The House of Favourite Newspapers

JPM: Uongozi Haujaribiwi Kama Limao, Nitajenga Airport Simiyu – Video

0

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Magufuli amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Simiyu kujenga uwanja wa ndege ili kurahisisha usafiri wa wakazi wa mkoa huo badala ya wao kwenda kupata usafiri huo katika miji ya Mwanza na Shinyanga.

Ametoa ahadi hiyo leo, Agosti 4, 2020, wakati akiendelea na kampeni za kuwania nafasi hiyo na kuwatambulisha madiwani na wabunge wa chama hicho katika mji wa Bariadi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwaka huu.

Baadhi ya kauli muhimu alizotoa Magufuli katika hotuba yake ni:

“Tumeamua kutoa elimu bure ili watoto wetu wasihangaike, hata Ulaya hawasomi bure ndugu zangu. Tumejenga shule za msingi mpya zaidi ya 900, shule mpya za sekondari zaidi ya 200, tumejenga hospitali, tumeongeza upatikanaji wa maji kutoka Ziwa Victoria.

 

“Nilimwambia (Meneja Mkuu wa Shirika la Reli nchini, Masanja) Kadogosa nataka tujenge reli ya umeme kwa ajili ya treni za mwendokasi kama tunazoona Ulaya. Tumekamilisha kipande cha Dar es Salaam – Morogoro sasa tunaendelea na Morogoro – Dodoma, wiki iliyopita tumetangaza tenda kipande cha Mwanza – Isaka. Pesa ipo.

 

“Zao la pamba kulikuwa na shida kwenye malipo sababu soko letu lipo Ulaya, kule walijifungia kutokana na janga la #CoronaVirus, ndege zilizuiwa, meli zilizuiwa watu walijifungia hakukuwa na biashara, serikali tumeona tutoe bilioni mbili na wakulima sasa wanalipwa madeni yao.

 

“Ilani ya CCM imezungumza mengi, ikiwemo barabara za Simiyu kwa sababu tunataka tujenge nchi yenye uchumi wa kwelikweli.  Uongozi haujaribiwi kama limao, uongozi unapimwa, na ninyi wananchi wa Bariadi mmetupima, tupeni miaka mingine mitano tukatekeleze makubwa zaidi.

 

“Simiyu nayo itatengenezewa kiwanja cha ndege, zitakuwa zinatua hapa badala ya ninyi kwenda Mwanza au Shinyanga.  Mtakuwa mnaamua leo uende kwa ndege au kwa barabara, huu ndiyo uchumi tunaoutaka.”

 

Leave A Reply