The House of Favourite Newspapers

Yanga yaenda Mauritius na mchele, unga

0

SIMBA-YANGA-3.jpgKikosi cha yanga

Omary Mdose na Mohammed Mdose
KWA kile kilichoelezwa ni kuepuka hujuma za wapinzani wao, Yanga wamekwenda nchini Mauritius ukiwa kamili huku wakiondoka leo alfajiri na kila kitu cha kwao ikiwemo chakula na maji.
Kikosi cha Yanga chenye wachezaji 21, viongozi saba wa benchi la ufundi na mkuu wa msafara huo akiwa ni Mwenyekiti wa Soka la Vijana wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, ndio waliotarajiwa kusafiri kwa ajili ya mchezo wa awali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, mechi hiyo itapigwa kuanzia saa 9:30 alasiri kwa saa za Mauritius ambapo kwa saa za Tanzania ni saa 8:30 mchana. Mechi ya marudiano inatarajiwa kupigwa wiki mbili baada ya mchezo huo jijini Dar.
“Tumejipanga kukabiliana na hujuma zote, watu tuliowatuma awali kwa ajili ya kuandaa mazingira itakayofikia timu wamefanya kazi yao ipasavyo na tayari sehemu hiyo imepatikana na sisi tutaondoka na kila kitu chetu ikiwemo vyakula na maji.
“Katika msafara huo wachezaji watatu tu hatutaondoka nao kutokana na matatizo mbalimbali, Geofrey Mwashiuya na Benedict Tinoko wao paspoti zao zina matatizo, pia Mateo Simon yeye kwa upande wake hayupo fiti.
“Tumepanga baada ya mchezo wetu huo, tukae kwa muda kujiandaa na mechi yetu ya ligi dhidi ya Simba, kama tulivyofanya mchezo wa kwanza tulipowafunga pia tumepania kuwafunga tena mchezo huu ili kuendeleza rekodi yetu,” alisema Muro.
Hii ina maana kuwa Yanga wataondoka na mchele wao, unga, chumvi, mafuta, vitunguu na kila kitu ambacho kinahusika na chakula pamoja na maji ya kunywa.
Wakati huohuo, TFF kupitia kwa katibu wake, Selestine Mwesigwa, imewapa baraka zote Yanga na wanaitakia kila la kheri kuelekea katika mchezo huo na kusema kuwa wanaamini timu hiyo itafanya vyema kutokana na jinsi ilivyojiandaa huku ikiwa na wachezaji wazuri.

Leave A Reply