The House of Favourite Newspapers

Wananchi wa Singida Wanajua Lissu Yupo Wapi; Ndugai Hajui!

KAMA kuna jambo lililoshangaza wananchi wa kawaida kabisa wa Tanzania ni tamko la kumvua ubunge Mbunge wa Singida- Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Tumemsikia Spika Job Ndugai akitangaza kumvua ubunge Lissu, hilo hakuna aliyeshangazwa hasa tukizingatia kwamba hata kwenda kumuona wakati anaumwa, hakufanya hivyo.

 

Tumemsikia pia akieleza kosa la kutojulishwa alipo Lissu tangu apigwe risasi 16 na watu wasiojulikana, hilo ndilo lipo midomoni mwa wananchi wakiwemo watu wa Singida.

 

Nilibahatika kupita Singida wakati narejea Dar es Salaam kutoka Mwanza hivi karibuni nikapata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya vijana wa pale. Sijui kwa nini, lakini niliwauliza kimzaha tu kama wanajua alipo mbunge wa mkoa wao, Lissu.

 

Niliwauliza watu saba kwa nyakati tofauti, wote walisema yupo Ubelgiji kwa matibabu. Hapo ndipo akili yangu ikamfikiria sana Ndugai baada ya kumfuta ubunge Lissu na kujiuliza ina maana amekosa kumbukumbu kiasi cha kushindwa na wale watu wa Singida?

 

Sikupata jibu la swali hilo. Uamuzi wake umetufanya tufikiri zaidi na hasa tukikumbuka Ndugai alivyoamua suala la matibabu ya Lissu, alivyoamua suala la mishahara yake na hilo alilofanya ni muendelezo wa kile alichokiamini kuwa kina tija kwake.

 

Lakini wakati haya yanafanyika najiuliza, je, Ndugai amewahi kumpelekea Lissu barua ya kumjulia hali tangu aumizwe?

Siku ya kwanza baada ya kupigwa risasi Lissu jijini Dodoma sijui kama Ndugai anakumbuka alichokisema na wananchi wakamshangilia sana.

 

Aliahidi kusimamia kumtibu, lakini alivyogeuka na kuzungusha suala hilo lilifanya kila Mtanzania mpenda haki amuone anafanya ukatili.

La pili, Ndugai anasema Lissu hajajaza fomu za maadili, kwani hukumu ya kutojaza fomu hizo anatoa Spika? Watu wanajiuliza.

 

Nijuavyo mimi Tume ya Maadili ina adhabu zake kwa mtu asiyetekeleza wajibu huo na wala hilo halihusu Bunge. Inafahamika kuwa hiyo tume inayopokea fomu za mali za viongozi inafahamu Lissu alipatwa na tatizo gani na ndiyo maana hata mwaka jana hatukusikia ikisema chochote juu yake. Au mwaka jana alijaza?

 

Wenye wajibu wa kujibu haya ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ipo ndani ya Tume ya Maadili inayotafsiri sheria ya maadili ya viongozi wa umma na siyo Bunge. Sijawahi kusikia tume hiyo ikimhoji Lissu kuhusu suala hilo.

 

Naamini tume hiyo hawajawahi kumtafuta kwa kuzingatia kuwa awali kabla ya kupigwa risasi hakuwa na tabia ya kutojaza fomu hizo.

Niupongeze mhimili wa mahakama kwa sababu Serikali iliwahi kwenda mahakamani kutaka kufuta dhamana ya Lissu; mahakama ikawakatalia.

 

Najua Ndugai ana familia na wabunge wengine pia wana familia na najua wanafahamu machungu ya kuuguliwa tena kwa kupigwa risasi nyingi, kibinadamu naamini hiyo ni adhabu kubwa kuliko.

 

Nilipigwa na mshangao kuona Spika alipotangaza uamuzi wake huo wa kumvua ubunge Lissu wapo wabunge japo siyo wote, walishangilia! Tuwaulize; walishangilia nini? Walifurahishwa na Lissu kuondolewa ubunge au walifurahi kurejewa uchaguzi au walifurahia kwamba Lissu anakwenda kuishi bila mshahara?

 

Kuna askofu mmoja aliwahi kuhoji, katika historia ya taifa letu Lissu ni kipi ambacho amekifanya kilichoiletea madhara Tanzania hadi aandamwe?

Kurudia ubunge hakuna maslahi kwa taifa badala yake ni kuingiza taifa hasara ya mamilioni ya shilingi ambazo zingeweza kufanya kazi za kimaendeleo.

 

Nichukue nafasi hii kumpongeza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alimtembelea Lissu alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Makamu huyo alikwenda hospitalini humo muda mfupi baada ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, Novemba 28, mwaka jana, hakika wanawake wana huruma.

 

Makamu huyo wa rais aliandamana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Pindi Chana, wote hawa ni wanawake. Tuwapongeze.

Mama Samia ndiye kiongozi wa ngazi ya juu wa Serikali ya Tanzania kumtembelea Lissu miezi mitatu baada ya shambulio, nawaombea huruma zizidi kutamalaki mioyo yao, kushabikia ukatili anaofanyiwa mwanadamu mwenzako ni hatari sana. Tukatae.

 

Lissu anasema anapanga kwenda Mahakama Kuu nchini Tanzania kupinga kuvuliwa ubunge wake.

Lissu ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa ataenda mahakamani muda mfupi baada ya Ndugai, kulitangazia bunge kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi kuileleza kuwa Jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu lipo wazi.

 

Mwanasiasa huyo pia ameiambia BBC kuwa yeye si mtoro bungeni na bado anapokea matibabu barani Ulaya.

“Mimi siyo mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa,” anasema Lissu na kuongeza; “Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo, navuliwa ubunge…”

 

Wakati akitoa taarifa juu ya kuvuliwa ubunge wake Spika Ndugai aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado hana taarifa rasmi ya alipo Lissu na anachokifanya kwa sasa huko alipo.

 

Lakini kama madai ya Ndugai ni ya kweli, kwa nini Lissu au uongozi wa Chadema haukufuata utaratibu wa kulijulisha Bunge hali ya matibabu ya Lissu? Au kwa kuwa Bunge lilimsusa kama wanavyodai? Hapo pana jambo lililo nyuma ya pazia!

Siasa za Siasa | Na Elvan Stambuli

 

JPM: Kenyatta ‘Aniombe Radhi’, Hatukukubaliana Watufunge Mabao 3-2- Video

Comments are closed.