The House of Favourite Newspapers

Wateule: ‘Vichwa vya Uswazi Vilivyothibitisha Uwezo’

0

SOLOTHANG

Solo Thang

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakatimuziki wa Kizazi Kipya ukiwa katika mhemko mkubwa, pale Makumbusho, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, vijana kadhaa walikuwa na mazoea ya kukutana katika kijiwe chao kinaitwa Graveyard.

Jay_Mchopnga Jay Mo

Vijana hao, walikuwa ni pamoja na Jafari Ally Mshamu, Taikun Ally, Kevin Kimari na Juma Mohamed Mchopanga ambao walikuwa na kundi lao wakijaribu Hip Hop lililoitwa Sewer Celibacy. Enzi hizo Juma Mcho-panga akijiita Ex-Marhem, Taikun akiwa na jina la JambaziMox na waliobaki wakitumia majina yao ya kawaida.

Ikatokea mwaka 2000, Kituo cha Redio cha Clouds FM kiliandaa tamasha kubwa la muziki ndani ya Ukumbi wa Mambo Club, Oysterbay jijini Dar na ndani ya tamasha hilo kulikuwa na shindano la kusaka vipaji vya kuimba lililosimamiwa na majaji watatu, ambao walikuwa ni maprodyuza wakubwa, Dunga, Master J pamoja na P Funk.

Jafarai

Jafarai

Katika shindano hilo, kundi la Hip Hop la Sewer Celibracy lilichukua nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ilikwenda kwa Msafiri Kondo ‘Solo Thang’, Lady Luu akachukua nafasi ya tatu huku ile ya nne, ikienda kwa Mack Maliki a.k.a Simba a.k.a Mack 2B.

Baada ya washindi kupatikana, Kundi la Sewer Celibacy, Mack 2B pamoja na Solo Thang, walipata ofa ya kutengeneza wimbo wa Hip Hop wa pamoja ndani ya Studio ya Bongo Records chini ya Mtayarishaji P Funk a.k.a Majani.

Wakiwa ndani ya Bongo Records wakisubiri kurekodiwa ngoma yao iliyoitwa Hip Hop na Ragga, Kevin Kimari, mmoja wa wanaounda Kundi la Sewer, alipata wazo na kuwaambiwa wenzake kwa kuwa jana yake waliteuliwa kuwa washindi na kupata nafasi ya kurekodi, basi wajiite WATEULE, lililokubaliwa ndipo ikawa chimbuko la jina la kundi hilo.

MoxMchizi Mox

BONYEZA HAPA KUMSIKIA MCHIZI MOX

Taikun Ally, ambaye baadaye alibadili jina lake la kisanii kutoka Jambazi Mox hadi Mchizi Mox, anasema enzi zao, kundi lao lilikuwa tishio kila walipoibuka kwenye shughuli za kimuziki, hasa kutokana na wao kupenda zaidi kuzungumza Kiingereza.

“Ilikuwa balaa bro, tulikuwa watu wa amshaamsha sana, kila tulipotokea walikuwa wanasema wale watoto wa

Kijitonyama wamekuja, yaani ni simulizi nzuri sana. Enzi zile msanii hawezi kuwa msanii kama hujafika maskani Graveyard, pale ndo kila kitu.

“Ilikuwa hata ukienda kwa P (P Funk) akikuambia subiri uje baadaye, lazima akuelekeze uje pale, atakuambia nenda kwa Wateule kanisubiri, utakaa pale hadi muda wako ukifika unasepa.

“Hapo ndiyo kipindi kile Jay Moe anajiita Ex-Mayhem yaani muuaji mkatili aliyestaafu, Kevin Kimari alijiita Guardian yaani mlinzi mkuu na Mark Maliki akawa anajiita Simba au Mark 2B.”

KUHUSU NYIMBO ZAO

Wateule wanaweza kuwa ni miongoni mwa makundi yaliyotengeneza ngoma nyingi hadi linasambaratika na hapa Mchizi Mox anashuka!

“Tulifanya ngoma nyingi aisee na hadi sasa zipo nyingi tu ambazo zilirekodiwa lakini hazikutoka. Siwezi kuzikumbuka zote lakini ni pamoja na Usipime, Tumerudi Tena, Msela si Mchafu, Bado Yupo Vilevile, Siasa Chafu, Nani Kachafua Hewa, Watu Kibao, Nipende au Nichukie na zingine.

“Zilizosumbua kwa kweli ni nyingi, lakini labda ile ya Watu Kibao, ambayo niliitunga mimi ndiyo ilikamata sana, pia Tumerudi Tena, Msela siyo Mchafu na Usipime nazo zilikimbiza aisee.”

KILA MTU NA ‘PROJECT’ YAKE

LICHA ya kufanya vizuri sana kama kundi, lakini pia Wateule ni miongoni mwa makundi ambayo wasanii wake pia walifanya vizuri sana kwenye ngoma zao binafsi.

Jay Moe Mwishoni mwa mwaka 2001, Jay Moe alijiunga na lebo ya Bongo Records kama solo artist na mwaka uliofuatia albamu yake pekee aliyoiita Ulimwengu Ndiyo Mama iliyokuwa na ngoma kali kama vile Misosi, Mitungi na Pamba aliomshirikisha AY, Safari Njema aliomshirikisha Dudu Baya na Complex, Mpenzi Kwaheri akiwa na TID, Ni Mshamba akiwa na Sir Nature, Kama Unataka Demu akiwa na Q Chillah na Solo Thang.

Nyimbo zake nyingine zilizobamba akiwa solo ni Bishoo, Story 3, Kimya Kimya, Cheza kwa Step, Tingisha, Sihitaji, Famous na nyingine nyingi.

MCHIZI MOX ‘MOOKIE’

Mchizi Mox ambaye sasa alibadili jina la kisanii na kujiita Mockie ambalo hata hivyo limeshindwa kukamata, naye alifanya vizuri kazi zake nje ya kundi, hasa akitingisha na kibao chake matata cha Mambo Vipi, akaja pia na Kinyumenyume aliowashirikisha Mandojo na Domokaya, Nataka

(K-Lynn), Demu wangu (Ngwea) Brand New, Chupa Nyingine na zingine kibao, achilia mbali Wimbo wa Mikasi alioshirikishwa na marehemu Ngwea ambao wakati f’lani, uliwaletea tafrani baada ya kuwa ‘haushikiki’.

SOLO THANG

Msafiri Kondo ‘Solo Thang’ mmoja kati ya wakali wa Hip Hop wa muda wote Bongo, ambaye baadaye aliamua kujiengua katika kundi hilo na kufanya kazi kivyake, aliibuka na albamu kadhaa ikiwemo Kima cha Chini na Kilio Changu.

Miongoni mwa nyimbo alizobamba nazo ni Vina Utata, Mambo ya Pwani, Homa ya Dunia, Sukari Ina Pilipili, Simu Yangu, Wanatamani, Si Ulinikataa, Msako wa Haki, Bongo Trans, Ndani ya Party, Ulingoni na nyingine nyingi.

JAFFARYHEMS ‘Jaffarai’ Jaffari Ally Mshamu naye alifanya kazi nzuri akiwa nje ya kundi ambazo ni pamoja na ile iliyomtambulisha vyema ya Niko Bize, Napenda Nini aliyomshirikisha Fatma pamoja na Demu Wangu aliofanya na TID.

Pia alifanya kazi zingine zilizokimbiza nje ya Wateule kama Blahblah aliomshirikisha marehemu Ngwea, Mcharuko aliofanya na Wyre, Sio Kweli (Lady Jaydee), Toa Hela ambao alishirikiana na Q Chief kabla ya kuachia kibao chake cha mwisho mwaka jana, Wakati.

WAKO WAPI NOW!

Mack Malik ‘Mack 2 B’ ambaye aliimba chorus na pia wakati mwingi akiwa prodyuza (alikuwa pamoja na Enrico kwa muda mrefu) alifariki dunia mwaka juzi wakati Kevin Kimari alishaachana na muziki wa kivile.

Solo Thang yuko zake Ulaya akiendelea na maisha huku akifanya muziki ambao hauvumi sana nyumbani. Jay Moe, Mchizi Mox na Jaffarai wapo wakijichanganya na mishemishe zingine huku wakiendelea na muziki.

Leave A Reply