The House of Favourite Newspapers

Viongozi wa Dini Walia na ‘Vimini’ vya Wadada

0

KASI ya matukio ya ubakaji nchini yamesababisha Baraza la mahusiano ya dini mbalimbali kwa ajili ya amani nchini kutoa wito kwa viongozi wa dini zote nchini kuamka na kukemea vitendo hivyo ikiwamo ndoa za utotoni.

 

Pia wameiomba serikali kuanzisha mfumo wa kisheria ambao utapiga marufuku uvaaji wa sketi fupi ‘vimini’ kwa wanawake na mavazi mengine yasiyo na stara kwa jinsia zote ili kutokomeza kasi ya matukio ya ubakaji nchini.

 

Kauli hiyo imekuja kufuatia ongezeko la matukio ya ubakaji kwa wasichana kuzidi kuongezeka ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizoripotiwa katika vituo vya polisi, zaidi ya wasichana 22,000 wamebakwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2017.

Akizungumza katika warsha ya viongozi wa dini nchini iliyoandaliwa na Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni (TECMN), Mwanasheria kutoka katika mtandao huo, Fundikila Wazambi alisema takwimu hizo zinaonesha kwa mwaka wasichana 4,500 wanabakwa.

 

Katibu wa baraza hilo ambaye ni Paroko wa Parokia Magomeni, Likoko Nyumayo alisema tatizo hizo la mavazi limekuwa likiongezeka kila kukicha jambo ambalo linadhihirisha jamii inazidi kupotoka.

 

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mchungaji Erika Ludela ambaye alisema akina mama wanatia aibu kutokana na kuwavalisha watoto wadogo wa kike vimini ambavyo hata jamii inayowazunguka inawashangaa.

 

“Niliwaita wazazi wa jinsia zote mbili, akina baba na mama, kwa kweli akina baba walikiri kuwa akina mama wanawanunulia na kuwavalisha watoto vinguo vinavyowabana.

“Haya ni mambo ya kuiga ambayo hayana maadili kwa jamii zetu, lazima kina mama wabadilike, mimi ni mwanamke ila ninakerwa sana kuona watoto wadogo kabisa wamevalishwa vinguo vya ajabu na mwisho wa siku wakiwa wasichana wanaendeleza tabia hiyo na kuchochea matendo ya ngono,” alisema.

 

Naye Imam wa Msikiti wa Magomeni, Mursalina Mavere alisema kutokana na hali hiyo, umefika wakati sasa kwa serikali kuandaa sheria ambayo itakaza kabisa uvaaji wa mavazi ya aina hiyo yasiyo na stara.

 

“Kwa sababu ni jambo la aibu unapita mtaani unakutana na watoto, wasichana na wanawake wakubwa ambao wamevaa mavazi ambayo yanaamsha ashki za wanaume, sasa si wote wenye hofu ya Mungu, wengine ndio hao wanazidiwa na kubaka,” alisema.

 

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao huo, kutoka Jukwaa la Utu wa motto (CDF), Michael Jackson alisema mtandao huo umedhamiri kuwatumi viongozi wa dini kushirikiana na jamii kutokomeza ndoa za utoto.

“Ili kufikia Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025. Ni wajibu wa jamii kwa ujumla kuachana na mila hatarishi kama ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia, mambo yanayochangia kukandamizwa, na kurudisha nyuma maendenel ya mtoto wa kike.” Alisema.

 

Aidha, Mkuu wa Mawasiliano na Utetezi kutoka Plan International alisema Desta Laiser alisema “Hatusemi mtoto wa kiume ameachwa nyuma, lakini mtoto wa kike ameminywa zaidi. Mtoto wa kike anapitia changamoto nyingi mfano ubakaji, ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.”

 

Wakati mmoja wa maofisa utetezi kutoka taasisi ya Msichana Initiative, Karen Paul alitoa wito kwa serikali kutekeleza haraka maboresho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa kuwa imekuwa ikiendelea kumkandamiza motto wa kike.

NA GABRIEL MUSHI

Leave A Reply