The House of Favourite Newspapers

Yanga Wapoteza Matumaini Kombe la Shirikisho Afrika

0

YANGA
Mwandishi Wetu, Ghana
NDOTO za Yanga kufuzu kucheza hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika zimefifia zaidi baada ya jana kufungwa mabao 3-1 na Medeama ya Ghana.
Kutokana na matokeo ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sekodi mjini Takoradi, Ghana, Medeama imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali baada ya ushindi huo kwani imefikisha pointi tano.
Katika mechi hiyo, Medeama ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Abbas Mohamed aliyefunga katika dakika ya sita tu ya mchezo.
Mara baada ya Medeama kupata bao hilo, walionekana kutoridhika nalo badala yake walikuwa wakilielemea lango la Yanga muda wote huku wakionekana kucheza kwa kasi na uhakika.

YANGA (11)
Dakika ya nane, Medeama walipata penalti baada ya nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumchezea vibaya Kwesi Ndosu na penalti kupigwa na Paul Aidoo ambaye alikosa baada ya Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ kuupangua mpira huo.
Wakati mechi hiyo inaendelea, lango la Yanga liliendelea kushambuliwa muda wote huku washambuliaji tegemeo wa Medeama, Enock Atta Agyei na Mohamed wakionekana kushindwa kudhibitiwa na mabeki wa Yanga, Kelvin Yondani na Cannavaro ambao hawakuonyesha kiwango kizuri.
Katika dakika ya 21 ya mchezo huo, Moses Amphonsah aliifungia Medeama bao la pili kwa kichwa baada ya kupokea krosi safi iliyoshindwa kuokolewa na mabeki wa Yanga.

Katika krosi hiyo Yondani alionekana kufanya kosa kwani kama angekuwa makini alikuwa anaweza kuokoa mpira huo.
Dakika ya 24, Yanga ilipata bao lililofungwa na Simon Msuva kwa njia ya penalti baada ya Obrey Chirwa kuchezewa vibaya na Aidoo wa Medeama dakika ya 23.
Mara baada ya kupata bao hilo, Yanga walijitahidi kushambulia wakitafuta bao la pili lakini ikashindikana kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Medeama iliyokuwa inaongozwa na Aidoo na Samuel Adede.
Medeama walihitimisha idadi ya mabao katika dakika ya 36 ya mchezo huo baada ya Mohamed kufunga bao lake la pili, lakini likiwa ni la tatu kwa kwa timu yake.
Mohamed alitumia vizuri uzembe wa mabeki wa Yanga, ambao tena walishindwa kuukoa mpira baada ya Dida kuupangua.
Hadi mapumziko, Medeama walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-1.
Kipindi cha pili, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm aliwatoa Haruna Niyonzima na Yondani na kuwaingiza Juma Mahadhi na Andrew Vicent ‘Dante’.
Mabadiliko hayo, hayakuzaa matunda kwa Yanga licha ya Dante kuimarisha safu ya ulinzi na kuimudu vizuri nafasi hiyo.
Pluijm pia alimtoa Juma Abdul aliyepata majeraha dakika 70 na kumuingiza Amissi Tambwe ambaye alionekana kuleta uhai na kumtengenezea nafasi Msuva aliyepiga shuti kali lililogonga mwamba na mpira kurudi uwanjani dakika 90.
Sasa Yanga wana pointi moja baada ya kucheza michezo minne, huku TP Mazembe ambao wanacheza leo na Mo Bejaia wakiwa na pointi saba kileleni.
Hata hivyo bado Yanga wana mechi mbili ambazo wakishinda zote wanaweza kufuzu kwa bahati.

 

Leave A Reply