Mbunge Peneza: Kwani Mume Wangu Anaenda Bungeni? – Video

 

MBUNGE wa Viti Maalum, Geita, Upendo Peneza (Chadema) amesema kuwa wanaohoji iwapo ameolewa ama la,  hawana haja ya kufanya hivyo kwa sababu hayawahusu na hayo ni maisha yake binafsi wala hayamhusu mtu yeyote.

 

Peneza ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge Vijana katika Bunge la Tanzania amesema hayo wakati akizungumza na Front Page ya +255 Global Radio na kuongeza kuwa, mumewe haingii Bungeni hivyo wananchi wanapaswa kutazama na kufuata kile anachokifanya yeye kama mbunge wao na si maisha yake binafsi.

 

“Kwani mume anaenda Bungeni? Ninayeenda Bungeni si ni mimi!  Hayo ni mambo yangu binafsi, wanipime kwa kazi ninayoifanya Bungeni na sio kuhusu ndoa au mume.

 

Kuhusu wajibu wake kuikumbusha serikali

“Nimewakumbushia tena kuhusu mradi wa maji Geita, suala la umeme nimekuwa nikiongea sana Bungeni. Kuna maeneo ambayo hatuna umeme, Serikali ikakubali na ikasema inatambua na itafanyia kazi.

 

Kuhusu mapambano dhidi ya Corona

“Nimegawa barakoa kwenye vituo vingi Geita Mjini, kama kuna mtu anasema hajapata basi anaweza kuwasiliana na mimi katika muda huu ambao umebaki.

 

“Sisi kama Chadema tumefanya kazi kubwa ya kuikumbusha Serikali kuwahimiza wananchi kufuata taratibu zilizowekwa na WHO (shirika la afya duniani) ili kuhakikisha gonjwa hili la Corona linatokomea. Pia, tumejitahidi sana kutoa elimu kwa wananchi wetu kwa kushirikiana na Serikali.

 

Kuhusu miradi iliyotekelezwa na Rais Magufuli, Geita

“Mimi sio msemaji wa Serikali, wenyewe wamekuwa na nafasi ya kuwasemea yale ambayo wameyafanya. Mimi nina jukumu langu, tunahitaji kuwasemea watu zaidi, Serikali kutenga hela zaidi, kuweka miundombinu mbalimbali. 

 

Kuhusu tuhuma za wabunge wa kike kutoa rushwa ya ngono ili wapewe Ubunge viti maalum

“Mimi kwa mtazamo wangu kuhusu kiongozi kuweza kusema kwamba fulani amepewa nafasi kwa sababu ya rushwa ya ngono utakuwa ni uvivu wa kufikiri. Haya mambo hata kama yapo watu wanayafanya kama extra business.   Tusiwaaminishe mabinti zetu kwamba ukitoa rushwa ya ngono unakuwa kiongozi sio vizuri.

 

Kuhusu Wabunge waliotimuliwa

“Mheshimiwa Wilfred Rwakatare hakuwahi kuwa “Role Model” wangu lakini ni miongoni mwa wabunge ninaowaheshimu ndani ya chama. Kwa wabunge waliotimuliwa Chadema nadhani hakuna haja ya kwenda mahakamani kwa sababu tayari Mheshimiwa Spika amesema atalinda nafasi zao.

 

 “Kama mtu anaona hajatendewa haki kuna nafasi ya kukata rufaa, hivyo kama wale wabunge wenzetu waliovuliwa unachama wanaona hawakutendewa haki, wanaweza kukata rufaa.

 

Unyanyasaji wa kijinsia

“Kuhusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia hili linahitaji elimu pana. Tunahitaji viongozi wa Serikali na  kanisa kushirikiana kwa pamoja tukemee wote ukatili wa kijinsia. Kuna tatizo sana kwa Serikali kutoa elimu, kuna tatizo sana kwa Serikali kutoa elimu kuhusu fursa mbalimbali.

 

Wajibu wa wabunge vijana

“Tukiangalia wabunge vijana bila kujali vyama, tumekuwa tukijitahidi kuwasemea vijana na kuwasikiliza katika shida mbalimbali. Vijana wa bodaboda Geita Mjini nimekuwa nikiwapa elimu, kuwasemea kwa polisi ambao wamekuwa wakiwaonea lakini pia kuwapa elimu vijana hawa wa bodaboda kuhusu usalama wao wawapo kazini,” amesema mbunge huyo.

 


Loading...

Toa comment