vilevile kama yeye anavyotoa. Hata hivyo, siyo sahihi kutegemea mwenzi wako naye akupende kama unavyompenda.

Badala ya kukaa kusubiri kuona naye anakurudishia mapenzi ya dhati kama unayompa, unachotakiwa kufanya ni kujipenda wewe kama unavyompenda yeye, au pengine hata zaidi ya hapo. Upendo una kawaida ya kuvutana, yaani mtu anayejipenda ni rahisi sana kupata mtu ambaye atampenda kwa moyo wake wote.

Upendo huwa haujifichi, kwa maana mtu anayejipenda huwa ni rahisi sana kumtambua na hata mtu asiyejipenda pia ni rahisi kumgundua kwa kumtazama tu. Hutakiwi kujikatia tamaa, kama kwa kipindi kirefu ulikuwa huoni umuhimu wa kujipenda, anza leo.

Hakikisha muda wote unajifanyia mambo mazuri wewe kwanza, baada ya hapo ndiyo umfikirie mwenzi wako.

Kama unajipenda, hata ikitokea mwenzi wako akawa hakuoneshi mapenzi kama unayompa, au akakutenda, bado utakuwa na ujasiri mkubwa wa kusonga mbele kwenye maisha yako bila kutetereka.

Hujawahi kuona mtu anakuwa ‘rafurafu’, anashindwa kuoga, kuvaa vizuri, kula au hata kufanya kazi kwa sababu tu ameachwa na mpenzi wake? Hawa ni wale ambao badala ya kuanza kujipenda wao kwanza, walielekeza nguvu katika kuwapenda wenzi wao.

Au hujawahi kuona mtu anayakatisha maisha yake kwa sababu amemfumania mwenzi wake au kwa sababu amegundua kwamba amesalitiwa? Inafahamika kwamba maumivu ya mapenzi yanatesa sana moyoni lakini kama unajipenda, huwezi kukubali kuendelea kuteseka au kuyakatisha maisha yako eti kwa sababu tu mtu fulani amekutenda, amekuumiza au amekuacha.

Katika kila unachokifanya katika uhusiano wa kimapenzi ni lazima ujitangulize wewe kwanza, jipende na kujithamini kwa uwezo wako wote ndipo utakapoweza kumpenda mwenzi wako kwa dhati, na kumfanya naye akupende maisha yake yote.

Hakuna mtu ambaye hapendi kuwa na mwanaume au mwanamke anayevutia, msafi, anayejipenda na kujitunza. Ili huyo uliyenaye aendelee kukupenda ni lazima ujipende wewe kwanza. Ukijipenda siku zote utakuwa unavutia, msafi na unayependeza.

Neno la mwisho ni kwa wanawake, wengi wanapokuwa kwenye hatua ya kulea watoto wadogo, huwa wanajisahau sana katika suala zima la kujipenda na kuelekeza nguvu na akili zote kwa watoto. Hawakumbuki tena kujipamba na kupendeza wala kuwa na mwonekano utakaowafanya wenzi wao waendelee kutamani kuwa nao karibu. Hata kama unanyonyesha, jipende na jithamini, ukizingatia haya, mateso ya kimapenzi utakuwa unayasikia kwa wenzako tu.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Leave A Reply