The House of Favourite Newspapers

Zijuwe dawa za kisukari na jinsi ya kupimwa

NI vema watu wakapima sukari kwani wataalamu wanatumia vipimo vya damu kudhibiti kisukari (Diabetes).  Tutaeleza jinsi ya kupima na dawa lakini usitumie dawa bila kushauriwa na daktari.

Kutumia kifaa cha kupima sukari kwenye damu (glukomita) na kutumia kipimo cha A1C ni njia mbili za kufuatilia kiwango cha sukari kwenye damu ni muhimu. Njia hizo mbili hutoa taarifa tofauti, lakini zote husaidia. Glukomita ni kifaa rahisi ambacho huonesha kiwango cha sukari kwenye damu dakika hiyo unapopima.

Ni bora zaidi kupima muda tofauti wa siku ili kuona iwapo matokeo ya vipimo yanabadilika kabla na baada ya mlo, na kutoka siku moja hadi nyingine. Unaweza kupima: Kabla ya mlo. Kiwango kizuri ni kati ya 4.4 – 7.2 mmol/l (80 – 130 mg/ dl). Saa 2 baada ya mlo. Kiwango kizuri ni chini ya 10 mmol/l (180 mg/ dl).

Katika kupima, weka tone la damu kutoka kwenye ncha ya kidole kwenye kipande cha karatasi maalum cha kupimia na kiwango cha sukari kitaoneshwa kwenye glukomita. Kutegemea na glukomita, unaweza kuelekezwa kuweka kipande cha karatasi maalum cha kupimia kwenye glukomita kabla ya kuongeza tone la damu kwenye kipande hicho (angalia chini), au unaweza kuelekezwa kuweka tone la damu kwanza kwenye kipande cha kupimia.

Baadhi ya watu wana kifaa cha glukomita nyumbani kwao na wanaweza kujipima mara kwa mara. Wengine hutumia glukomita kwenye kiliniki ya karibu au kwenye kikundi cha kusaidiana cha wenye kisukari.

Glukomita inaweza kutumiwa na watu wengi kwa usalama. Lakini usitumie sindano au kifaa cha kutobolea kwa zaidi ya mtu mmoja kutoa damu- kinaweza kueneza VVU na magonjwa mengine kupitia damu. Kipimo cha A1C (glycosylated hemoglobin test) kinapatikana tu kwenye kliniki au kituo cha afya au hospitali.

Kipimo hiki hukupa wastani wa kiwango cha sukari kwenye damu kwa miezi iliyopita. Hivyo kinaonesha jinsi unavyokidhibiti kisukari chako kwa ujumla, na siyo kwa siku husika tu. Kwa watu wenye kisukari, kiwango kizuri ni chini ya 8.0%. Kama kipimo hiki kinapatikana, jaribu kupima angalau mara moja au mbili kwa mwaka.

Daktari au mfanyakazi wa afya au programu ya kisukari inaweza kutumia namba tofauti kidogo kwa ajili ya hali yako binafsi. Kitu muhimu unachohitaji ni kuuelewa mwili wako, mambo yanayoathiri kiwango chako cha sukari na kiwango gani kinakufanya ujisikie vizuri zaidi.

Itaendelea wiki ijayo. Simu 0754391743.

Comments are closed.