The House of Favourite Newspapers
gunners X

Bashiru Alaani Mauaji ya Makada wa CCM – Video

0

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Bashiru Ally, leo Oktoba 05, 2020, amezungumza na wazee wa Zanzibar kuhusiana na mwenendo wa kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020, ambapo, pamoja na mambo mengine, amelaani mauaji dhidi ya makada wa chama hicho.

 

Baadhi ya mambo aliyoyasema katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi Kisiwandui ni yafuatayo:

 

“Jana tumezika kijana katika  Wilaya ya Chemba aliyeshambuliwa na wafuasi wa Chadema.  Agosti 25 katika pilikapilika za uchaguzi wilayani Momba tulimpoteza kijana mwingine ambaye kichwa chake kilipondwapondwa kama chapati na wafuasi wa Chadema; haya hayakubaliki.

 

 

“Kama alivyotufundisha Mzee Karume na Nyerere kuwa kujitegemea ni kujitawala, kama huwezi kujitegemea basi huwezi kujitawala. Msimamo wetu katika Chama ni kujitegemea.

 

“Kinachonichanganya ni wagombea kuapa na mihuri ya mawakili halafu baadaye wanaishiwa pumzi na kubadilisha watu bila vikao. Shukrani ya punda ni mateke.  Tumeelekezwa kuvumilia na ikiwezekana tuwajibu kwa hoja sio matusi.

 

“Hatuna Mungu wa siasa za chuki. Tuna Mungu mmoja. Tunaomba viongozi wa nyumba za ibada wazuie fitina na chokochoko katika nyumba za ibada. Kuna chama nimesikia wamezindua ilani yao jana. Sasa najiuliza walianzaje kampeni?

 

“Vijana tuutumie ujana wetu vizuri ili tuje kuacha alama, niwahakikishie walimu na watumishi wote wa umma kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaziangalia haki zao na mahitaji yao na kuboresha mazingira mnayotendea kazi. Elimu ni haki ya kila mmoja hapa Zanzibar. Hamna mtu atakayelipa, ila italipwa na kodi zetu wenyewe.

 

“Dkt. Mwinyi alisema ataboresha zaidi pale alipoishia Dkt. Shein  Mgombea wetu, Ndugu Magufuli, alipokuwa Songwe alisema kuwa serikali ya CCM itakaposhinda nafasi ya wazee itapewa kipaumbele.

 

“Kila eneo lina mtu wake na wote wanafanya kazi usiku na mchana. Sisi kikubwa si pesa, kikubwa ni watu. Nawashukuru wazee wetu kwa moyo wenu wa kujitolea. Na hatutumii pesa kuwarubuni wapiga kura. Ni mwiko katika CCM.

 

“Rais Magufuli amenituma anaomba kura zenu, na dua zenu, amenituma nisawalimu sana, na akiwa Songwe alisema CCM ikishinda uchaguzi wa Zanzibar na Tanzania itaendelea kuboresha masuala ya wazee. Dkt. Mwinyi akiingia madarakani atazindua miradi mbalimbali.

 

“Hatuna mpango wa kuungana na yeyote, wala kusaidiana na yeyote, tuna uwezo, tuna wagombea wenye pumzi na stamina, tuna wagombea wenye uwezo wa kuanza na kumaliza kampeni. Wana-CCM tutumie maarifa yetu ili tuzuie harakati zote za kuharibu uchaguzi huu.

 

“Mwezi utaandama na utaandama kwa CCM kushinda kwa kishindo. Kuna watu wamejipanga kuharibu uchaguzi huu. Tushughulike na vibaraka wao. Na jinsi ya kushughulika nao ni kushinda kwa kishindo na wala sio kwa matusi.

 

“Tafiti zinaonesha upo uwezekano wa asilimia 90 kujitokeza kupiga kura. Tujiandae kupokea matokeo mazuri. Kama tulivyoendesha kampeni zetu kistaarabu hivyohivyo ushindi wetu tutaupokea kistaarabu. Iweje tuchonganishwe na watu waliochoka kisiasa?

 

Leave A Reply