The House of Favourite Newspapers

Waoo..! kama jana vile!-14

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:

Baadhi ya wateja walisikia mazungumzo ya mama Monica na Magembe, wakashangaa kugundua kuwa, kumbe mwanamke huyo jamaa yake wa mchepuko ni huyo.

Mara aliingia yule mteja anayependa pilipili, wasichana wa kazi wakawaangalia mama Monica ambaye naye alimwona mteja huyo akiingia…

“Mapilipili karibu sana.”

SHUKA NAYO MWENYEWE…

Haya asante,” aliitikia mteja huyo na kukaa huku akimwangalia sana Magembe. Lakini Magembe yeye hakuonesha kumwangalia Mapilipili hivyo ilionesha kuwa hamfahamu.

Baada ya kumaliza kula, Magembe alisimama kuondoka huku akichomoa waleti kama kawaida yake. Akatoa mwekundu mmoja na elfu mbili na mia tano, akamuwekea mama Monica kwenye kifua…

“Asante sana baby, kwa hiyo?” aliuliza mama Monica. Sasa alikuwa amejisahau kuwa yeye ni mke wa mtu hivyo kumwita Magembe baby tena watu wakisikia hakuona shida kabisa…

“Nitakupigia baadaye.”

“Haya sawa darling.”

Magembe alipoingia kwenye gari, Mapilipili akamfuata mama Monica…

“Mama Monica huyu jamaa we unamfahamu sawasawa?”

“Kwa nini? Wewe unamfahamu vipi?” mama Monica alimuuliza kijana huyo…

“Huyu jamaa mi namjua, mkewe alikufaga.”

“Alikuwa anaumwa nini?”

“Sijui. Ila aliuguaga kwa muda mrefu. Halafu alikonda sana,” alisema Mapilipili kwa sauti ya umbeya… “Una uhakika?”

“Ndiyo mama Monica.”

“Mbona mimi kaniambia mkewe alikufa kwa ajali ya gari? Tena kanionesha na picha za ajali.”

“Mh! Niamini mimi mama Monica. Kuwa makini naye sana. Halafu anapenda sana mademu, watu wanasema huenda ana ngoma sasa anawaambukiza kusudi baada ya mke wake kufa.”

Mama Monica presha ilimpanda, akaanza kuhisi maneno ya Mapilipili yana ukweli f’lani. Alihisi kifua kujaa upepo.

Alisimama na kufanya kazi zake kwa kujilazimisha ili asahau habari za Magembe lakini wapi! Kichwani alijiuliza…

“Lakini mimi naaminije kuziona picha za ajali! Mbona hajanionesha picha za mkewe akiwa ameshapata hiyo ajali? Kwani si anaweza kuchukua picha ya ajali yoyote ili kujitetea.”

“Mapilipili,” aliita mama Monica…

“Naam.”

“Njoo mara moja.”

Mapilipili alimsogelea mama Monica na kumwangalia kwa macho ya kumsikiliza…

“Hebu niambie…we yule mtu anakufahamu?”

“Sana tu.”

“Mbona hakuonesha kukufahamu wakati unaingia?”

“Kha! Sasa mama Monica yule anajua mimi namjua vizuri. Kunichangamkia ingekuwa ngumu maana si anajua nitakwambia mambo yake.”

“Da! Inawezekana kweli?”

“Ndiyo maana yake. Huamini au?”

“Nitayafanyia kazi maneno yako.”

“Fanyia kazi, utaniambia. Kama umeshaanguka naye basi habari ndiyo hiyo.”

Mama Monica alipaona pale kazini kwake kama jehanamu ya moto, akajikuta akiwaaga wasichana wake…

“Mimi natoka kidogo, hakikisheni wateja wanaandaliwa vizuri kama nipo mwenyewe. Nikisikia malalamiko tutakosana, si mnanijua?”

Mama Monica alipotoa kauli hiyo, Tina Mapepe ambaye alikuwa akipenda sana utani na wakati mwingine kumtania hata bosi wake, alimwambia mama Monica asiwe na wasiwasi juu ya hilo kwani atasimamia kila kitu na mambo yatakwenda sawasawa.

“Wewe jifanye mjuaji lakini ole wenu nikipata malalamiko kutoka kwa wateja wangu kwamba wakati nikiwa sipo hawakupata hudumu nzuri ndipo mtanitambua,” mama Monica alimwambia Tina Mapepe.

“Mama nakuhakikishia hutasikia mteja akitulalamikia tumempa huduma mbovu, wewe nenda uendako kwa amani,” Tina Mapepe alimwambia bosi wake bila kujua kilichokuwa kikimsibu moyoni.

Aliondoka bila kujua anakwenda wapi. Akajikuta akishuka Tip Top na kwenda kukaa kwenye baa ileile aliyokaa na Magembe siku ile.

“Hivi mimi mama Monica na umakini wangu wa muda mrefu, imekuaje mpaka nimekubali kuanguka kitandani na Magembe tena muathirika wa Ukimwi bila kutumia kinga?” mama Monica aliwaza.

Mama huyo hakuishia hapo, alijiuliza itakuwaje mumewe akimhitaji faragha wakati kishaambukizwa virusi vya Ukimwi na Magembe aliyemnasa kirahisi kwa kutumia fedha zake.

“Najuta kufahamiana na Magembe kwani amekwishaharibu kabisa maisha yangu, hii ni aibu kubwa kwa mwanamke aliyeolewa kuanza kuchepuka na kuambukizwa virusi vya Ukimwi!” Mama Monica aliendelea kuwaza hadi aliposhtuliwa na mhudumu aliyemuuliza alihitaji huduma gani.

“Niletee bia ya baridi sana!” Mama huyo alimwambia mhudumu.

“Bia gani?” mhudumu alimwuliza.

“Wewe kalete bia yoyote ila iwe ya baridi sana, zingatia hilo,” mama Monica alimwambia mhudumu.

“Mh! Huyu mama atakuwa na strees zinamsumbua,” mhudumu alijisemea moyoni wakati akielekea kaunta kumchukulia bia mama Monica.

Wakati mama Monica akisubiri kinywaji alichoagiza, alishika simu, akamtumia meseji Magembe…

“Uko wapi?”

“Nipo kazini baby, lakini natoka nakwenda Magomeni mara moja,” alijibu Magembe…

“Unaweza kunipitia hapa kwenye baa tuliyokaa siku ile?”

“Poa nakuja.”

“Akifika hapa ndiyo atanitambua mimi ni nani, hawezi kunidanganya kwamba mkewe alikufa kwa ajali wakati alikufa kwa maradhi ya Ukimwi!” mama Monica aliwaza.

Hata hivyo, alikwenda mbele zaidi na kujiuliza kama hawezi kumshtaki Magembe kwa kuwaambukiza wanawake virusi vya Ukimwi kwa makusudi.

“Nafikiri jambo hilo linawezekana kwani mtu anayewaambukiza watu wengine virusi vya Ukimwi hana tofauti na wauaji wengine, ngoja kesho nitawasiliana na mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kujua kama naweza kumshtaki Magembe,” mama Monica aliwaza.

Baada ya dakika kumi tu, Magembe akafika kwenye baa hiyo na kumkuta mama Monica akinywa bia ya baridi…

“Vipi baby…mmmmwaaa…” Magembe alimbusu mwanamke huyo ambaye hakuonesha uchangamfu wowote zaidi ya kumwangalia tu…

“Nakunywa bia hii kwa ajili yako Magembe…”

“Kisa nini?”

“Maneno niliyosikia kuhusu wewe.”

“Kwamba..?”

“Kwamba mke wako alikufa kwa ngoma na kwamba unapenda sana mademu kwa sababu unawaambukiza virusi vya Ukimwi.”

“Mh! Hayo maneno anakwambia nani wewe mama Monica.”

“Yule kijana Mapilipili. Mbona mwenyewe kasema mnajuana sana.”

“Ni kweli yule kijana aliyeingia namjua. Lakini mimi mke wangu alikufa kwa ajali mama Monica, si nilikuonesha hata picha zake jamani!”

“Picha ni za gari Magembe. Mbona hujanionesha picha za mwili wake baada ya ajali?”

Magembe alitoa simu, akafungua na kwenda kwenye sehemu ya picha ambapo alimwonesha mama Monica picha za mwili wa mkewe ukiwa ndani ya jeneza akiagwa…

“Sasa hapa si anaagwa tu, hata kama alikufa kwa ngoma ni vilevile, anaagwa.”

“Kwa hiyo mama Monica unaamini mimi nina ngoma na nimekuambukiza wewe?”

“Ndiyo. Kama si kweli twende sasa hivi tukapime hospitali ili niamini,” alisema mama Monica na kuanza kulia.

Leave A Reply