The House of Favourite Newspapers

Wikiendi ya vita Ligi Daraja la Kwanza

0

Omary Mdose, Dar es Salaam

WIKIENDI hii msimu wa Ligi Daraja la Kwanza 2015/16, unatarajiwa kuhitimishwa kwa kuchezwa mechi 12 katika viwanja tofauti huku timu zote 24 zikishuka dimbani, zipo zinazosaka pointi muhimu huku nyingine zikikamilisha ratiba tu kwani hazina cha kupoteza.

Tayari Ruvu Shooting kutoka Kundi B, imeshajikatia tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku JKT Kanembwa iliyokuwa Kundi C ikiwa ni timu ya kwanza kushuka daraja.
Vita iliyobaki ni ya kutafuta nafasi ya kuungana na Ruvu Shooting na nyingine ni ile ya kuepuka kuifuata JKT Kanembwa.

Katika vita ya kupanda, African Lyon inaongoza Kundi A ikiwa na pointi 26, inafuatiwa na Friends Rangers yenye pointi 23 sawa na Ashanti United inayoshika nafasi ya tatu, lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ndiyo inayowatenganisha.

Mechi zao za mwisho, African Lyon vs Ashanti na Friends vs Kiluvya United, hivyo basi endapo Friends ikiibuka na ushindi na Lyon ikapoteza, Friends inapanda, lakini ikiwa kinyume na hivyo Lyon itapanda.
Kundi C napo kuna kimbembe, Polisi Tabora kwa sasa ina pointi 27, Geita 24, lakini Geita mechi yake iliyopita dhidi ya JKT Oljoro ilivunjika wakati wakiwa wanaongoza 2-0, hivyo inasubiri kauli ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama litawapa pointi za bure au litasema mechi irudiwe.

Kama watapewa pointi watakuwa na 27 na hivyo Jumamosi itajulikana nani kupanda nani kabaki.
Katika mechi zao za mwisho, Polisi Tabora itacheza dhidi ya JKT Oljoro huku Kanembwa ikipambana na Geita, lakini inavyoonyesha Polisi Tabora ina nafasi kubwa ya kupanda.

Vita ya kushuka daraja ipo Kundi A na B baada ya Kundi C kuipata timu iliyoshuka tayari. Polisi Dodoma na Mji Mkuu zote za mkoani Dodoma ndizo zipo kwenye hatari ya kushuka kutoka Kundi A. Mji Mkuu ina pointi sita na Polisi Dodoma pointi saba na mechi zao za mwisho Polisi Dodoma itacheza na Polisi Dar huku Mji Mkuu ikipambana na KMC FC.

Kwa upande wa Kundi B, Kimondo na Burkinafaso mojawapo lazima itashuka. Kimondo ina pointi tisa na Burkinafaso saba. Kila timu itataka ishinde na kumuombea njaa mwenzake na ratiba za mechi zao za mwisho ni Kimondo FC dhidi ya Kurugenzi FC na Burkinafaso FC itacheza na JKT Mlale.
Ikumbukwe kuwa, timu kinara kwa kila kundi itapanda daraja na timu moja ya chini kutoka kila kundi itashuka daraja.

Leave A Reply