The House of Favourite Newspapers

Yanga SC haina plan B, ukiibana imekwisha

0

YANGA (2)
Nicodemus Jonas,
Dar es Salaam
INAWEZA kuwa kweli kwani kiungo wa Prisons, Mohammed Mkopi, amesema wazi kuwa Yanga inakosa njia mbadala katika michezo yake, ndiyo maana wao walitoka nao sare ya 2-2 katikati ya wiki hii.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Yanga ilisawazisha dakika za majeruhi kwa njia ya penalti, mfungaji akiwa ni Simon Msuva na kupata sare hiyo.
Mkopi ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza la Prisons lililofungwa na Jeremiah Juma, kisha akafunga bao la pili kwa kichwa kipindi cha pili.
Akizungumzia na Championi Jumamosi, Mkopi alisema Yanga ilikuwa ishinde mechi yao lakini falsafa yao iliwaponza kwa kiasi fulani, tofauti na wao waliolazimika kubadili staili ya uchezaji kuendana na hali halisi.
“Muda wote wao walikuwa wakilazimisha kucheza soka la pasi, nasi tukawashtukia, tukaamua kucheza soka la pasi za kutanguliza na mashambulizi ya kushtukiza, ndiyo maana mpira kwao ukawa mgumu.
“Sasa sisi tulipobadilika wao Yanga wakaendelea kucheza soka lilelile la pasi nyingi, ndiyo maana walishindwa kabisa kufurukuta tofauti na sisi ambao tulipata mabao mazuri,” alisema Mkopi.
Hata hivyo, Mkopi alisema straika wa Yanga, Donald Ngoma aliwapa wakati mgumu katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja uliojaa maji na matope licha ya kutofunga.

Leave A Reply