The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaanza na Straika Aliyeibeba Stars

ZIKIWA zimebakia siku chache kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, uongozi wa Yanga tayari umeanza harakati zake za kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya kuhakikisha msimu huu timu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

 

Uongozi huo unaiangalia zaidi safu yake ya ushambuliaji ambayo tangu kuanza kwa msimu huu haijafanya vizuri kama mashabiki wengi wa timu hiyo walivyotarajia kutokana na utitiri wa washambuliaji wa kimataifa waliojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumatatu limezipata, zimedai kuwa uongozi huo hivi sasa upo katika mazungumzo na mshambuliaji wa kutumainiwa wa Azam FC anayeichezea Polisi Tanzania kwa mkopo.

 

Mchezaji huyo si mwingine bali ni Ditram Nchimbi ambaye hivi karibuni alifanikiwa kuipiga Yanga hat trick katika mchezo wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Uhuru.

 

Lakini pia kama haitoshi, Nchimbi alifanya kweli alipokuwa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ huko nchini Sudan ambapo aliiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-1 na ikafanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) zitakazofanyika nchini Cameroon, mwakani.

 

Katika ushindi huo wa Stars, bao moja lilifungwa na Nchimbi lakini pia alihusika katika upatikanji wa bao la kwanza lililofungwa na Erasto Nyoni.

“Kutokana na kiwango alichoonyesha katika mechi hizo mbili, ndipo uongozi wetu ulipoona kuwa mchezaji huyo anaweza kutufaa na kuwa msaada mkubwa katika kikosi chetu.

 

“Ana sifa zote za ushambuliaji, ana nguvu lakini pia anajua kufunga, kwa hiyo hivi sasa mazungumzo naye yanaendelea, japokuwa pingamizi kubwa la kumpata linaweza kuwa kwa polisi.

 

“Wanaweza wasiwe tayari kumuachia kutokana na kuwa na mkataba naye wa muda mrefu kidogo,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Walipotafutwa viongozi wa Yanga ili waweze kuzungumzia hilo, hawakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa akili zao zote zilikuwa katika mchezo wa jana wa kimataifa dhidi ya Pyramids ya Misri. Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Tanzania, Frank Geofrey baada ya kuulizwa kuhusiana na mpango huo wa Yanga alisema:

 

“Wao waje tu tuzungumze lakini pia wanapaswa kuzungumza na Azam FC ambao pia nao wana mkataba naye, sisi kwetu yupo kwa mkopo lakini pia tuna mkataba naye.”

Comments are closed.