The House of Favourite Newspapers

Waganda wampa mtihani wa kwanza Omog

0

Joseph-Marius-OmogKocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog.

Na Wilbert Molandi

TIMU ya URA ya Uganda imetajwa kuja nchini kwa ajili ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba inayonolewa na Mcameroon, Joseph Omog.
Mechi hiyo, ni kipimo cha kwanza cha kocha huyo ambaye Agosti 8, mwaka huu atatarajiwa kukaa kwenye benchi la timu hiyo akiiongoza Simba ikivaana na URA, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo, ina wiki ya tatu tangu iweke kambi yake huko Morogoro, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuanza Agosti 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezinasa, timu hiyo imepanga kucheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa kwa ajili ya kukipima kikosi hicho na mchezo wa kwanza itacheza na URA siku ya ‘Simba Day’.
Mtoa taarifa huyo, alisema mchezo huo wa kirafiki utakwenda sambamba na utambulisho wa wachezaji wao wapya waliowasajili ambao ni Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Mzamiru Yassin na Hamad Juma.
Aliongeza kuwa, mara baada ya mechi ya URA, timu hiyo itacheza michezo mingine miwili ya kirafiki hivi karibuni na timu kutoka nje ya nchi ambazo bado hazijathibitisha ujio wao.
“Benchi la Ufundi la Simba limependekeza tucheze mechi tatu za kirafiki za kimataifa tofauti na za hapa nchini tutakazocheza nazo wakati wowote kuanzia hivi sasa.
“Kwa kuanza, tutacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya URA ambayo ina nafasi kubwa ya kuja hapa nchini kwa ajili ya kucheza mchezo huo na hiyo ni kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa katibu mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele, kuzungumzia hilo, alisema: “Ni kweli kabisa Benchi la Ufundi la Simba limependekeza kucheza michezo mitatu au miwili ya kirafiki ya kimataifa.
“Mechi ya kwanza ya kirafiki ya kimataifa tutaicheza siku ya Simba Day ambayo itaenda sambamba na utambulisho wa wachezaji wetu wapya tuliowasajili.
“Timu tutakayocheza nayo bado itajulikana kesho (leo) Jumatatu kwani hivi sasa tupo kwenye mazungumzo nazo, nisingependa kuzitaja timu hizo sasa hivi,” alisema Kahemele.

Leave A Reply